KILIMO CHA PILIPILI HOHO SEHEMU YA 2
KUTUNZA SHAMBA
a. Kuweka Matandazo
Tandaza nyasi kavu ili kuhifadhi unyevu ardhini, kuongeza rutuba ya udongo, kuzuia uotaji wa magugu, na mmomonyoko wa ardhi.
b. Palizi
Palilia shamba kila magugu yanapoota. Wakati wa kupalilia pandishia udongo kuzunguka shina ili kuifunika mizizi, na kuzuia mmea usiangushwe na upepo mkali.
c. Kumwagilia Maji
Pilipili hoho hustawi vizuri iwapo zimepata maji ya kutosha. Hivyo umwagiliaji wa mara kwa mara hasa wakati wa kiangazi ni wa muhimu.
d. Kuweka Mbolea
Zao hili huhitaji mbolea za kukuzia. Hizi ni kama mbolea ya, S/A, CAN, Urea na mbolea ya mchanganyiko aina ya N.P.K. Mbolea ya mchanganyiko (N.P.K) huwekwa wakati maua yanapoanza kutoka. Kiasi kinachowekwa ni gramu tisa hadi 10 (kijiko kimoja kikubwa) kwa kila mmea. Majuma manne baadae weka CAN, S/A au Urea. Weka gramu 6 (kijiko kidogo cha chai/ kizibo cha soda kimoja) kwa kila mche, kama utatumia CAN au S/A. Ikiwa utatumia Urea, weka gramu tatu (nusu kijiko cha chai) kwa kila mche.
e. Wadudu Waharibifu na Magonjwa
A. Wadudu
(i) Vidukari au Wadudu Mafuta (Aphids)
Hivi ni vijidudu vidogo vyenye rangi nyeusi, kijani au kahawawia.
Hushambuliwa majani kwa kufyonza utomvu wake na husababisha mmea kudumaa.
Vidukari huzuiwa kwa kunyunyizia kama vile Actellic 50 EC, Diclorvos, karate, Dimethoate au Selecron na dawa zingine nyingi.
(ii) Mbawakau
Ni wadudu wenye rangi nyeusi iliyochanganyika na kahawia. Mabawa yao kwa nje ni magumu. Hushambulia shina karibu na usawa wa ardhi au kulifanya liwe na nundu.
Zuia wadudu hawa kwa kutumia mojawapo ya dawa zifuatazo Carbaryl, Dimecron na nyinginezo nyingi.
(iii) Fukusi wa Pilipili (Pepper Weevil)
Mdudu huyu ni hatari sana kwa zao hili na mashambulizi hufanywa na funza wake wenye rangi nyeupe. Funza hawa hula sehemu ya ndani ya vichomozo na matunda machanga na husababisha kuanguka. Angamiza wdudu hawa kwa kutumia moja ya dawa zifuatazo; Actellic, Sumithion au Carbaryl na dawa nyingine nyingi.
(iv) Vithiripi (Thrips)
Hivi ni vidudu vidogo vyenye rangi ya njano. Hushambulia majani na husababisha mmea kuwa na rangi nyeupe yenye kung'aa. Mmea pia hunyauka kuanzia kwenye ncha ya jani. Vidudu hivi hueneza magonjwa yatokanayo na virusi.
Zuia vijidudu hivi kwa kutumia dawa kama vile; Cypermethrin, Sumicidin au Dimecron na dawa zingine nyingi.
(v) Sota (Cutworms)
Hawa hukata miche michanga karibu na usawa wa ardhi. Ili kuwazuia wadudu hawa, tumia dawa kama vile Carbaryl, Sumicidin au Ekalux na dawa nyingine nyingi.
(vi) Inzi Weupe (White flies)
Ni vidudu vidogo vyenye rangi nyeupe, na huonekana kama vumbi la unga vikiwa kwenye majani. Mmea ukitikiswa huruka.
Hushambulia mmea kwa kufyonza utomvu wake, na hueneza ugonjwa wa virusi unaosababisha kujikunja kwa majani.
Inzi weupe wanaweza kuzuiwa kwa kutumia Actellic 50 EC, Sumicidin, Dapa Diazinon au Diclorvos, Karate na dawa zingine nyingi.
(vii) Utitiri Mwekundu (Red spidermites)
Hawa ni wadudu wadogo wenye rangi nyekundu au rangi ya machungwa yaliyoiva. Huonekana upande wa chini wa majani na hushambulia mmea kwa kufyonza utomvu wake.
Zuia utitiri kwa kutumia dawa kama vile Actellic 50 EC, Diazinon, Dimethoate na nyinginezo nyingi.
Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo
Post a Comment