KILIMO CHA BAMIA - SEHEMU YA NNE
12. Semiloopers (Anomis flava) and Leafrollers (Haritalodes
derigata)
Hawa ni aina ya viwavi wanaoharibu majani ya bamia. Aina
zote hizi mbili huharibu majani ya bamia. Aina ya kwanza (Semiloopers), viwavi
hawa hula na hutengeneza matundu kwenye majani, wengine hula sehemu ya chini ya
majani na kuacha ngozi nyembamba ya juu ya jani kubakia (windowing).
Aina ya pili (Leafrollers), viwavi hawa huviringisha majani
pamoja na kuanza kula majani, hatimae majani hujikunja na kudondoka. Viwavi
wanaotoboa majani huleta athari sana kwenye mmea endapo watakua wengi hususani
kwa mimea michanga.
Viwavi hawa wana rangi nyeupe inayong'aa au rangi ya njano
mpauko lakini wanaweza kuonekana kama wana rangi ya kijani endapo wakila na
kumeza majani ndani ya utumbo wao.
A: LEAFLOOPERS
Picha: Kipepeo wa kiwavi (Semiloopers) Photo Credit: www.eagri.org
- Pulizia dawa mbalimbali za asili zitokanazo na Mwarobaini, Pareto n.k au tumia dawa za kemikali zinazopatikana kwenye maduka ya pembejeo za kilimo.
- Chunguza mara kwa mara uwepo wa viwavi hawa, kwa miche michanga unaweza ukawatoa kwa mkono kama shamba lako ni dogo.
13. Flower beetles (Mylabris spp.
and Coryna spp.)
Hawa ni wadudu wanaokula maua ya bamia, hali hii husababisha
uzalishaji wa matunda ya bamia kupungua kwa kiasi kikubwa, vilevile wadudu hawa
hula majani na kubakiza makovu kwenye majani. Viwavi wa beetles hawa hawali
mmea wa bamia bali hula mayai ya panzi, kwa hiyo viwavi hawa ni muhimu sana
kwani huzibiti ongezeko la panzi Kibailojia (Biological Control)
Wadudu hawa(beetles) hutaga mayai kwenye udongo, mayai
yakishaanguliwa hutengeneza viwavi. Viwavi hawa wanatembea sana kutafuta mayai
ya panzi, Wadudu kamili (beetles) ni vigumu sana kuwadhibiti kwa sababu
hawatulii sehemu moja wanatembea tembea sana. Kama beetles hawa wakiwa
wachache, hawaleti athari sana kwenye mmea.
Picha: Flower beetle (Beetle wa maua) Photo Credit: www.treknature.com
Namna ya kuwadhibiti
- Tembelea na chunguza uwepo wa wadudu hawa shambani mara kwa mara.
- Kama shamba lako ni dogo, wakusanye na watoe kwa mkono mara kwa mara kila unapowaona, hii itasaidia kupunguza idadi yao. Ingawaje usiwaondoe wote ila hakikisha wanabaki wa wachache. Vile vile unapokua unawashika hawa beetles hakikisha unavaa gloves kwa sababu wadudu hawa wakisumbuliwa hutoa majimaji yatakayoweza kuunguza ngozi.
- Panda mazao mbadala yenye maua pembezoni mwa shamba
- Pulizia dawa za asili zinazofukuza beetles hawa kama eucalyptus, lantana, kitunguu maji, kitunguu swaumu n.k. Namna ya kuchanganya dawa hizi za asili na maji fwata uwiano ufuatao;
* Changanya gramu 20 hadi 100 za mojawapo ya dawa hizo za
asili kwa Lita moja (1) ya maji. Unachofanya unachukua kiasi cha majani makavu
ya mojawapo ya dawa hizo, unayatwanga kisha unatumbukiza kwenye maji
yanayochemka baadae unayaipua halafu uayaacha yapoe. Yakishapoa unayachuja
halafu unapulizia mimea yako. Dawa hizi za asili zimeripotiwa kufukuza wadudu
hawa shambani.
14. Bugs: Cotton stainers
(Dysdercus spp.)
Wadudu hawa huvamia matunda ya bamia na kusababisha makovu
na madoa madoa yenye rangi nyeusi. Bugs hawa mara nyingi huvamia bamia wakati
mmea ukitoa matunda. Wanaharibu matunda na mbegu zake kwa kutoboa na kufyonza
majimaji yenye chakula, kwa hali hii uzalishaji upungua kwa kiasi kikubwa.
Mimea michanga iliyovamiwa hunyauka na kufa. Wakila kwenye matunda huharibu
mbegu za matunda. Vilevile wadudu hawa huvamia zao la pamba, wadudu hawa
wanakua na urefu wa mm 14 hadi mm 24.
Namna ya kuwadhibiti
- Wakati wa kulima lima vizuri kwa kina cha kutosha ili kuaacha mayai ya wadudu hawa peupe. Mayai yakiachwa peupe juu ya ardhi huharibiwa na Jua.
- Baada ya kuvuna hakikisha una unang'oa mashina yote shambani na kuyachoma moto.
- Majani ya Custard apple yanasaidia sana kuwadhibiti wadudu hawa.
- Zuia uwepo wa wadudu hawa shambani kwa kutumia njia zifuatazo;
*Usafi wa shamba: Ondoa masalia yote shambani mara tu baada
ya kuvuna.
* Hakikisha stoo ya kuhifadhia mazao yako inakuwa safi
wakati wote.
* Kama shamba lako ni dogo, unaweza ukawakusanya kwa mkono
halafu ukawaondoa shambani na kuwaua.
* Tumia kuku kupunguza wadudu hawa, kuku wana uwezo mkubwa
wa kupunguza idadi ya wadudu hawa. Idadi ya kuku 15 wanatosha kuwaondoa wadudu
hawa kwa eneo lenye ukubwa wa hekta 0.1 sawa na mita za mraba 1000 (1000m2) au
Robo akari. Njia hii ni nzuri kama shamba lako ni dogo na likiwa karibu na
nyumbani.
- Tumia njia ya kibailogia kama kutumia wanyama au wadudu wengine wanaokula wadudu hawa kama; Assassin bugs, jamii fulani ya sisimizi au siafu (Ants), buibui, Ndege (kama kuku) na Parasitic flies.
- Mti wa mbuyu ndio mahala pekee ambapo wadudu hawa huzaliana na kustawi vema. Kwa hiyo kama umepanda bamia zako au pamba karibu na mti wa mbuyu jalikisha unapulizia dawa za asili (Biopesticides) au zinginezo kama Pareto (Pyrethrm) n.k.
15. Bugs: Stink bugs (Nezara
viridula, Atelocera sp. and Halydicoris sp.)
Hatua zote mbili za mdudu huyu (Adult na Nymphs) wanakula
kwenye machipukizi, maua, matunda na mbegu za matunda. Wana urefu wa mm 6 - 15.
Wakivamia matunda husababisha makovu yanayopelekea kuwepo kwa mibonyeo kwenye
matunda, pia husababisha mmea kupukutisha matunda.
Namna ya kuwadhibiti
- Tumia dawa za asili kama Mwarobaini, unaweza ukatumia mazao yoyote ya mti huu kama majani, matawi, mbegu, au magome. Chakufanya; baada ya kuchuma au kuandaa mojawapo ya mazao haya, yaanike sehemu yenye kivuli mpaka yakauke, yakishakauka yatwange mpaka yawe unga, changanya na maji kiasi kulingana na uhitaji wako, alafu yachuje ili kuondoa makapi, kicha tumia pampu kupulizia.
- Hakikisha unapulizia mchanganyiko huu wa mti mwarobaini nyakati za asubuhi, kipindi hiki huwa wapo juu ya majani.
- Dawa zingine za asili unazoweza kuzitumia ni kama Pareto, lantana, Kitunguu swaumu (garlic), oleander, African marigold, blackjack, goat weed, wormseed n.k.
Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo
Post a Comment