Kilimo cha Kabichi - Sehemu ya kwanza (Growing Cabbage - Part one)


KILIMO CHA KABICHI SEHEMU YA KWANZA

Kabichi ni zao linalopendelea hali ya ubaridi. Zao hili hustawi na kutoa mazao mengi na bora kwenye sehemu zenye miinuko ya kuanzia mita 1200 hadi 1900 kutoka usawa wa bahari.
Hustawi vizuri kwenye udongo wa kitifutifu wenye rutuba nyingi na uwezo wa kuhifadhi unyevu kwa muda mrefu. Vilevile linaweza kustawi katika aina nyingi za udongo ili mradi udongo huo usituamishe maji na usiwe na chumvi nyingi. Endapo udongo hauna rutuba ya kutosha uongezwe mbolea za asili kama vile mbolea ya kuku, samadi na mbolea vunde.

AINA
Zifuatazo ni aina za kabichi zinazolimwa hapa nchini Tanzania.

1. Prize Drumhead

Vichwa vyake ni vikubwa (Kilo 2.0 mpaka 2.5) na bapa. Huchelewa kukomaa (Siku 110 hadi 120) tangu kupandikiza na hupasuka kirahisi. Aina hii huvumilia hali ya jua kali.


2. Early Jersey Wakefield
Aina hii inazaa kabichi zenye umbo lililochongoka kidogo (koniko) na zinazofunga vizuri. Kabichi moja inaweza kufikia kilo 1.5 hadi 2.0. Hukomaa mapema (siku 90 hadi 100) tangu kupandikiza miche.



3. Copenhagen Market
Vichwa vya Copenhagen Market ni vya mviringo na hupasuka kirahisi. Aina hii pia hukomaa mapema (siku 90 hadi 100) tangu kupandikiza miche.


4. Oxheart
Kabichi zake ni ndogo zilizochongoka mfano wa moyo wa ng'ombe. Zinapendwa sana na walaji kutokana na ladha yake tamu. Hukomaa mapema na hazipasuki.


5. Glory of Enkhuizen
Vichwa vyake ni vya mviringo. Aina hii huvumilia hali ya jua kali, lakini huchelewa kukomaa (siku 110 hadi 120) tangu kupandiza miche na haivumilii hali ya kupasuka.
Aina nyingine ni Brunswick na Danish Ball head



KUBADILISHA MAZAO
Kabichi ni zao linalotumia virutubisho vingi ardhini kulinganisha na mboga zingine. Hivyo kabla ya kustawisha, panda mazao jamii ya mikunde ili kuongeza rutuba. Halikadhalika baada ya kuvuna panda mazao yanayotumia chakula kidogo kama vile Karoti, Radishi au Lettuce. Kubadilisha mazao pia hupunguza kuenea kwa wadudu waharibifu na magonjwa.

Mbegu huoteshwa kwanza kitaluni na baadae miche huhamishwa shambani. Lima vizuri sehemu itakayooteshwa mbegu. Weka mbolea za asili zilizooza vizuri kiasi cha ndoo tano mpaka 10 zenye ujazo wa lita 20 kwa eneo la mita mraba 10. Changanya vizuri mbolea na udongo, kisha lainisha udongo kwa kuvunjavunja mabonge makubwa, kwa kutumia reki au kifaa chochote. Baada ya kulainisha udongo, tengeneza tuta liluloinuliwa kiasi na lenye upana wa mita moja. Mwagilia tuta siku moja kabla ya kusia mbegu ili kuloanisha udongo. Tengeneza mistari katika tuta hilo yenye nafasi ya sentimita 10 mpaka 15 kutoka mstari hadi mstari. Sia mbegu katika mistari hiyo na katika kina cha nusu sentimita mpaka 1.0. Kiasi cha mbegu kinachohitajika ni gramu moja katika eneo la mita mraba moja. 

Gramu 200 mpaka 300 za mbegu zinatosha kupandikiza katika eneo la hekta moja. Funika mbegu kwa udongo au mbolea laini, kisha tandaza nyasi kavu ili kuhifadhi unyevu. Mwagilia maji kila siku asubuhi na jioni mpaka mbegu zitakapoota. Mbegu huota baada ya siku 5 hadi 10. Umwagiliaji utategemea hali ya hewa. Kama kuna mvua hakuna haja ya kumwagilia kila siku.


Makala hii Imehaririwa mara ya mwisho Tarehe: 18/11/2016

Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

Previous Post Next Post