Kilimo cha Nyanya - sehemu ya tatu (Growing Tomatoes - Part three)


KILIMO CHA NYANYA SEHEMU YA 3

Wadudu Waharibifu
a. Funza wa Vitumba (American Bollworm)
Hawa ni funza watokanao na aina fulani ya nondo. Funza hawa wenye rangi ya kijani hutokea baada ya mayai ya nondo kuanguliwa. Kisha hutoboa matunda na kuishi humo. Jinsi wanavyokula na kukua husababisha matunda kuoza. Wadudu hawa wanazuiwa kwa kunyunyiza dawa za kuuwa wadudu zilizopo madukani kama Karate, Actellic n.k


b. Inzi Weupe (White flies)
Wadudu wadogo wapevu na wamefunikwa na vumbi jeupe kama unga. Hufyonza utomvu chini ya majani na kuifanya mimea idumae. Vilevile hueneza magonjwa yanayosababishwa na virusi. Piga dawa za kuuwa wadudu hawa zilizopo kwenye maduka ya pembejeo.


c. Kantangaze (Tuta absuluta)
Huyu ni mdudu kama kipepeo ambaye hutaga mayai juu ya majani, yale mayai yakianguliwa huleta funza ambao huanza kula shina kutokea juu ya majani hadi ndani ya shina kufwata uelekeo wa mizizi. Pia funza huyu huharibu matunda kwa kiasi kikubwa. Funza huyu kadri anavyoendelea kula shina kwa ndani anaendelea kukua, anapokalibia usawa wa ardhi hubadilika na kuwa Buu (hatua hii huwa kama kitu kilicho kufa). Wakati huo mmea hunyauka na kufa. Baada ya muda mchache ile hatua ya Buu hubadilika kuwa mdudu kamili (kantangaze) ambae ataruka na kupaa kuendelea tena kutaga mayai. Kwa sasa dawa za kudhibiti mdudu huyu zipo kwenye maduka mbalimbali ya pembejeo mfano kuna dawa inaitwa "Kantangaze" Piga dawa hii wiki chache baada ya kupandikiza Ili kuwawahi wadudu hawa wakiwa bado hawajataga mayai au kabla mayai hajaanguliwa kuwa Funza muharibifu.



Mayai ya Kantangaze (Picha ya juu)


d. Utitiri (Red Spider Mites)
Hivi ni vijidudu vidogo na vyenye rangi ya machungwa yaliyoiva, nyekundu, au kikahawia. Vijidudu hivi hushambulia kwa kufyonza utomvu chini ya majani. Majani yaliyoshambuliwa huwa na rangi ya njano, hukunjamana, hukauka na hatimaye mmea hufa. Zuia utitiri kwa kutumia dawa mbalimbali zilizopo kwenye maduka ya pembejeo za kilimo.






e. Vidukari/Wadudu Mafuta (Aphids)
Ni wadudu wadogo wenye rangi ya kijani, nyeusi au kikahawia. Baadhi yao wana mabawa na wengine hawana. Hufyonza utomvu wa majani na kusababisha mmea ulioshambuliwa kudhoofika, kudumaa, majani kunyauka na hatimaye kukauka. Wadudu hawa huangamizwa kwa kutumia dawa mbalimbali zilizopo kwenye maduka ya pembejeo ya kilimo kama Selecron, Actellic 50 EC, Karate na nyinginezo.







f. Minyoo Fundo (Root Nematodes)
Ni wadudu weupe wadogo wanaoishi ardhini ambao hawaonekani kirahisi kwa macho. Hushambulia mizizi na kuifanya mimea kudhoofika na kushindwa kutoa matunda. Vile vile husababisha matunda kuiva kabla ya kukomaa. Uking'oa mmea ulioshambuliwa utaona mizizi ina nundunundu. Zuia minyoo fundo kwa kubadilisha mazao. Baada ya kuvuna nyanya, zao linalofuata lisiwe la jamii yake kwa mfano pilipili na bilinganya. Kama madhara ni makubwa sana, tumia Furadan au dawa ya kufukiza ardhi Kama vile Dazomet na Curaterr.



KUMBUKA
Kumwagilia kwa kutumia mifereji kunaweza kusambaza minyoo shambani.

g. Sota (Cut worms)
Hawa ni funza wakubwa wenye rangi ya kijivu. Hupendelea kujichimbia katika udongo wakati wa mchana na kujitokeza wakati wa usiku au asubuhi sana kukata miche michanga karibu na usawa wa ardhi.






Zuia wadudu hawa kwa kutumia majivu au dawa kama vile Cabaryl (Sevin), Fenvalerate (Sumicidin) na Deltamethrin (Decis) mara baada ya kupanda. Kama mche utakatwa mtoe mdudu kwa kumfukua na kumuua kisha pandikiza mche mwingine.

Njia nyingine ya kumzuia mdudu huyu ni kuweka shamba na mazingira yake katika hali ya usafi ili wasiweze kuzaliana kwa wingi. Ikiwezekana tifua udongo bila ya kupanda zao lolote kwa muda wa mwezi mmoja.




Makala hii Imehaririwa mara ya mwisho Tarehe: 18/11/2016

Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

Previous Post Next Post