Jifunze namna ya Kutengeneza Friji ya asili inayotumia Mkaa


Habari ya majukumu ya kila siku ndugu wasomaji wangu? Leo nimekuja na maada kuhusu namna ya kutengeneza friji (Jokofu) ya asili inayotumia mkaa au chenga za mkaa. Sekta ya kilimo cha mbogamboga imekua ikiongezeka kila uchwao, lakini tatizo kubwa linalowakumba wakulima wengi ni jinsi ya kuhifadhi mbogamboga hizo kwani zimekuwa zikidumu kwa siku chache sana, chini ya wiki moja. Kutokana na shida hiyo mkulima anaweza kutumia tekinologia rahisi ya kuhifazi mbogamboga hizo ili kuepukana na uharibifu au kuoza kwa mboga hizo. Friji hii ya asili inatunza mbogamboga hadi mwezi mmoja tangu kuchumwa bila kuharibika na kubaki na ubora ule ule kama imechumwa leo. Pia friji hizi hazihifadhi mbogamboga tu bali hata vinywaji.

Kama ulivyofahamu kwamba friji (jokofu) hii ya aisili inatumia mkaa, mkaa hupatikana kwa kuharibu mazingira yaani kukata miti. Kwa hiyo upatikanaji wa mkaa ufwate taratibu za serikali yaani kupata vibari vya serikali ili kuwepo na upatikanaji endelevu wa rasilimali hii muhimu kwa Taifa letu la Tanzania.

VIFAA VINAVYOHITAJIKA
1. Mbao
2. Nyasi kavu kwa ajili ya kuezekea paa.
3. Wire mesh (waya mesh) yenye matundu madogo yatakayozuia mkaa pamoja na chenga zake kutodondoka.
4. Misumali
5. Bawaba kwa ajili ya mlango
6. Maji

Muhimu*
Kiasi cha vifaa vitakavyotumika itategemeana na ukubwa wa friji yako kulingana na mahitaji. Kuhusu vipimo hivi vya friji hii ya asili unaweza ukatumia vipimo vya friji za umeme za majumbani au za makampuni ya vinywaji hususani hizi za kusimama wima. Kama mahitaji yako ni kufadhi vitu vingi unaweza ukatengeneza friji yenye ukubwa uutakao.

Jambo lingine la kufahamu kuhusu friji hizi za asili ni kwamba hazihami kutoka eneo moja hadi jingine, ukishajenga umejenga labda uibomoe.

HATUA ZA KUANZA KUTENGENEZA FRIJI HII YA ASILI
  • Chagua eneo zuri lililopo mahali salama, haijalishi ni eneo gani pengine kivulini au juani cha msingi ni kwamba hakikisha unachagua eneo ambalo hutaweza kuihamisha friji yako kwenda sehemu nyingine. Ukijenga friji hii ni ya kudumu.
  • Chagua ukubwa wa friji yako kulingana na mahitaji yako
  • Tengeneza ubavu wa pande zote nne za friji yako zenye waya meshi pande zote mbili pamoja na mbao ili kuruhusu nafasi ya kujaza vipande vya mkaa katikati. Ubavu mmoja kati ya hizo nne utakua mlango.
  • Ubavu huo uliotengeneza wa pande zote nne jaza vipande vya mkaa pamoja na chenga katikati ya waya meshi mbili mpaka juu, usitumie vumbi za mkaa kwani zitachafua mbomboga zako.
  • Unganisha vipande vyote vinne kutengeneza boksi ambalo utalisimamisha juu ya ardhi. Unaweza ukabuni muendelezo wa mbao kwa kila ubavu ili uchimbie chini.
  • Tengeneza droo mfumo wa shelvu kulingana na mahitaji yako, hii itakusaidia kuhifadhi mbogamboga zako kama ilivyo kwenye friji za kisasa.
  • Baada ya kukamilisha droo au shelvu, lisimike boksi lako vizuri juu ya ardhi sindilia vizuri na udongo na kuziba pande zote na matope ukitumia udongo wa mfinyanzi itakua vizuri sana.
  • Ezeka nyasi kavu juu ya hilo box lako ulilolisimika juu ya ardhi.
  • Sehemu ya sakafu ya ndani siliba na udongo usitumie simenti, pia usitumie waya au mkaa kuweka sehemu ya chini au kuezekea.
  • Usisahau kuweka mlango kwa ajili ya kuzuia wezi na wanyama waharibifu kama mbuzi, panya n.k. Mlango huo lazima uwe na vipande vya mkaa katikati pamoja na chenga kama ilivyo kwenye upande mwingine wa friji yako.
  • Baada ya kukamilisha friji yako ikiwa ina muonekano mzuri na imesimama barabara juu ya ardhi. Jambo linalofwata na la muhimu sana ni utaratibu wa kumwagia maji vipande vya mkaa vilivyopo kwenye waya meshi kwa siku mara tatu (yaani asubuhi, mchana na jioni), ili kudhibiti hali ya ubaridi isipotee. Kiwango cha kumwagia maji vipande hivyo vya mkaa itategemeana na hali ya hewa, kama kuna joto sana inabidi umwagie maji kila wakati na kila siku. Au unaweza ukaweka mfumo wa kumwagilia wa moja kwa moja kwa njia ya matone (Drip Irrigation), kama hutaweza kuweka mfumo huu basi tumia njia ya kawaida.
Friji hii ya asili itamsaidia mkulima wa mbogamboga kutoharibikiwa bidhaa yake, na kumfanya kuuza bidhaa hizo kwa faida kubwa. Friji hii haimfai mkulima peke yake bali hata mfanyabiashara wa mbogamboga anaenunua kwa wakulima anaweza kuhifadhi kwa muda mrefu hadi mwezi mmoja kwa kuuza kidogo kidogo kulingana na hali ya soko pasipo kupata hasara ya uharibifu. Pia kwa majumbani au wafanya biashara wa vinywaji waliopo kwenye maeneo yasiyokua na umeme au wakishindwa kupata friji za kisasa zinazotumia umeme, wanaweza wakatumia tekinolojia hii rahisi kuhifadhi vinywaji vyao na kuwa na ubaridi kama ilivyo kwenye friji za kisasa.

Muhimu*
Kama nilivyoelezea mwanzoni kabisa mwa makala hii kwamba upatikanaji wa mkaa lazima ufwate taratibu za serikali hususani kwa wale wanaochoma mkaa, lazima wapate vibali vya serikali ili kuchoma mkaa, kwani mchakato huu wa kupata mkaa unaleta uharibifu wa mazingira unaohusisha ukataji wa miti. Kwa hiyo utaratibu huu wa kupata vibali unasaidia kuepukana na ukataji horela wa miti na huhifadhi miti ambayo ni rasilimali muhimu sana kwa manufaa ya nchi yetu pendwa ya Tanzania.

Kama umevutiwa na makala hii na ungependa umshirikishe mwenzako kwenye mitandao ya kijamii, bofya batani za mitandao hiyo ya kijamii hapo chini kama Facebook, Twitter, Google+ n.k.

Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

Previous Post Next Post