Kilimo bora cha Karanga - Sehemu ya Kwanza (Growing Groundnuts - Part One)


SEHEMU YA KWANZA

Karanga (Groundnuts) ni zao linalolimwa maeneo mengi nchini Tanzania, Barani Afrika na Duniani kote. Karanga hutumiwa kwa matumizi mbalimbali kama chakula, kutengenezea mafuta, kutengenezea bidhaa mbalimbali za viungo, pia hutumika kama dawa za kutibu magonjwa mbalimbali (medicinal value) n.k. Karanga zina virutubisho mbalimbali na muhimu kwa afya ya binadamu kama Mafuta (38-50%), Protini (Protein), Kasiamu (Calcium), Potasiamu (Potassium), Fosforasi (Phosphorus), Magnesiamu (Magnesium) na Vitamini. Kwa upande wa kutibu magonjwa mbalimbali imeripotiwa kwamba Karanga hutibu magonjwa yafuatayo; Kutokwa na damu puani (Hemophilia), Vivimbe vya mdomoni (Stomatitis), Kuharisha (Diarrhoea) n.k.

Barani Afrika zao la Karanga limekua na kiwango kidogo sana cha mavuno, hii inatokana na mvua zisizokua na uhakika, pia wakulima wengi hawatumii tekinolojia ya kisasa kulima zao hili, Ongezeko la wadudu na magonjwa mbalimbali, Matumizi ya mbegu za kienyeji, na ongezeko la ufinyu wa maeneo ya kulima.

Picha: Mmea wa karanga       Photo Credit: www.greatlakesstapleseeds.com

MAZINGIRA
Zao la karanga hupendelea maeneo ya kitropiki yenye hali ya hewa yenye joto kiasi pia yaliyo kwenye mwinuko chini ya mita 1500 kutoka usawa wa bahari. Pia hustawi maeneo yenye hali ya hewa yenye baridi lakini pawe na kiangazi kirefu chenye joto (Long wam Summers). Joto mahsusi linalohitajika kwa zao hili ni nyuzijoto 30°C joto likipungua hadi kufikia nyuzijoto 15°C, mmea hudumaa. Hali ya baridi huchelewesha mmea kutoa maua.

Kiasi cha maji au mvua inayohitajika wakati wote wa ukuaji ni mm 500 hadi 600, Zao la karanga huvumilia sana hali ya ukame, lakini hali ya ukame ikizidi uzalishaji hupungua.

Udongo unaofaa kwa zao la karanga ni ule usiotwamisha maji na unaotunza virutubisho kama udongo wenye kichanga kiasi, tifutifu au wenye mfinyanzi kiasi. Pia kiasi cha tindikali ya udongo kinachofaa ni kuanzia pH 5.5 hadi 6.5, ingawaje aina ya karanga inayokua sana (Bush types) huvumilia udongo wenye tindikali nyingi (acidic conditions) na baadhi ya aina nyingine hustawi vema kwenye udongo usiokua na tindikali kabisa (Alkaline soils to pH 8.5)

AINA
Aina za karanga zimegawanyika katika makundi mawili; Zile zinazotambaa (Runner) na Zile ambazo hazitambai (Bunch). Kuna aina zaidi ya 11 za mbegu za kisasa za karanga zinazozalishwa na watafiti nchini Tanzania kupitia taasisi za utafiti za serikali 'ARI' (Agricultural Research Institute). Miongoni mwa mbegu hizo, mbegu ya kisasa aina ya PENDO ndio inayopendwa na wakulima wengi, na hupandwa sana mikoa ya Singida, Mwanza, Shinyanga, Tabora, Mtwara na Dodoma, nchini Tanzania. Majina ya aina nyingine za mbegu hizi za kisasa nitayaongeza ndani ya makala  hii hapo baadae.

Mbali na kuwepo kwa mbegu hizo za kisasa, bado wakulima wengi wamekua wakipanda mbegu za kienyeji, hali inayopelekea uzalishaji kuwa wa kiwango kidogo sana.

KUPANDA
Karanga hupandwa kwenye ardhi iliyo tambalale au kwenye matuta, matuta hupendekezwa kutumika endapo eneo hilo la shamba linatwamisha  maji (water logging). Pia  karanga zilizopandwa kwenye matuta huwa na mavuno mengi. Kwa upande wa kupanda kwenye ardhi iliyo tambalale hakikisha unalima kina cha kutosha ili kuipa nafasi mizizi ya karanga kutawanyika vizuri na pia kupata mavuno mengi.

Nafasi inayotumika kupanda kwenye ardhi tambalale ni sm 30 au 40 x sm 20 yaani sm 30 au 40 mstari hadi mstari na sm 20 shina hadi shina. Kupanda kwenye matuta; tengeneza matuta yenye kimo cha wastani na yaliyo tambalale kwa juu na yatakayowezesha kuwa na mistari miwili ya karanga yenye nafasi ya sm 30 × sm 20. Nafasi ya tuta hadi tuta ni sm 75 hadi 80.

Kama udongo  una tindikali nyingi tumia chokaa kupunguza hali hiyo, pia unaweza ukatumia mbolea za kupandia kabla ya kupanda kama TSP au DAP.

KUBADILISHA MAZAO
Kubadilisha mazao ni muhimu sana kwa ustawi wa zao lako la karanga, hii ina maana kwamba usipande karanga kwenye eneo moja la shamba kwa miaka kadhaa mfululizo, bali inatakiwa upande na mazao mengine kwa awamu. Zifuatazo ni sababu muhimu za kufanya hivyo;
  • Kupunguza kuzaliana kwa wadudu waharibifu na magonjwa kama Minyoo wa kwenye udongo (Nematodes), Magonjwa ya Ukungu (kama; White mould), Madoa ya kwenye majani (Leaf spots) n.k.
  • Kuboresha rutuba ya udongo kwani baadhi ya mimea hususani jamii ya mikunde huongeza virutubisho muhimu kwenye udongo.
  • Kuboresha muonekano na mshikamano wa udongo (Soil structure) na kupunguza upotevu wa rutuba. Zao la karanga hunyonya virutubisho kwenye udongo kwa kiasi kikubwa kwa hiyo ni vyema ukayarejesha kwenye udongo masalia yote baada ya kuvuna ili yakishaoza rutuba iongezeke kwenye udongo.
Wakati wa kuamua ni zao gani upande baada ya kupanda karanga, ni vyema kufahamu kwamba mimea yote iliyopo kwenye familia moja na karanga haitakiwi kupandwa kwani itaendelea kudumisha magonjwa na wadudu kama wale wa kwenye karanga. Kwa hiyo inatakiwa kupanda mazao yasio kwenye familia moja na karanga.

Mazao yanayofaa kubadirishana na karanga ni kama; Mahindi, Mtama, Uwele, Mihogo, Viazi vitamu na Alizeti. Mazao yasiyofaa kubadirishana na karanga ni kama; Mimea yote jamii ya mikunde kama Soya, maharage n.k., Tumbaku, Pamba na Nyanya.


Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

Previous Post Next Post