KANUNI ZA UKUZAJI WA MBOGAMBOGA
SEHEMU YA 3
KUBADILISHA MAZAO SHAMBANI
Kubadilisha mazao shambani ni utaratibu wa kuacha kupanda mfululizo aina ileile ya zao katika eneo hilo hilo. Iwapo eneo ni kubwa, bustani igawanywe katika sehemu tatu au nne ili kuepuka kupanda mfululizo aina ileile ya zao. Katika kila sehemu panda aina nyingine ya mazao na ya aina tofauti kila baada ya kuvuna.
Baada ya kuvuna, Mazao ya sehemu ya kwanza yapandwe katika sehemu ya pili, ya pili katika sehemu ya tatu na ya tatu yapandwe katika sehemu ya nne na yale ya nne yapandwe katika sehemu ya kwanza.
Kubadilisha mazao shambani huzuia ongezeko la wadudu na magonjwa yanayoshambulia jamii moja ya zao. Vilevile huhifadhi rutuba ya udongo na huzuia uotaji wa magugu. Utaratibu huu pia humwezesha mkulima kuweka kiasi cha mbolea kinachotakiwa shambani. Ufuatao ni mfano wa kubadilisha mazao ya mbogamboga;
>>> Bofya mchoro hapo juu kuuona vizuri
MATUMIZI YA MADAWA
Ni muhimu kutumia madawa ili kukinga mimea kutokana na athari za wadudu na magonjwa. Hata hivyo madawa yatumike pale inapobidi kwani ni ghali na yana madhara kwa mazingira na watu.
Mambo yafuatayo yanatakiwa kuzingatiwa wakati wa kutumia madawa. Hakikisha unatumia dawa inayoshauriwa na wataalamu.
1. Soma kwa uangalifu maelezo yanayoambatana na dawa toka kwa watengezaji, kabla ya kutumia na yasikiukwe. Hii itakusaidia kujua vifaa, kiasi na jinsi ya kutumia. Madawa ni hatari kwa binadamu na wanyama kama yatatumika isivyopasa.
2. Wakati wa kuchanganya na kunyunyiza dawa, vaa nguo na vifaa vya kinga Vifaa hivi ni kofia, glovus, viatu (gumboots), kitambaa cha kufunika mdomi na pua, miwani na ovaroli.
3. Tumia maji safi kuchanganya dawa.
4. Epuka kuvuta hewa yenye dawa. Wakati wa kunyunyiza dawa usiekekee upepo unakotoka baki elekea upepo unakoenda.
5. Usile wala kuvuta wakati wa kuchanganya au kunyunyiza dawa.
6. Baada ya kunyunyiza dawa osha mwili kwa sabuni na maji mengi na safi.
7. Maji yanayotumika kusafishia bomba/Pampu yasimwagwe katika maji yanyotuama au yanayotembea kwani yanaweza kuleta madhara sehemu nyingine. Maji yamwagwe kwenye shimo na kufukiwa.
8. Nguo zilizotumika zifuliwe mara moja kwa sabuni na maji safi pia vifaa vingine vilivyotumika vioshwe kwa maji safi na sabuni.
9. Osha vizuri mikono kwa sabuni kabla ya kula, kunywa chochote au kuvuta sigara.
10. Makopo au chupa zilizokuwa na dawa zisitumike bali ziharibiwe kwa kuchomwa moto (Kama ni za plastiki) kwenye eneo lililo mbali na makazi kwani moshi wake ni sumu. Kama ni chupa za grasi basi zifukiwe kwenye shimo lililo mbali kidogo na eneo ambalo watoto hawawezi kufikia au kufukua.
11. Hifadhi madawa mahali salama na pasipofikiwa na watoto kwa urahisi. Dawa ziachwe kwenye makasha, chupa au makopo yake zilimokuwemo. Hata siku moja madawa ya mimea yasitumike kuribu bibadamu.
12. Endapo kutakuwepo na matatizo yeyote katika matumizi muone Mtaalamu/Afisa kilimo kwa ushauri.
13. Iwapo sehemu ya kutolea dawa itaziba, tumia nyazi au kijiti kuzibua. Kamwe usizibue kwa mdomo.
Makala hii Imehaririwa mara ya mwisho Tarehe: 01/09/2016
Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo
Post a Comment