KANUNI ZA UKUZAJI WA MBOGAMBOGA
SEHEMU YA 2
KUITAYARISHA MICHE KABLA YA KUPANDIKIZA
Wiki mbili kabla ya kuihamisha miche toka kitaluni, unashauriwa kupunguza kumwagilia ili kuizoesha iweze kustahimili hali ya sehemu inapohamishiwa.
Mwagilia kitalu siku moja kabla ya kung'oa miche ili kurahisisha ung'oaji na kuepuka kuikata mizizi. Pia shamba kwa ajili ya kuhamisha miche limwagiliwe siku moja kabla ya kupandikiza ili kuloanisha udongo.
MATUMIZI YA MBOLEA
1. Mboji, Samadi na Mbolea Vunde
Mboga hustawi vizuri sana katika udongo wenye mbolea hizo. Hivyo ni vema mbolea hizo ziwekwe shambani kabla ya kupanda au kupandikiza. Kiasi kinachotakiwa ni ndoo moja kubwa ya Lita 20 kwa tuta lenye upana na urefu wa mita moja.
2. Mbolea za Viwandani
Mbolea za viwandani zimegawanyika katika makundi makuu makuu matatu, nayo ni mbolea za Chumvichumvi, Chokaa na Kijivu.
(a) Mbolea za Chumvichumvi
Mbolea hizi hujulikana kama Mbolea za kukuzia na huwekwa shambani baada ya mimea kuota. Zina virutubisho vingi vya Nitrojeni ambavyo huifanya mimea kukua haraka. Pia zinahusika na utengenezaji wa kijani kibichi kwenye mmea.
Nchini Tanzania mbolea za chumvichumvi zinazotumika zaidi ni;
-Sulphate of Ammonia (S/A) 21%N
-Calcium Ammonium Nitrate (CAN) 26%N au 27%N
-Urea 46%N
-Mbolea ya mchanganyiko N.P.K 25:5:5 na 20:10:10
(b) Mbolea za Chokaa
Hizi ni mbolea zinazotumika kupandia mbegu au miche. Husaidia uotaji mzuri wa mimea, huimarisha mizizi na hutumika katika utengenezaji wa chakula na mbegu kwenye tunda. Vilevile huhusika na usafirishaji wa nguvu kwenye mmea na hufanya mazao kukomaa haraka. Mbolea hizi huwekwa shambani wakati wa kupanda.
Aina ya mbolea za chokaa zinazotumika hapa nchini Tanzania ni;
-Diamonium Phosphate (DAP) 18 - 21%N na 46 - 53%P2O5
-Triple Super Phosphate (TSP) 46% P2O5
-Vilevile unaweza kutumia N.P.K. 6:20:18 au 10:30:10, kwa sababu mbolea hii ina mchanganyiko wa virutubisho vitatu yani Nitrojeni (N), Phosphate (P) na Potassium (K) pia ukiangalia kwenye Uwiano huu (6:20:18) au 10:30:10 kirutubisho cha Phosphorus/Phosphate (P) kina asilimia 20%P2O5 kuzidi vrutubisho vingine kama 6%N na 18%K2O. Hivyo basi uwiano huu N.P.K 6:20:18 inafaa kupandia.
(c) Mbolea za Kijivu (Potashi)
Potashi (Potassium) ni kirutubisho kinachosaidia mimea katika utengenezaji wa protini na wanga. Kadhalika huhusika na utumiaji wa madini muhimu kwa maisha ya mimea. Mbolea hii pia huwezesha matunda kukomaa, kuiva haraka, na kutengeneza mbegu bora. Vilevile husaidia ongezeko la maji kwenye mmea na kuufanya ustahimili magonjwa, ukame, baridi na hali ya udongo wenye alkali nyingi.
Mbolea za Potashi zinazotumika ni;
-Murate of Potash 48 - 60% K2O
-Sulfate of Potash 48 - 50% K2O
MUHIMU
Inapendekezwa kwamba unaweza kutumia makundi haya mbolea yote mawili kwa pamoja ili kuongeza ufanisi wa udongo kwa sababu zifuatazo;
>Afya ya udongo inalindwa na maozea ya samadi, mboji ama masalia/majani yaliyooza kwenye udongo.
>Hii ina maana kwamba Udongo wenye kiasi kidogo sana cha maozea, una uwezo mdogo sana wa kuupa mmea virutubisho. Hata kama utaweka mbolea za viwandani. Hii ni kwa sababu zifuatazo;
1. Uwezo wa Udongo kuupa mmea virutubisho ama kwa kimombo "Cation exchange capacity" (CEC) unatengenezwa na uhusiano wa hali ya HASI (-ve) na CHANYA (+ve) kwenye udongo.
2. Virutubisho vya mmea vina Chaji ya CHANYA (+ve) kama N+, P205+, K20+ na vingine kama Mg2+, Ca2+, Zn2+, Mo+ na vingine. Kama unavyofahamu kwamba CHANYA na HASI huwa zina vutana au kushikana na CHANYA na CHANYA au HASI na HASI hukwepana, Hivyo basi ili kurahisisha udongo kuwa na uwezo wa kukamata au kuvuta hivyo virutubisho ambavyo vina Chaji ya CHANYA kama nilivyoeleza hapo juu, lazima Udongo uwe na Chaji ya HASI (-ve). Udongo wenye hali ya HASI nyingi ndio wenye uwezo wa kuzalisha sana kwani unakua na uwezo wa kuvuta virutubisho vingi ambavyo ni vya CHANYA (+ve) na kuupa mmea kwa haraka na kwa ufanisi zaidi.
3. HASI (-ve) nyingi kwenye udongo hujengwa na maozea shambani kwa kuweka mbolea za asili kama Samadi, Mboji, au masalia ya mimea isiyokua na magonjwa au majani. Udongo wenye maozea mengi au Samadi au mboji nyingi unauwezo wa kuzalisha sana kwani unakua na uwezo wa kukamata au kunasa virutubisho na kuupa mmea virutubisho hivyo ambavyo vina hali ya CHANYA (+ve) kwa haraka na ufanisi zaidi.
Kwa mazao ya mbogamboga weka samadi ndoo moja kubwa ya Lita 20 kwenye tuta lenye upana wa mita 1 au eneo la mita 1 (1m2). Kama tuta lako lina urefu wa mita 5 ina maana utamwaga samadi ndoo kubwa 5, kwani eneo la tuta ni mita 5 kwa mita 1. Japokua hapa tunaeleza mazao ya mbogamboga hebu kidogo nigusie uwekaji wa samadi kwenye mazao mengine kama magindi, maharge na mengine.
Uwekaji wa mbolea ya samadi kwenye mazao mengine unaweka Kiganja kimoja au viwili vya samadi kwenye shimo kabla ya kuweka mbegu pia kama una mbolea za kupandia za viwandani kama DAP, TSP au NPK unatupia kifuniko cha soda kimoja (hii ni kama utapanda mbegu moja kila shina, kama utapanda mbegu 2 utaweka visoda viwili) baada ya kuweka Samadi kisha unafukia kidogo afu unaweka mbegu. Tunatenganisha mbolea(Samadi + DAP) na mbegu au mche kwa udongo kiasi kwa sababu mbolea ikigusana moja kwa moja na mbegu, Mbegu inaungua.
Hivyo basi Kadri maozea yanavyozidi kuongezeka kwenye udongo ndivyo jinsi uwezo wa udogo kuupa mmea virutubisho unavyoongezeka. Pia ukiweka mbolea za viwandani kwenye udongo huo utapata matokeo mazuri sana, kwani itatumika haraka na kwa ufanisi.
Udongo usiokua na maozea kabisa au kidogo unakua na uwezo mdogo sana wa kuzalisha hata kama utaweka mbolea za viwandani lakini hutaona matokeo kwenye mmea, kwa nini? Hii ni kwa sababu Udongo usiokua na maozea yaani Samadi au mboji unakua na hali ya CHANYA (+ve) nyingi kiasi kwamba kunakua na kukwepana na virutubisho vya mbolea ya viwandani uliyoweka ambavyo navyo ni CHANYA (+ve), kwani CHANYA na CHANYA kamwe hazikamatani zinakwepana. Kwa mchanganuo huu unajikuta unaweka mbolea za viwandani lakini mimea haishtuki.
Kwa hiyo kutumia mbolea za asili ni muhimu kuongeza uzalishaji wa shamba au bustani yako pia kulifanya shamba lako lisichoke. Kwa hiyo kama utatumia mbolea za viwandani anza au pandia mbolea za asili kwanza ndipo uweke mbolea za viwandani. [<<Bofya hapo chini kusoma sehemu ya kwanza na sehemu ya tatu ya Makala hii>>]
Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo
Post a Comment