Kanuni za Ukuzaji wa Mbogamboga - Sehemu ya Kwanza (Principles for Growing Vegetables - Part one)


KANUNI ZA UKUZAJI WA MBOGAMBOGA 
SEHEMU YA 1


KUCHAGUA ENEO:
Katika uchaguzi wa eneo kwa ajili ya bustani zingatia yafuatayo;

1. Mwinuko
Eneo lisiwe kwenye mwinuko mkali kwa sababu sehemu kama hizo zinaweza kusababisha mmomonyoko wa udongo. Endapo sehemu itakuwa ya mwinuko tengeneza matungazi (terrace) ili kuzuia mmomonyoko.


2. Udongo
Udongo unaofaa ni wenye rutuba, mboji nyingi na unaopitisha maji kwa kirahisi. Vilevile usiwe na historia ya magonjwa na wadudu waharibifu.

3. Chanzo cha Maji
Eneo la bustani liwe karibu na maji ya kudumu. Maji yasiwe na chumvi nyingi kwani huathiri ukuaji wa mimea.

4. Kitalu
Kitalu kisiwekwe mahali palipo na kivuli kingi kwa kuwa husababisha mimea kuwa dhaifu.


5. Kuzuia Upepo Mkali
Eneo la bustani lipandwe miti mipakani ili kuzuia upepo mkali. Upepo mkali huharibu mimea kwa kuvunja vunja majani na matawi na husafirisha vimelea vya magonjwa na wadudu. Pia hufanya udongo wa juu kukauka haraka na kuleta mmomonyoko.

KUTAYARISHA MATUTA
Ni muhimu udongo utifuliwe vizuri. Mabonge makubwa yavunjwe vunjwe ili kurahisisha upitaji wa maji na hewa katika udongo. Matuta huinuliwa kidogo toka usawa wa ardhi ili kuzuia maji yasituame, Matuta haya yasitumike wa kiangazi. Wakati wa kiangaz tengeneza matuta yaliyodidimia kidogo.

KUMWAGILIA MAJI
Hakikisha udongo una unyevu wa kutosha kwa kumwagilia siku moja kabla ya kuotesha mbegu. Pia baada ya kupanda mwagilia kitalu au shamba maji ya kutosha. Maji mengi husababisha mbegu au miche kuoza.



KUPANDA
Kina cha kupanda kinategemea ukubwa wa mbegu. Mbegu ndogo hupandwa kina kifupi zaidi kuliko mbegu kubwa. Upandaji wa baadhi ya mbegu unaweza kufanyika kila wiki ili kuweza kupata mboga mfululizo.

KUOTESHA MBEGU KWENYE KITALU
Baadhi ya mbegu za mboga huoteshwa kwenye kitalu na baadaye miche huhamishiwa shambani. Mbegu hizi ni kama vile Bilinganya, kabichi, nyanya, pilipili hoho na vitunguu. Kitalu kwa ajili ya kuotesha mbegu hakina budi kitayarishiwe wiki moja kabla ya kusia mbegu. Wakati wa kutayarisha kitalu, ardhi ikatuliwe katika kina cha kutosha sentimita 30 kwenda chini. Ili kuongeza rutuba ya udongo mbolea za asili kama vile Samadi, takataka za mbolea vunde zilizooza vizuri ziwekwe kabla ya kusia mbegu.



KUTUMIA MBEGU BORA
Tumia mbegu bora zilizohifadhiwa kwenye dawa. Mbegu bora ni zile ambazo zimekomaa na kukauka vizuri, hazikushambuliwa na wadudu wala magonjwa na ambazo zina uwezo wa kuota vizuri. Inashauriwa kutumia mbegu zilizothibitishwa kitaalamu.

KUWEKA KIVULI CHA MATANDAZO
Utandazaji wa majani makavu na uwekaji wa kivuli ni muhimu ili kuzuia jua linaloweza kunyausha miche. Matandazo pia husaidia kuhifadhi unyevu, joto la udongo na hupunguza palizi ya mara kwa mara. Kivuli kiruhusu mwanga wa kutosha na kiondolewe kidogo kidogo kadiri mimea inavyokua.


>>> Bofya mchoro hapo juu kuuona vizuri

[>>Bofya hapo chini kusoma sehemu ya pili ya Makala hii>>]







Makala hii Imehaririwa mara ya mwisho Tarehe: 31/08/2016

Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

Previous Post Next Post