Kilimo cha Bilinganya - Sehemu ya tatu (Growing Eggplant - Part three)


KILIMO CHA BILINGANYA 
SEHEMU YA 3

WADUDU WAHARIBIFU NA MAGONJWA.
Wadudu Waharibifu
1. Vinyatomvu wa Bilinganya (Eggplant Lacebugs)
Wadudu hawa hushambulia zaidi sehemu ya chini ya jani. Hufyonza utomvu wa majani na kusababisha majani kuwa na mabaka meupe au njano. Mashambulizi yakizidi majani huanguka chini. Vinyatomvu wanaweza kuzuiwa kwa kunyunyiza dawa za wadudu zenye viua sumu vifuatavyo;

Deltamethrin, Dimethoate, Fenvalerate na Lambda - Cyhalothrin.


Viua sumu hapo juu unaweza ukavipata kwenye dawa za kuua wadudu, huwa vinaandikwa kwenye kava la chupa ya dawa. Majina kama Karate, Actellic, Selecron ni majina ya kibiashara lakini yanakua na viua sumu mojawapo kati ya nilivyovitaja hapo juu.

Kwa hiyo ukienda kuulizia dawa ya kuua wadudu ni muhimu kuchunguza viua sumu vilivyopo ndani ya dawa kwa sababu majina ya biashara kama Actellic au karate yanabadilika kila kukicha lakini viua sumu ni vilevile havibadiliki

 
Picha zifuatazo zinamuonyesha mdudu huyu muharibifu alivyo;



 

2. Vidukari au Wadudu mafuta (Cotton Aphids)
Hawa ni wadudu wadogo wenye rangi nyeusi. Hushambulia majani machanga na kuyasababisha kudumaa na kukunjamana. Zuia wadudu hawa kwa kutumia dawa zenye viua sumu vifuatavyo;

Lambda - Cyhalothrin, Dichlorvos, profenofos


Picha zifuatazo zinaonyesha wadudu hawa (Vidukari)




3. Utitiri wa Mimea (Red Spider mites)
Ni vidudu vidogo venye rangi nyekundu iliyoiva. Hushambulia majani kwa kufyonza utomvu. Majani yaliyoshambuliwa huonyesha utando kama wa buibui. Mashambulizi yakizidi mmea hudumaa, majani hukauka na hatimae hufa. Utitili unazuiwa kwa kutumia dawa zenye viua sumu vifuatavyo;

Lambda - Cyhalothrin, Dimethoate, Quinofos na Profenofos

Picha zifuatazo zinaonyesha wadudu hawa (Utitiri wa mmea)




4. Minyoo Fundo (Root Knot nemtodes)
Wadudu hawa hushambulia mizizi. Hutoa kinyesi ambacho ni sumu kwa mmea. Sumu hii husababisha mizizi kuwa na nundu kama ya mizizi ya maharagwe. Mashabulizi yakizidi mmea hudumaa, hunyauka na hatimaye hufa.

 
Picha zifuatazo zinamuonyesha huyo mnyoo (anavyoonekana kwa njia ya hadubini/Microscope)

 Picha ya juu: Mnyoo Fundo unavyoonekana kwa kutumia Hadubini/Microscope


Picha ya juu: Mnyoo Fundo unavyoingia kwenye mzizi wa mmea


Picha ya juu: Mzizi wa mmea ulivyoathiriwa na Mnyoo fundo

Njia ya kuzuia wadudu hawa ni kubadilisha mazao. Kwa mfano; baada ya kuvuna zao hili, zao linalofuata lisiwe la jamii moja na bilinganya, kama vile nyanya, pilipili na viazi mviringo. (Rejea kanuni za Ukuzaji wa mbogamboga nilizochapisha kwenye Blogi hii)

Pia unaweza ukatumia dawa yoyote yenye kiua sumu cha Carbofuran. [<<Bofya hapo chini kusoma sehemu ya pili na sehemu ya nne ya makala hii>>]


Makala hii Imehaririwa mara ya mwisho Tarehe: 04/09/2016

Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

Previous Post Next Post