Kilimo cha Nyanya - sehemu ya tano (Growing Tomatoes - Part five)


KILIMO CHA NYANYA SEHEMU YA 5

HITILAFU ZA MATUNDA

a. Kupasuka Matunda
Kuna aina mbili za mipasuko; Mpasuko wa mviringo na mpasuko wa nyota
(i) Mpasuko wa Mviringo
Hali hii hutokea wakati mmea haukupata maji ya kutosha hasa wakati wa jua kali. Wakati huu maji yaliyoko kwenye tunda hayawezi kulingana na maji yanayopotea angani kama mvuke.

(ii) Mpasuko wa Umbo la Nyota
Hutokea hasa tunda linapokuwa na maji mengi na wakati huo unyevu angani ni mwingi sana. Hivyo tunda hushindwa kupoteza maji kwa njia ya mvuke na hupasuka kabla ya kukomaa. Hutokea zaidi kwenye nyanya aina ya "Marglobe". Mpasuko wa mviringo na umbo la nyota huzuiwa kwa kumwagilia maji inavyotakiwa

b. Kuoza Kitako
Vidonda vyeusi vilivyodidimia huonekana kwenye kitako cha tunda. Sehemu hii baadae hunyauka na ngozi huwa nyeusi. Hali hii hutokea zaidi wakati wa jua kali na katika sehemu zenye udongo wenye chumvi na tindikali nyingi.

Zuia hali hii kwa kuhakikisha udongo unaunyevu wa kutosha wakati wote. Pia epuka kuweka mbolea nyingi za chumvi chumvi.

c. Mabaka ya Matunda
Matunda yaliyopigwa na jua kali huwa na mabaka hasa sehemu za ubavuni. Hali hii inaweza kuzuiwa kwa kuepuka kupunguza matawi mengi kwa wakati mmoja.

d. Matunda ya kijani kibichi
Mabega ya tunda huwa na rangi ya kijani kibichi. Hitilafu hii hutokana na chanikiwiti (chlorophyll) kuwa nyingi na kutokea hasa wakati wa jua kali. Ili kuepuka hali hii unashauriwa kutokuweka mbolea nyingi ya chumvi chumvi na punguza mwanga wa jua kwa kufunika matunda na majani makavu.

KUVUNA
Zao la nyanya huwa tayari kwa kuvunwa baada ya wiki 14 hadi 16 (miezi 3 hadi 4) tangu kuotesha mbegu. Kwa kawaida aina fupi huchukua muda mfupi kukomaa kuliko aina ndefu. Uvunaji huchukua muda wa wiki sita hadi nane. Aina ndefu huchukua muda mrefu kuvuna kuliko aina fupi. Uchumaji hufanyika mara mbili au mara tatu kwa wiki kutegemea aina, usafiri, mahali pa kuhifadhi na mahitaji ya soko.

Nyanya kwa ajili ya matumizi ya nyumbani huvunwa wakati zimeiva kabisa. Nyanya kwa ajili ya kusafirisha au kuhifadhiwa kabla ya matumizi huchumwa kabla ya kuiva sana. Wakati huo huwa bado na rangi kati ya kijani na njano. Chuma nyanya kwa uangalifu sana. Nyanya zivunwe na vikonyo vyake kwani huwezesha tunda kuendelea kuiva vizuri na kusaidia nyanya zisioze haraka.

Chombo cha kuvunia kiwe imara na kiwe na uwezo wa kuingiza hewa ya kutosha. Iwapo mimea ya nyanya itatunzwa vizuri, inaweza kutoa mavuno kiasi cha tani 25 hadi 60 kwa hekta.



Makala hii Imehaririwa mara ya mwisho Tarehe: 18/11/2016

Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

Previous Post Next Post