Kilimo cha Nyanya - sehemu ya sita (Growing Tomatoes - Part six)


KILIMO CHA NYANYA SEHEMU YA 6

KUPANGA NYANYA KATIKA DARAJA
Nyanya zikushavunwa hupangwa katika daraja kufuata ubora wa tunda, ukubwa na rangi yake.

a. Kupanga kufuata Ubora wa Tunda
Ondoa nyanya zote zilizo mbovu, zenye kushambuliwa na wadudu au magonjwa kabla ya kuamua kuchagua zitakazosafirishwa au kuhifadhiwa. Nyanya zilizofanyiwa uchaguzi mzuri hupata bei nzuri zikiuzwa katika masoko makubwa.

b. Kupanga kufuata Rangi ya Tunda
Ni muhimu kupanga nyanya kufuata rangi. Kupanga nyanya kufuata rangi husaidia kupata nyanya zenye usawa wa kukomaa. katika kupanga kufuata rangi, panga ifuatavyo:-
- Nyanya zilizokomaa zenye rangi ya kijani kibichi.
- Nyanya zilizoiva zenye rangi ya pinki
- Nyanya zilizoiva zenye rangi nyekundu.

KUFUNGASHA
Nyanya kwa ajili ya kusafirisha zinatakiwa ziwekwe kwenye visanduku vya mbao vidogodogo visivyozidi ujazo wa ndoo mbili.

KUUZA NA KUHIFADHI
Nyanya ni bidhaa zinazoharibika haraka, hivyo ni muhimu zifikishwe kwa mlaji mapema baada ya kuchumwa. Kama inawezekana kupata vyombo vya kuleta hali ya ubaridi inafaa kuhifadhi na kusafirisha katika hali ta ubaridi ipatayo nyuzi joto 12 za Sentigredi ( 12 °C). Katika hali hii nyanya zinaweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu.

KUBADILISHA MAZAO
Zao la nyanya hutumia chakula kingi ardhini. Hivyo baada ya kuvuna zao hili lisifuatwe na mazao jamii ya nyanya kama vile bilinganya, ngogwe, pilipili na viazi mviringo. Hali kadhalika zao hili lisifuatiwe na zao lingine lolote linalotumia chakula kingi mpaka kumewekwa mbolea ya kutosha. Kubadilisha mazao hupunguza kuenea kwa wadudu na magonjwa yanayoshambulia jamii hii ya mazao. Vilevile huhifadhi rutuba ya udongo. Mfano unaofaa wa kubadilisha mazao ni huu ufuatao:-
1. Nyanya 2. Kabichi/Mchicha
3. Vitunguu/Karoti 4. Jamii ya kunde


*** MWISHO WA MAKALA HII ***

***ENDELEA KUFWATILIA MAKALA ZINGINE***

Makala hii Imehaririwa mara ya mwisho Tarehe: 18/11/2016

Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

Previous Post Next Post