Kilimo cha Vitunguu - sehemu ya pili (Growing Onions - Part two)



KILIMO CHA VITUNGUU SEHEMU YA 2

KUTUNZA SHAMBA

(i) Kuweka Mbolea
Mbolea ya kukuzia kama vile CAN au S/A huwekwa shambani katika wiki ya tatu na ya sita baada ya kupandikiza. Weka kiasi cha mifuko mitatu kwa hekta katika wiki ya tatu na mifuko minne katika wiki ya sita. Mbolea iwekwe kwenye mstari na isiguse mimea yani weka mbolea sentimita 5 kutoka mstari wa vitunguu. Mche mmoja huhitaji kiasi cha kijiko kimoja cha chai au kifuniko cha soda kilichojaa na hakikisha udongo una unyevu wa kutosha wakati wa kuweka mbolea.

(ii) Kumwagilia
Kila wakati hakikisha shamba lina maji ya kutosha. Punguza kumwagilia wakati vitunguu vinakomaa. Vitunguu vinavyokomaa majani hubadilika rangi kuwa njano. Maji mengi husababisha vitunguu kuoza baada ya kukomaa.

(iii) Palizi
Palilia na tifulia mara kwa mara uonapo magugu yanaota, na hasa miche inapokuwa bado michanga. Palizi ifanyike kwa uangalifu bila kuikata mizizi. Wakati unapopalilia katikati ya matari ni vema kung'oa magugu kwa mikono na kufunika shina kwa kupandisha udongo kuzuia mizizi isipigwe na jua.

(iv) Magonjwa na wadudu waharibifu

A. Magonjwa
a. Ubwiri Vinyonya (Downy Mildew)
Ugonjwa huu husababishwa na ukungu na hupendelea hali ya unyevu unyevu. Dalili zake ni majani kuwa na ukungu au uyoga wa rangi ya njano iliyochanganyika na nyeupe. Kwa kawaida majani yaliyoshambuliwa hukauka kabla ya vitunguu kukomaa. 



Ubwiri vinyoya huzuiwa kwa kuzingatia yafutayo;
  • Kubadilisha mazao. Baada ya kuvuna vitunguu, zao linalofuata lisiwe la jamii moja kama vile vitunguu saumu na Liki.
  • Nyunyuzia mojawapo ya dawa za kuzuia ukungu kama vile Dithane - M 45, Ridomil, Topsin M 70 na dawa zingine zenye viua sumu vifuatavyo; 1. (Mancozeb na Metalaxyl) kama Ivory M 72, Linkmil M 72 n.k,  2. "Copper" kama Blue copper, Cupric Hydroxide (Champion) n.k
b. Purple Blotch
Huu pia ni ugonjwa uletwao na ukungu na hushambulia majani, shingo na vitunguu vilivyokomaa. Dalili zake ni, majani huonyesha vidonda vyenye na vilivyodidimia. Baadaye baka la zambarau huonekana katikati ya jani. Baka hili baadaye huwa jeusi na hufunikwa na uyoga au ukungu. Shina lililoshambuliwa hulegea na huanguka katika wiki ya tatu au ya nne baada ya dalili za ugonjwa huu kuonekana.


Vitunguu vilivyokomaa huoza kuanzia shingoni, hugeuka rangi na kuwa njano iliyochanganyika na nyekundu. 


Zuia ugonjwa huu kwa kuzingatia yafuatayo;
  • Panda vitunguu vilivyothibishwa na wataalamu
  • Badilisha mazao
  • Vuna vitunguu kwa wakati unaotakiwa
  • Epuka kukwaruza au kuchubua vitunguu wakati wa kuvuna.
  • Ondoa masalia ya mazao shambani baada ya kuvuna na kuyachoma.
  • Panda vitunguu vinavyovumilia mashambulizi ya ugonjwa huu kama vile vitunguu vyekundu.
c. Kuoza Shingo (Neckrot)
Ugonjwa huu husababishwa na ukungu na hupendelea sana hali ya unyevu. Hushambulia vitunguu vilivyokwisha vunwa na kuhifadhiwa.
Vitunguu vilivyoshambuliwa na ugonjwa huu huwa laini, kubonyea na huonekana kama vilivyopikwa. Ugonjwa huanzia kwenye shingo na baadae huenea kwenye kitunguu chote na kufunikwa na ukungu wa kijivu. Mwisho machipukizi madogo hujitokeza. 



Ugonjwa huu unazuiwa kwa kuzingatia yafuatayo;
  • Vuna vitunguu vilivyokomaa kwa wakati unaotakiwa.
  • Badilisha mazao
  • Panda vitunguu vilivyothibitishwa na wataalamu.
  • Ondoa na yachome moto masalia ya mazao baada ya kuvuna.
  • Epuka kuchubua au kukwaruza vitunguu wakati wa kuvuna.
  • Kausha vitunguu vizuri baada ya kuvuna.
  • Hifadhi vitunguu kwenye sehemu zisizo na unyevu mwingi.


Makala hii Imehaririwa mara ya mwisho Tarehe: 27/11/2016

Makala na:
Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

Previous Post Next Post