Kilimo cha Vitunguu - sehemu ya kwanza (Growing Onions - Part one)


KILIMO CHA VITUNGUU SEHEMU YA KWANZA

Zao la vitunguu hulimwa karibu kila mahali hapa nchini Tanzania. Vitunguu na majani yake ni viungo maarufu kwa kuongeza harufu nzuri na ladha katika vyakula. Vile vile hutumika katika kutengeneza supu, siki na kachumbari. Kiafya vitunguu ni muhimu kwani hutupatia madini na vitamini.

MAZINGIRA
Vitunguu huhitaji udongo tifutifu wenye rutuba nyingi na usiotuamisha maji. Hustawi vizuri zaidi kwenye sehemu zenye mwinuko wa kuanzia mita 800 hadi 1500 kutoka usawa wa bahari. Hupendelea hali, ya ubaridi kiasi wakati wa kuotesha mbegu mpaka vinapoanza kuweka tunguu na joto la wastani (nyuzi joto 20 hadi 27 za Sentigredi "20 - 27 °C") hadi kuvuna. Hivyo ni vizuri vioteshwe wakati wa baridi ili viweze kuvunwa kipindi cha jua.

AINA
Aina za vitunguu zinazoshauriwa kustawishwa katika ukanda wa joto ni:-

Singida Local, Red Creole, Texas Grano, Tropical Red F1 Hybrid, Red Bombay na Pretoria Grano.

KUOTESHA MBEGU KATIKA KITALU
Mbegu za vitunguu huoteshwa kwanza kwenye kitalu na baadaye huhamishiwa shambani. Matayarisho ya kitalu hufanyika wiki moja au mbili kabla ya kupanda mbegu. Tengeneza tuta lenye upana wa mita moja na urefu wowote kutegemea mahitaji yako. Weka mbolea ya asili kiasi cha ndoo moja hadi mbili katika kila mita mraba mmoja. Changanya mbolea hii na udongo vizuri. Sawazisha kwa kutumia reki au kifaa chochote.

Mwagilia kitalu siku moja kabla ya kupanda. Sia mbegu katika mistari yenye nafasi ya sentimita 10 hadi 15 kutoka mstari hadi mstari. Kiasi cha mbegu konachotakiwa kuotesha katika eneo la mita mraba moja ni gramu tano ambacho ni sawa na kijiko kidogo cha chai. Kiasi hiki pia hutoa miche inayotosha kupandikiza eneo la mita mraba 100. Kilo mbili hadi 2.5 za mbegu hutoa miche ambayo inatosha kupandikiza katika eneo la hekta moja.

Baada ya hapo weka matandazo kama vile nyasi, kisha mwagilia mara mbili kila siku (asubuhi na jioni) hadi mbegu zitakapoota. Mbegu bora huota baada ya siku 10 mpaka 12.

KUTAYARISHA SHAMBA
Tayarisha shamba vizuri mwezi mmoja kabla ya kupandikiza. Kisha lainisha udongo katika kina cha kutosha (sentimita 30). Kisha lainisha udongo wiki mbili kabla ya kupandikiza. Weka mbolea za asili zilizooza vizuri ili kuufanya udongo ushikamane vizuri na uweze kuhifadhi unyevu kwa muda mrefu. Kiasi kinachotosha hekta moja ni tani 20 au zaidi. Kwa hali halisi kupata kiasi kikubwa cha mbolea hizi ni nadra sana. Kwa hiyo njia rahisi ya kubana matumizi ya mbolea hizi pindi utakapopata kiasi kisichoweza kutosha shamba lako ni kuweka kiasi kidogo kwenye kila shimo. Kiasi cha kiganja kimoja au viwili kwa kila shimo hutosha kwa kila mche.

Kutokana na kwamba nafasi utakayopandikiza itakuwa ya kubanana kiasi (sentimita 8 hadi 12) na kuweka kiganya cha mbolea za asili kwa kila shimo itakua changamoto yani utaweka mashimo mengi sana kwa semu ndogo na itakupa kazi sana, basi unaweza kumwaga mbolea hizo kidogo kidogo kwa upana wa kiasi cha kiganja kimoja au viwili kwa kufwata mstari kisha changanya mbolea hii kwa kutumia ncha ya leki au jembe dogo. 

Lakini unavyomwaga mbolea hii kwa kufwata mstari hakikisha unapandikiza wakati huo huo ili kuhakikisha unapanda sehemu husika yenye mbolea hiyo. Ukishachanganya mbolea hiyo vizuri na udongo unaweza kupandikiza. Kama una eneo dogo la kupandikiza unaweza kumwaga mbolea hizo za asili kwenye shamba hilo alafu changanya vizuri ndipo upandikize.

Matuta yanafaa pia kwenye kilimo cha vitunguu kwa kutumia nafasi nitakazo kupa kwenye maelezo yanayofuata kwenye makala hii. Kama hutotumia matuta hakikisha kina cha udongo ni kikubwa sana (sentimita 30 kwenda chini) ili upate vitunguu vikubwa na vyenye afya.

KUPANDIKIZA
Miche inakuwa tayari kwa kupandikizwa shambani baada ya wiki sita tangu kusia mbegu. Wakati huo miche inakuwa na urefu wa sentimita 12 hadi 15 na unene uliosawa na kalamu ya risasi.
Loanisha kitalu siku moja kabla ya kung'oa miche ili kuepuka kukata mizizi. Tumia kijiti au chombo chochote kinachofaa kwa kung'oa. Baada ya kung'oa punguza majani na mizizi ili kuzuia upotevu wa maji.

Pandikiza miche katika nafasi ya sentimita 30 kutoka mstari hadi mstari na sentimita 8 hadi 12 mche hadi mche. Vitunguu vilivyopandwa kwa nafasi hii hukomaa mapema na idadi ya mimea kwa eneo ni kubwa.


Chagua miche yenye afya na ambayo haikushambuliwa na wadudu wala magonjwa. Miche michanga sana au iliyokomaa sana haifai kwa kupandikiza. Miche ipandikizwe katika kina kama vile ilivyokuwa kwenye kitalu. Pandikiza wakati wa asubuhi au jioni ili kuepuka jua kali na joto linaloweza linaloweza kuunguza miche. Mara baada ya kupandikiza mwagilia maji. Endelea kumwagilia asubuhi na jioni mpaka miche itakaposhika vizuri.


Makala hii Imehaririwa mara ya mwisho Tarehe: 27/11/2016

Makala na:
Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

Previous Post Next Post