Kilimo cha Matikiti - Sehemu ya tatu (Growing Watermelons - Part three)


UTUNZAJI SHAMBANI
Kutandaza makaratasi meusi ya plastiki juu ya udongo huweza kusaidia yafuatayo: kuongeza joto kwenye udongo, kuzuia ukuaji wa magugu na kuweka matunda katika hali ya usafi. Kama utashindwa gharama za kununua hayo makaratasi basi tumia nyasi zilizokauka vizuri, zisiwe na miiba au mbegu, ili zisiweze kuota tena shambani au kumjeruhi mkulima.

Umwagiliaji unaofaa ni muhimu sana kuanzia kupanda hadi matunda yanavyoanza kutokeza, vile vile matikiti yanahitaji kina cha maji kwenye udongo cha inchi 1 hadi inchi 2 kwa wiki ili kuweza kusaidia mmea tangu kuota, kukua, kutoa maua na kutengeneza matunda.

Hakikisha udongo unakua na maji muda wote lakini isiwe hali ya mafuriko. Mwagilia chini ya matawi au majani muda wa asubuhi, usilowanishe sana majani epuka kumwagilia juu ya majani (Overhead watering) hii ni kwa sababu athari ya magonjwa ya ukungu. Punguza kiwango cha kumwagilia kadri matunda yanavyokua. Hali ya ukavu huyafanya matunda kuwa matamu sana.

Unapochagua kutumia mbolea hakikisha unatumia mbolea zenye nitrojeni (N) nyingi kuliko mbolea zenye Fosforasi (P) na Potasiamu (K) kwa kipindi cha mwanzo wa ukuaji wa mmea, Baada ya maua kutunga tumia mbolea zenye Nitrojeni kidogo kama CAN, N.P.K yenye uwiano mdogo wa Nitrojeni kulinganisha na virutubisho vingine pamoja na mbolea za maji (foliar fertilizer)

Kupunguza matawi ya matikiti ni muhimu sana, lakini uzalishaji utaongezeka pale ambapo utakuwa unapunguza mashine ya Pembeni na kuliacha shina kuu kuendelea kukua. Mmea unavyokua mchanga kata sehemu ya mwisho ya shina mpaka itakapokua shina kamili. Pia unaweza kutoa baadhi ya maua ili kubakia na maua machache kwa lengo la kutunza akiba ya chakula itakayosaidia kukuza vizuri matunda machache.

Mashina ya matikiti hutengeneza maua ya kiume na ya kike yanayotofautiana katika mmea mmoja. Mara nyingi mmea wa matikiti hutengeneza maua ya kiume wiki kadhaa kabla ya maua ya kike kuanza kutokea. Usijali wala usihofu pale unapooa baadhi ya maua ya kiume yanaanguka. Maua ya Kike (ambayo yana uvimbe mdogo kwa chini) yatabakia kwenye shina kubeba matunda.

Maua ya matikiti huhitaji uchavushaji ili kutengeneza matunda, kwa hiyo uwe makini sana kwa wadudu kama Nyuki, yani usiwaangamize kwa madawa kwa sababu hao ndio wanafanya uchavushaji. Matunda yanavyokua yanaelekea kukomaa na kuiva, zuia kuoza kwa matunda kwa kuweka nyasi kavu au maboksi chini ya tunda kati yake na udongo.

PALIZI
Ni muhimu kupalilia shamba kwa kuondoa magugu ambayo hushindana na mmea kufyonza maji na virutubisho. Palizi hii ifanyike wiki ya tatu au ya pili baada ya mbegu kuota kwa kutumia jembe la mkono au madawa ya kuuwa magugu kama Roundup, 2,4-D n.k

MAGONJWA NA WADUDU WAHARIBIFU
Magonjwa makuu ya matikiti maji ni Leaf spot, dumping off, powdery mildew na blight. Pia yanakumbwa na wadudu kama Beetles, mites, leaf miners na thrips.

1. Magonjwa
Dumping off ni ugonjwa wa ukungu ambao husababisha mbegu kuoza kabla ya kuota.

...Picha yake itakujia hivi karibuni

2. Wadudu waharibifu
Spider mites ni wadudu wanaoathiri sana matikiti maji hasa wakati wa joto, kipindi cha kiangazi na wannyonya majimaji ya ndani ya mmea na wanaangusha majani ya matikiti kwa wiki chache tu.

...Picha yake itakujia hivi karibuni

Leaf miners wanajeruhi majani, hali inayopelekea kuharibu tishu za mmea.

...Picha yake itakujia hivi karibuni

Thrips ni wadudu wanaovamia maua na kufyonza Majimaji ya mmea, hawa wadudu wanaonekana kwa macho ya kawaida.

...Picha yake itakujia hivi karibuni

NAMNA YA UDHIBITI
Namna ya kudhibiti hawa wadudu waharibifu na magonjwa tumia dawa za ukungu, na za wadudu zinazopatikana kwenye maduka ya pembejeo za kilimo. Pia hakikisha shamba lako lipo katika hali ya usafi ikiwa ni pamoja na kuondoa magugu, shamba safi hudhibiti magonjwa na wadudu waharibifu.

Hakikisha unasoma lebo za dawa uliyonunua ili ujue matumizi sahihi ya dawa husika, hii haitasaidia tu kulinda mmea wako, bali itakusaidia pia kutunza mazingira yanayokuzunguka. Pulizia hayo madawa kwa kutumia vifaa sahihi vya kujikinga (Protective gears).

MAVUNO
Kukomaa kwa matikiti hutegemea aina ya tikiti lenyewe. Kama nilivyokwisha kueleza hapo juu kwamba aina ya matikiti hutofautiana zenyewe kwa kulinganisha idadi ya siku za kukomaa kuanzia siku 75 hadi 100. Ili kujua kama matunda yako yamekomaa, ligeuze tunda alafu angalia sehemu ya chini iliyokalia udongo, Ukiona kuna michilizi ya njano basi matikiti yako yamekomaa na yapo tayari kwa kuvunwa. Pia namna nyingine ya kutambua kama matiki yako yamekomaa unayagonga kidogo, ukisikia kama sauti ya chombo kilichowazi basi tikiti lako limekomaa. Hekta moja huzalisha matunda 30,000 hadi 37,500 sawa na tani 360 - 450 na kuendelea kwa hekta moja, hii ni kwa wastani wa kilogramu 12 kwa tikiti moja.

<<< BOFYA HAPA KUSOMA SEHEMU YA PILI <<<

MWISHO WA MAKALA HII

Makala hii Imehaririwa mara ya mwisho tarehe: 07/07/2017

Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

Previous Post Next Post