Ufugaji wa Kuku wa kienyeji - Sehemu ya Tatu (Indigenous Chicken Farming - Part three)


SEHEMU YA TATU

MAGONJWA YA KUKU
Udhibiti wa magonjwa mbalimbali ya kuku ni muhimu sana kwa mfugaji, udhibiti huo ni pamoja na Kukinga kuku wako dhidi ya magonjwa ambukizi kwa kuwapa Chanjo mbalimbali pamoja na kuzingatia usafi wa banda na chakula. Pia udhibiti wa magonjwa ni pamoja na kuwatibu kuku mara wanapoumwa. Asilimia kubwa magonjwa yanayoathiri wa kuku ni yale yanayodhibitiwa na Chanjo, Kwa hiyo ukizingatia utoaji wa chanjo kwa kuku wako kama inavyofaa kitaalamu, utaweza kidhibiti vifo vya kuku kutokana na magonjwa kwa asilimia kubwa.

Mambo Muhimu ya kuzingatia ili Kufanikisha chanjo bora
Chanjo mbalimbali za kukinga magonjwa zina utaratibu wake kitaalamu, kama namna ya utunzaji na namna kuwapa kuku. Zifuatazo ni dondoo muhimu za kufahamu ili chanjo yako ifanikiwe;

1. Ukihifadhi chanjo yako hovyo hovyo bila kufwata maelekezo ya kitaalamu, chanjo hiyo inakua Sumu badala ya kuwa kinga na tiba. Chanjo iliyohifadhiwa vibaya haiwezi kufanikisha matibabu. Chupa za chanjo huwa zinakuwa na lebo au karatasi yenye maelekezo ya jinsi ya kutumia pamoja na tarehe ya mwisho ya matumizi (Expire date). Usipochanja kuku wako vizuri, ugonjwa unaweza kuenea zaidi.

2. Vifaranga vilivyoanguliwa huweza kuwa na magonjwa mbalimbali yaliyotoka kwa Mama kuku, kupitia yai. Kwa hiyo kuwachanja kuku walio na umri chini ya siku kumi (10) ni muhimu sana, kwa sababu itazuia magonjwa ambukizi kwa vifaranga kadri wanavyokua.

3. Kila chanjo imetengenezwa kwa kuwekwa mahali sahihi kwenye mwili wa kuku, kuna baadhi huwekwa kwenye macho, baadhi kwenye maji na baadhi huchomwa kwa sindano kwenye mabawa. Kwa hiyo usibadilishe matumizi ya chanjo.

4. Usiwape chanjo kuku Waliokwisha kuugua [Isipokua kama kuna mlipuko wa ugonjwa wa Laryngotracheitis au Fowl pox]

5. Hifadhi chanjo mahali salama pasipokua na joto & mwanga wa jua wa moja kwa moja.

6. Chanjo zilizo nyingi ni viumbe hai visivyoonekana kwa macho (Living micro-organisms) au chembe chembe zinazotengeneza magonjwa (disease-producing agents), Kwa hiyo hifadhi chanjo zako kwa Uangalifu.

7. Kama unatumia maji ya kunywa kuku kama njia ya kuwapa chanjo, hakikisha Unatumia maji yasiyokua na chumvi na Chlorine, kwa sababu chembechembe au viumbe waliopo kwenye chanjo huharibiwa na hizo kemikali.

8. Baada ya kutoa chanjo hakikisha unachoma au unavitibu (Kuosha na Kemikali inayoua vimelea vya magonjwa, Disinfect) vifaa vyote ulivyotumia wakati wa kutoa chanjo. Ukifanya hivi utazuia kueneza magonjwa kwa kuku wazima wasiokua magonjwa.

MAGONJWA YA KUKU NA UDHIBITI WAKE

1. MUHARO MWEKUNDU (COCCIDIOSIS)
Ugonjwa huu husababishwa na vimelea vinavyoitwa Coccidian, vimelea hivi huzaliana haraka sana kwenye utumbo mwembamba wa kuku. Mara nyingi ugonjwa huu huwakumba kuku walio na umri wa wiki 8 hadi 10, mara nyingi ugonjwa huu unaweza ukaua kuku kwa muda mfupi wa siku 5 hadi 7 (Acute type) au unaweza ukaua Kuku baada ya muda mrefu kupita (Chronic type).

Dalili za Ugonjwa
  • Kuku wanakua dhaifu, wanazubaa na kuinamisha kichwa chini
  • Kuku wanakua na manyoya yaliyovurugika
  • Kuku wanapauka mdomo na miguu
  • Kuku wanatoa kinyesi cha damu, hii hutokea endapo vimelea vya ugonjwa huu vikizaliana kwenye utumbo mpana wa kuku.
  • Kuku wanakufa wengi kwa muda mfupi.


Picha: Mharo wa damu


Namna ya kudhibiti
  • Tumia dawa za Salfa (Sulphur drugs) kwa matibabu
  • Tumia dawa za kuzuia kuzaliana kwa vimelea wa ugonjwa huu (Coccidiostat) kwa kuweka kwenye Chakula.
  • Hakisha banda linakuwa kavu wakati wote, kama unatumia mapumba ya mpunga au malanda ya mbao kwa kuweka chini, basi zingatia usafi yaani badilisha mapumba hayo au malanda yaliyoloana na kuweka Makavu.

2. KIPINDUPINDU CHA KUKU (FOWL CHOLERA)
Ugonjwa huu husababishwa na vimelea vinavyoitwa Pasteurella avicida na vimelea vingine vinavyozaliana kwa kasi sana ndani ya damu na kusababisha sumu. Kuku wagonjwa, Ndege wa mwituni, binadamu, wanyama na vifaaa mbalimbali husambaza ugonjwa huu kwa kiasi kikubwa.

Dalili za Ugonjwa
  • Kuku wanatoa majimaji au udenda wa rangi ya manjano
  • Kuku wanaharisha uhalo wa njano au wa kijani
  • Kuku wananyong'onyea kama wamemwagiwa maji
  • Kuku wanapatwa na homa na wanalala kila wakati
  • Kuku wanakaa wakiwa wameinamisha kichwa chini au wanageuza kichwa uelekeo wa mkia au wanalaza kichwa juu ya mabawa uelekeo wa mkia.
Picha: Kinyesi cha kuku mgonjwa




Namna ya kudhibiti
  • Teketeza au choma moto kuku wote waliokufa ghafra
  • Hakikisha banda la kuku linakua safi wakati wote
  • Tumia dawa za Salfa (Sulphur drugs) kuwatibu kuku waliougua
  • Hakikisha hakuna unyevuunyevu ndani ya banda kwa kubadilisha mapumba ya mpunga au malanda ya mbao yaliyoloana, kwa sababu unyevu unyevu ndani ya banda husababisha kuzaliana kwa vimelea (Coccidian) vya ugonjwa huu.
<<< BOFYA HAPA KUSOMA SEHEMU YA PILI <<<


Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

Previous Post Next Post