Ufugaji wa Kuku wa kienyeji - Sehemu ya Pili (Indigenous Chicken Farming - Part two)


SEHEMU YA PILI

UZURI WA KUKU WA KIENYEJI
1. Ladha ya Nyama na mayai yake ni tamu sana na hupendelewa na watu wengi kulinganisha na kuku wa kisasa.
2. Mtaji wa kuanzia kufuga kuku hawa wa kienyeji ni kidogo sana kulinganisha na kuku wa kisasa.
3. Wanavumilia sana mazingira hatarishi ikiwa ni pamoja na magonjwa
4. Wanalishwa vyakula vya gharama ya chini vinavyopatikana kwenye mazingira ya mfugaji
5. Wakiachiwa wajitafutie wenyewe, gharama za chakula zinakua ndogo kwa mfugaji.
6. Maranyingi Wanawake na watoto, wanajipatia kipato chao kutokana na ufugaji wa kuku.
7. Soko la kuku na mayai ya kienyeji linapatikana kwa kiasi kikubwa.
8. Kinyesi chao ni mbolea nzuri sana kwa mazao ya bustani na mazao mengine.

KWA NINI UNATAKIWA KUBOLESHA UFUGAJI WA KUKU HAWA?
1. Hali ya kuku kufa kutokana na magonjwa itapungua kwa kiasi kikubwa.
2. Ukifikia hatua ya kuangua mayai na kuuza vifaranga, mapato yako yataongezeka sana (mara 7 zaidi) kuliko kuuza mayai.
3. Kuangua mayai mengi kwa wakati mmoja hupelekea vifranga wengi kupatikana kwa wakati mmoja hivyo kusaidia taratibu za chanjo kufanyika vizuri na kwa ufanisi.
4. Utaweza kushirikiana na wafugaji wenzako, hivyo kwa wafugaji wenye kuku wachache wataweza kupata chanjo kwa bei ndogo ya kuchangiana.
5. Unaweza kupanga uzalishaji wa kuku wako ili kuteka soko hususani wakati wa sikukuu kubwa kama Christmas, Pasaka (Easter), Iddi na sherehe mbalimbali, utaratibu huu utakuongezea kipato kwa kiasi kikubwa.

JINSI YA KUANZA KUFUGA
Kabla ya kuanza ufugaji jitahidi uwe na mahitaji yafuatayo;
1. Uwiano wa kuku jike na jogoo uwe 10:1, yaani kila kuku jike (tetea) 10 jogoo awe mmoja. Ina maana kwamba kama una kuku jike 30, jogoo wawe watatu (3).
2. Maji na vifaa vya kulishia & kunywea maji
3. Banda la kuku la kutosha.
4. Sehemu ya kutagia mayai
5. Maranda ya mbao au mapumba ya mpunga kwa ajili ya kuweka juu ya sakafu la banda, ili kuongeza joto bandani.
6. Madawa ya kutibu na kukinga magonjwa (Drugs and Vaccines)

KUCHAGUA KUKU WA MBEGU (BREEDING STOCK)
1. Chagua kuku jike mwenye afya, umbile zuri na mkubwa, pia ambaye hasusi mayai wakati wa kuatamia, pia anayetunza vizuri vifaranga wake.
2. Chagua jogoo mwenye afya, mkubwa na mwenye nguvu.



SIFA ZA BANDA
Banda kubwa na lenye hewa ya kutosha ndilo linalofaa kwa ufugaji bora wa kuku wa kienyeji. Sifa nyingine nyingi za banda bora nimezieleza kwa undani kwenye Sehemu ya kwanza ya makala hii, bofya hapa kuona sifa hizo. Bofya hapa kurejea sehemu ya kwanza ya Makala hii.

MABORESHO YA UFUGAJI BORA
1. Chakula, Chanjo na Matibabu mara tu Wanapougua
  • Andaa chakula chenye lishe mbali mbali (Balanced diet), kwa mfano Pumba, Mashudu, kiasi kidogo cha dagaa waliosagwa na mboga za majani, pia kuku watajiongezea virutubisho wakila wadudu waliopo kwenye mazingira yao.
  • Wapatie maji ya kutosha wakati wote.
  • Wapatie chanjo za kuwakinga na Magonjwa
  • Watibu mara tu wanapougua.
2. Usafi wa Banda
  • Hakikisha banda linakua safi wakati wote, ili kuwakinga kuku wasipatwe na magonjwa mbalimbali yakiwemo ya mlipuko. 

3. Kukusanya mayai
  • Sehemu ya kutagia mayai lazima iwe salama, kavu na yenye kiza kidogo.
  • Kusanya mayai kila siku andika tarehe ya kutagwa yai hilo juu ya yai kwa kutumia penseli. Hakikisha unahifadhi mayai kwenye trei, sehemu pana ya yai iangalie juu na sehemu nyembamba iliyochongoka iangalie chini, kwa sababu sehemu hiyo pana ina kimfuko cha hewa ambacho husaidia kifaranga kukua kikiwa ndani ya yai.
  • Tunza mayai yako sehemu ya chini ndani ya nyumba, kwa sababu sehemu ya chini ndani ya nyumba kuna joto la kadri tofauti na sehemu ya juu. Joto linalotakiwa ili kutunza uhai wa yai ni sentigredi 10 hadi sentigredi 21 (10°C - 21°C)
  • Usioshe mayai na maji, "chonde chonde usioshe mayai na maji" kwa sababu ukiosha na maji bacteria wanaweza wakaingia ndani ya yai kupitia gamba la yai. Kama mayai yako yana udongo, yafute kwa karatasi kavu au kitambaa kikavu au tauro kavu. Kama limechafuka sana halifai kwa kuanguliwa.
  • Chunguza mayai yako kama yamevunjika au yana kreki au yaliyokua na shepu mbaya, mayai ya namna hiyo hayafai kuanguliwa au kuatamiwa.
  •  Wakati wa kuweka alama au tarehe za kutagwa kwenye mayai, tumia penseli. Usithubutu kutumia kalamu ya wino au mark pen au kuweka alama ya kudumu ya wino, kwa sababu baadhi ya wino huwa na sumu inayoweza kuharibu kiini cha ndani cha yai.
  •  Kuandika tarehe ya kutagwa kwenye yai ni jambo la msingi sana kwa sababu utaweza kujua umri wa yai tangu kutagwa.
NB:
* Mayai yanayofaa kuanguliwa ni yale yenye umri wa siku 7 hadi 10, mayai yenye umri zaidi ya siku 10 hayafai kuanguliwa kwa sababu uwezo wake unakua mdogo sana. *

4. Kuangua mayai / Kuatamia
  • Tumia mayai yaliyotagwa si zaidi ya wiki mbili zilizopita
  • Angua vifaranga kwa kutumia mama kuku, au kuku wengine wanaoatamia, au bata au mashine ya kutotoreshea (incubator).
  • Kwa kuku na bata hakikisha unawapa idadi ya mayai kulingana na ukubwa wa maumbile yao, yaani lazima mayai yatoshe chini ya matumbo yao wakati wa kuatamia.
  • Baada ya kuangua mayai safisha maeneo ya kutagia pamoja na kutupa maganda ya mayai yaliyoanguliwa.
  • Kama unatumia mashine ya kuangulia mayai, hakikisha unageuza mayai angalau kwa siku mara 3, isipokua siku tatu za mwisho kuelekea kuangua vifaranga (Siku ya 1 hadi 18: Geuza mayai, Siku ya 19 hadi 21: Usigeuze mayai)
KULEA VIFARANGA
1. Wapatie maji safi na salama wakati wote
2. Wapatie vyakula laini kama unga wa nafaka au mazao ya mizizi.
3. Waruhusu vifaranga watembee kwa uhuru, wakifikia wiki 3 au 4.
4. Wapatie vifaranga wako chanjo ya KIDELI wakiwa na umri wa siku 4 tangu kuzaliwa.

KUWEKA KUMBUKUMBU
Mfugaji anapaswa aweke kumbukumbu kimaandishi kwa kila anachokifanya kwenye mradi wake, hii itamsaidia kumpa dira mfugaji kama anafuga kwa hasara au kwa faida. Mfano wa kumbukumbu anazoweza kuandaa ni pamoja na Gharama za kuanzisha mradi, gharama za kendeshea mradi kama chakula na usafiri, idadi ya kuku jike, Majogoo, vifaranga, idadi ya mayai yanayokusanywa kwa siku au wiki au mwezi, Idadi ya mayai yaliyoanguliwa na taarifa nyingine muhimu.

<<< BOFYA HAPA KUSOMA SEHEMU YA KWANZA <<<


Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

Previous Post Next Post