Kilimo bora cha Mahindi (Growing Maize)


Zao la mahindi (Zee mays) hulimwa maeneo mbalimbali hapa nchini Tanzania, Zao hili hustawi vizuri maeneo yenye halijoto mbali mbali kama; hali ya joto la kadiri na baridi kiasi. Mbegu za kisasa za aina mbalimbali zimekua zikitumika kulingana na hali ya hewa ya eneo husika. Nchini Tanzania aina mbalimbali za mbegu za mahindi zimekua zikizalishwa kukidhi mahitaji ya mkulima na kwenda sambamba na mabadiliko ya tabia ya nchi.

MAZINGIRA
Zao la mahindi linapendelea hali joto ya kadiri na baridi kiasi kuanzia sentigredi 6°C hadi 28°C. Vilevile mahindi yanahitaji udongo wenye rutuba na usiotwamisha maji, pia kiasi cha tindikali ya udogo knachohitajika ni kuanzia  pH 5.5 hadi pH 7. Kiasi cha Tindikali kikiongezeka (<5.5) uzalishaji wa mazao hupungua sana kwa sababu mizizi ya mahindi itashindwa kukua hivyo kupunguza uwezo wa mizizi kuchukua virutubisho kwenye udongo.

Kama udongo wako una kiasi kikubwa cha asidi, tumia Chokaa (Lime) na Gypsum kudhibiti hali hii.

AINA
Mbegu za mahindi zimegawanyika katika makundi matatu kulingana na siku za kukomaa (maturity period). Makundi hayo ni kama yafuatayo;

1. Mbegu zinazokomaa mapema (Early maturity)
-Mbegu hizi hukomaa mapema sana kuanzia Siku 80 hadi siku 100.
2. Mbegu zinazokomaa muda wa kati (Medium maturity)
-Mbegu hizi hukomaa muda wa kati kuanzia siku 115 hadi siku 140.
3. Mbegu zinazochelewa kukomaa (Late or Full season maturity)
-Mbegu hizi huchelewa kukomaa kuanzia siku 150 na kuendelea.

Nchini Tanzania aina mbalimbali za mbegu chotara za mahindi zimekua zikitumiwa na wakulima waliowengi. Zifuatazo ni aina za mbegu chotara za Mahindi zinazozalishwa nchini Tanzania.

1. Uyole Hybrid ( UH 6603 na UH 615)
2. TMV ( TMV1, TMV2 na nyinginezo)
3. SITUKA
4. Meru

Vile vile mbegu za mahindi chotara za nchi jirani zimekua zikitumiwa na wakulima wa Tanzania. Mbegu hizo ni kama zifuatazo;

1. SEEDCO
2. PANNAR
3. Na nyinginezo nyingi.

NAMNA YA KUZITAMBUA MBEGU ORIJINO NA FEKI
Sekta ya kilimo hususani upande wa pembejeo za kilimo, umevamiwa sana watu wasio waaminifu kwa maana kwamba wanazalisha na kusambaza pembejeo feki. Makampuni ya mbegu nao wanajitahidi kwa kadri wanavyoweza kuandaa mbegu zao katika hali ya usasa zaidi ili kuzitofautisha na mbegu feki.

Zifuatazo ni njia za kuzitambua mbegu feki au orijino;

1. Mbegu orijino lazima iwe imethibitishwa na taasisi husika inayohakiki ubora wa mbegu. kwa mfano nchini Tanzania kuna taasisi ya kiserikali inayohakiki ubora wa mbegu inayoitwa TOSCI (Tanzania Official Seed Certification Institute). Mbegu yoyote orijino lazima iwe na kibandiko cha TOSCI. kama haina itakuwa ni feki.

Vilevile kuna baadhi ya mbegu mfano Pannar huwa zinakua na kibandiko cha rangi ya bluu kichoonyesha uthibitisho wa ubora wa mbegu hiyo kutoka kwenye taasisi ya nchi husika kama Zambia au Afrika kusini, kama haina kibandiko hicho itakua ni feki.

2. Kifungashio cha mbegu orijino lazima kiwe na tarehe ya mbegu ilipotengenezwa, kwa sababu kitaalamu mbegu lazima itumike ndani ya miezi sita tangu kufungashwa kiwandani. Baada ya miezi sita kupita inatakiwa mbegu hiyo irudishwe kiwandani kwa ajili ya kufanyiwa majaribio kama bado ina ubora wa kuota au haupo.

ANGALIZO
Ili kujihakikishia ununuzi mzuri wa mbegu kwenye maduka ya pembejeo ni vema kudai risiti, Risiti hii lazima ionyeshe jina la mwenye duka, aina ya mbegu uliyonunua. Umuhimu wa risiti ni kukusaidia kipindi ambapo utakuta mbegu uliyonunua isipoota vizuri au ikiwa feki.

Pia ni muhimu kutunza baadhi ya vifungashio vilivyotumika ili vikusaidie siku za usoni patakapotokea changamoto yoyote itakayohitaji kuhakiki ubora wa mbegu uliyonunua.

KUANDAA SHAMBA
Shamba la kupanda mahindi lazima liandaliwe vizuri, lilimwe kina cha kutosha cha sentimita 30 ili kuruhusu mizizi ya mahindi kuchukua virutubisho kwa urahisi kwenye udongo.

KUPANDA
Mahindi yapandwe mapema baada tu ya mvua za masika kuanza kunyesha, mara nyingi kwa upande wa nyanda za juu kusini mvua za kupandia huwa ni kuanzia wezi wa 11.

Mahindi yanapandwa kwa Mbolea au bila mbolea inategemeana na rutuba ya udongo.

Kama utapanda kwa mbolea za viwandani, cha msingi ufwate taratibu za kupanda yaani uhakikishe mbolea hiyo haigusani na mbegu. Kwamba ukichimba shimo weka mbolea kifuniko kimoja cha mbolea kama unapanda mbegu 1 kwa shimo na vifuniko viwili kama utaweka mbegu 2, kisha funika na udongo kiasi halafu weka mbegu juu, halafu tena funika na udongo kiasi.

Kama hutaki kutumia mbolea wakati wa kupanda, unaweza ukapanda kawaida bila mbolea halafu baada ya wiki mbili uchomekee mbolea ya kupandia.

Nafasi ya kupanda mahindi ni sentimita 25 au 30 shina hadi shina na sentimita 60 hadi 75 mstari hadi mstari. Nafasi hii huwa ni mbegu moja kwa kila shimo.

Picha: Muonekano wa sm 25 shimo hadi shimo na sm75 mstari hadi mstari. 
(* Bofya picha  kuona vizuri)

Picha: Kuweka mbolea na kupanda

TAZAMA VIDEO HAPA CHINI KUJUA ZAIDI NAMNA YA KUPANDA KWA KUTUMIA MBOLEA


KUTUNZA SHAMBA
Mahindi yanaota baada siku 5 hadi 7, muda huu ni  ndio wakati wa kuchunguza uotaji wa mahindi yako kama yameota yote au lah, Baada ya wiki 2 tangu kupanda punguzia mashina na rudishia zile sehemu ambazo hazijaota, aidha kwa kupanda mbegu zingine ama kwa kupandikiza mashina yaliyotolewa sehemu nyingine.

1. Palizi
Palizi ya kwanza hufanyika baada ya wiki mbili tangu kupanda

2. Kupiga dawa za kuua Viwavi (Maize stalk bore)
Chunguza mahindi yako kila wakati tangu yakiwa madogo (wiki moja) kama kutakuwa na wadudu hawa. Kama wapo tumia dawa za kuua wadudu hawa zinazopatikana kwenye maduka ya pembejeo.

3. Mbolea za kukuzia
Baada ya siku 30 hadi 48 piga palizi ya pili pamoja na kuweka mbolea ya kukuzia kama UREA, N.P.K na nyinginezo.

Kama kuna haja ya kuweka mbolea ya kukuzia kwa mara ya pili unaweza kutumia mbolea ya kubebea kama CAN. mbolea hii huwekwa wakati mahindi yanakaribia kutoa mbelewele.

Baada ya kuweka mbolea endelea kuchunguza mahindi yako ili kubaini magonjwa au wadudu waharibifu

PICHANI : Shamba la mahindi lililotunzwa vizuri

PICHANI: Muonekano wa sentimita 25 shina hadi shina

KUVUNA
Mahindi huwa tayari kuvunwa baada ya kuona yamekauka na yamebadilika rangi kuwa kahawia, wakati huu watoto wa mahindi huwa wanalegea na kuangalia chini.

Ni muhimu kuhakikisha mahindi yamekauka vizuri yakiwa shambani ili kuongeza ustahimilivu wakati wa kuhifadhi yaani hayawezi kubunguliwa kwa haraka.

Kama utahudumia vizuri mahindi yako Unaweza kuvuna magunia 40 hadi 50 ya kilo 100 kwa ekari moja kama utapanda mbegu inayozaa mahindi mawili kwa shina. Pia Unaweza kuvuna magunia 25 hadi 35 ya kilo 100 kwa ekari moja kama utapanda mbegu inayozaa muhindi mmoja kwa shina.

KUHIFADHI
Kuhifadhi mazao baada ya kuvuna ni jambo la msingi kwa mkulima kulitilia maanani. Njia za kuhifadhi mazao zipo za aina mbali mbali kama ifuatavyo;

1. Kutumia kemikali za maji au poda
Kuna dawa mbali mbali za kuhifadhi mahindi gharani ili kuzuia ubunguaji, zote hizo zinapatikana kwenye maduka ya pembejeo.

2. Kutumia mifuko maalumu
Mifuko hii inaangamiza au kuzuida wadudu wa gharani kwa kumnyima hewa mdudu huyo na kumsababishia asiweze kuishi. Mifuko hiyo ni kama PICS na AGROZEB

3. Kutumia mapipa maalumu (Silo tank)
Mfumo wa mapipa haya yanafanana na mifuko maalumu ya PICS au AGROZEB kwamba kinachofanyika ni kumnyima hewa mdudu ili asiweze kuishi, mapipa haya yana mifuniko thabiti inayozuia hewa kuingia ndani ya pipa.

4. Kutumia gesi ya kemikali (Fumigants)
Mfumo huu ni mzuri sana, ubora wake ni kama ukitumia mifuko ya PICS au AGROZEB kwani hauachi mabaki ya sumu za kemikali kwenye mazao.

Njia hii inatumia vidonge vya sumu (tablets/ Plates) ambavyo hubadilika kuwa gesi yenye sumu baada ya kuachwa wazi. Masharti ya njia hii lazima upange vizuri magunia yako ndani ya chumba ambacho hakiingizi hewa, baadae weka vidonge vyako ndani ya chumba hicho halafu kifunge mpaka siku utakapohitaji kutumia mazao hayo. Pia unaweza ukatumia maturubai yaani ufunike mzigo wako wa mahindi vizuri kiasi ambacho hewa haiwezi kupita kwa urahisi alafu weka vidonge hivyo ndani ya turubai.

Dawa hizi za gesi ya kemikali (fumigants) zipo za aina nyingi lakini kuna makundi mawili ya dawa hizo kama ifuatavyo;

1. Phosphine (PH3)
Kundi hili linakuwa na aina zifuatazo; Aluminium Phosphide (Phostoxin) tablets au Methyl Phosphide (Magtoxin) tablets.

2. Methyl  bromide,  CH3Br (Bromomethane/  BromoGas)  
Kundi hili linakua na aina ya Bromo methane/ Bromo gas

MUHIMU
Zifahamu Kanuni 10 za kilimo bora

1. Kuandaa shamba mapema

2. Kulima kwa wakati

3. Kupanda kwa wakati kwa kutumia mbegu bora

4. Kupanda kwa mistari au kwa nafasi

5. Kutumia mbolea (Mbolea ya kupandia na kukuzia)

6. Kupalilia kwa wakati

7. Kuangamiza wadudu waharibifu na magonjwa

8. Zuia magonjwa vamizi

9. Vuna kwa wakati

10. Hifazi mazao vizuri

*** MWISHO WA MAKALA HII ***

Makala hii Imehaririwa mara ya mwisho Tarehe: 16/01/2018

Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

Previous Post Next Post