Wafuatao ni wadudu waharibifu
wanaoharibu zao la bamia, nimeeleza mambo mengi yanayomuhusu mdudu husika
pamoja namna ya kumdhibiti.
1. Cutworms (Agrotis spp)
Hawa ni viwavi wenye rangi ya kijivu, wanakata mashina ya
miche michanga usawa wa ardhi, wanafanya uharibifu huu wakati wa usiku na
wakati wa mchana hujificha ndani ya udongo.
Picha: Kipepeo wa Cutworms, Photo Credit: www.extension.umn.edu
Picha: Cutworms jamii ya Kiwavi jeshi, Photo Credit: Joseph Berger, www.canolawatch.org
Picha: Cutworms wa kawaida, Photo Credit: John Obermeyer, Purdue University; www.almanac.com
Namna ya kuwadhibiti
- Andaa au lima shamba lako vizuri ili kuwaacha viwavi hawa peupe au juu ya ardhi, ili waweze kuliwa na wadudu au wanyama wengine pia wakiwa juu ya ardhi wanakufa kwa jua. Kama shamba lako litapandwa muda mfupi baada ya kulimwa, kuna hatari ya hawa viwavi kuvamia miche ya bamia.
- Hakikisha usafi wa shamba kila wakati kwani magugu yakiwa mengi yanavutia uwepo wa viwavi hawa.
2. Cotton Seed bugs (Oxucarenus
spp)
Wadudu hawa ni wadogo wana urefu wa mm 4 hadi 6 na wana
rangi nyeusi. Mabawa yao yanang'aa mfano wa kioo. Wadudu hawa wanakula matunda
madogo yanayokua. Hatua ya ukuaji ya buu na mdudu kamili hufyonza maji maji na
chakula kwenye mbegu za matunda machanga na kuzuia matunda kushindwa kukomaa.
Mara nyingi wadudu hawa huonekana wakati wa kutoa maua, kuchanua maua na wakati
wa kutengeneza matunda. Wadudu hawa hawaathiri sana uzalishaji wa bamia, kama
ni wachache sana unaweza kuwaacha tu bila kuwadhibiti.
Picha: Cotton Seed bugs, Photo Credit: James D. Young, www.blogs.ifas.ufl.edu
Picha: Cotton Seeds bugs, Photo Credit: www.infonet-biovision.org
Namna ya kuwadhibiti
- Hakuna haja ya kuwadhibiti kwani wana athari ndogo sana.
- Unaweza kuwaondoa tu kwa kutingisha mmea ili kuwadondosha.
3. African bollworm (Helicoverpa armigera)
Viwavi hawa wanakula majani, maua na matunda. Athari kubwa
sana huonekana kwenye maua na matunda ya bamia. Viwavi hawa huvamia maua na
kusababisha maua kudondoka (Flowers abortion). Pia viwavi hawa hutoboa matundu
ya mviringo kwenye matunda na kusabisha tunda la bamia kuoza kutokana na
magonjwa nyemelezi.
Picha: African Bollworm, Photo Credit: www.infonet-biovision.org
Namna ya kuwadhibiti
- Piga dawa mbalimbali za kuua viwavi hawa zinazopatikana kwenye maduka ya pembejeo za kilimo.
- Njia ya kibaolojia kwa kutumia viumbe wengine wanaokula viwavi kama Sisimizi, siafu na wengine.
- Tembelea shamba lako mara kwa mara ili kubaini wadudu hawa, kadri unavyowadhibiti wakiwa wachache ndivyo jinsi wanavyopoteza uwezo wao wa kusambaa.
4. Spiny bollworm or Spotted bollworm (Earias spp)
Kiwavi huyu ndiye anaeathiri sana uzalishaji wa bamia, Akiwa
mkubwa ana urefu wa mm 13 hadi 18 na upana wa mm 2.5. Wanakua na rangi tofauti
kuanzia rangi ya kijivu iliyochangamana na rangi ya kaki, pia wanakua na rangi
kijivu kwenda kijani iliyochangamana na mistari ya mpauko au myeupe. Mdudu
kamili (Kipepeo) anakua na urefu wa mm 12 na upana wa majani wa mm 20 hadi 22.
Mabawa yake ya mbele yanakua na rangi nyeupe, au kijani ya mng'ao au njano
inategemeana na aina ya kipepeo.
Viwavi hawa wanatoboa matawi ya bamia changa na kusababisha
maotea ya matawi kufa. Matunda ya bamia yakianza kuzalishwa viwavi hawa huvamia
maua na matunda madogo ya bamia na baadae huvamia matunda makubwa. Maua na
matunda yaliyoharibiwa hupukutika, hali inayopelekea kushuka kwa uzalishaji.
Uwekaji wa kiasi kikubwa sana cha mbolea zenye Naitrojeni (N) huongeza athari
za kiwavi huyu.
Picha: Kipepeo wa Spiny bollworm
Namna ya kuwadhibiti
- Tembelea shamba lako mara kwa mara ili kubaini athari za viwavi hawa.
- Tumia dawa mbalimbali za kemikali zinazopatikana kwenye maduka ya pembejeo za kilimo.
- Weka mbolea za viwandani kwa kiwango kinachofaa; epuka kuweka kiwango kikubwa sana cha mbolea zenye Nitrojeni.
- Usiwaangamize wadudu wanaokula viwavi hawa kama sisimizi, siafu, beetle na wengine kwani wanadhibiti kasi ya viwavi hawa.
- Tumia dawa za asili kama Mwarobaini, au dawa zingine za viwandani zilizotengenezwa kwa Mwarobaini (Biopesticides-Neem based pesticides)
- Teketeza masalia ya mimea ya bamia baada ya kuvuna.
- Pia unaweza ukawaua kwa kutumia mkono kama shamba lako ni dogo.
5. Spider Mites (Tetranychus spp)
Wadudu hawa wanafanana na buibui, tofauti yao ni kwamba
wadudu hawa ni wadogo sana na wana rangi nyekundu au njano iliyokolea. Buibui
hawa wadogo huvamia majani na kutandaza utando na kuanza kuzaliana, wakiwa
kwenye majani hufyonza majimaji na chakula kwenye mmea.
Majani yaliyoathiriwa yanaonyesha rangi nyeupe hadi njano,
athari ikizidi sana majani yanabadilika rangi na kuwa mekundu sana. Rangi hii
nyekundu ni muonekano wa buibui hawa wakiwa wengi. Athari ikiwa kubwa majani
yanajikunja baadae hukauka na hatimae hudondoka, hali itakayopelekea mmea
kupukutisha najani. Athari ikizidi sana buibui hawa wekundu huvamia matunda.
Hali inayovutia kuutokea na kuzaliana kwa hawa wadudu ni Joto na hali ya ukame
au kiangazi, kuondoshwa kwa wadudu wanaokula buibui hawa (Natural enemies) na
kuwepo kwa mimea mingine iliyohalibiwa sana na wadudu wengine au magonjwa kama
Pamba, Nyanya n.k, hali hii pia huvutia uwepo na kuzaliana kwa buibui hawa.
Picha: Red spider mites wakishambulia mmea, Photo Credit: www.researchgate.net
Picha: Muonekano wa Red spider mites kwa kutumia hadubini (Microscope); Photo credit: www.thebeatsheet.com.au
Namna ya kuwadhibiti
- Tembelea shamba lako mara kwa mara ili kubaini kiwango wa wadudu hawa, hii itakusaidia kujua wakati gani muafaka wa kuanza kupiga dawa.
- Hakikisha shamba lako linakua safi wakati wote kwa kuondoa magugu na kuchoma moto mabaki ya mimea yenye magonjwa na wadudu mara tu baada ya kuvuna.
- Usipande mimea mipya ya bamia karibu na shamba liloathiriwa na wadudu hawa, kama utapanda hakikisha unateketeza masalia yote ya mimea iliyoathiriwa.
- Tumia dawa mbalimbali za kemikali zinazopatikana kwenye maduka ya pembejeo za kilimo.
6. Thrips (Frankliniella spp)
Wadudu hawa au Vithripsi wanakula sehemu ya chini ya Jani,
Maua na Matunda. Hatua mbili za ukuaji wa mdudu huyu yaani Kiwavi na Mdudu
kamili huathiri mmea wa bamia. Wanachofanya wanafyonza majimaji ya mmea yenye
chakula, hatimae huathiri ukuaji na uzalishaji wa mmea.
Majani yaliyoathiriwa na wadudu
hawa hujikunja na kukakamaa, baadae hukauka. Mazingira yoyote yatakayodhoofisha
afya ya mmea husababisha wadudu hawa kuzaliana kwa kasi na kuongeza
mashambulizi kwenye mmea.
Wadudu hawa wakivamia miche
michanga ya bamia husababisha mimea kudumaa. Wakivamia maua husababisha matunda
kupinda au kuwa na sura mbaya. Pia wakivamia matunda ya bamia hutengeneza makovu
kwenye matunda ambayo huaribu ubora na soko la bamia hiyo.
Picha: Muonekano wa Vithripsi kwa kutumia Hadubini (Microscope), Photo Credit: Lance Osborne; www.entnemdept.ufl.edu
Photo Credit: www.infonet-biovision.org
Picha: Mabaka au makovu yaliyosababishwa na Thrips; Photo Credit: www.researchgate.net
Picha: Mabaka au makovu yaliyosababishwa na Thrips; Photo Credit: www.researchgate.net
Namna ya Kuwadhibiti
- Andaa shamba lako kwa kulima na kusawazisha vizuri mabonge ya udongo, hii itasaidia kuwaacha peupe Pupa wa Thrips (Hii ni hatua ya tatu ya ukuaji wa mdudu), Pupa hawa watakufa kwa kupigwa na jua au kwa kuliwa na wadudu wengine.
- Kama watakua wengi, piga dawa za kibaolojia (Biopesticides), Dawa hizi hutengenezwa kwa bakteria maalum ambao husababisha ugonjwa kwa hawa thrips hatimae thrips hufa. Mfano wa dawa hii ni SPINOSAD, Sharti la dawa hii ni kwamba unatakiwa upulizie mapema wakati maua yameanza kutoka. Ukipulizia baadae sana au wakati matunda yameanza kutoka, husababisha kuwepo kwa masalia ya sumu kwenye matunda.
- Tumia dawa nyingine za kemikali zinazopatikana kwenye maduka ya pembejeo za kilimo.
Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo
Post a Comment