Kilimo cha Bamia - Sehemu ya Kwanza (Growing Okra - Part One)


Bamia (Abelmoschus esculentus) ni zao la mbogamboga linalolimwa na wananchi wengi nchini Tanzania, matunda ya zao hili hutumika kwenye vyakula mbalimbali kama supu, kachumbali, kutumika kama mboga n.k. Majani ya zao hili yanaweza kutumika kama mboga na yana virutubisho vya aina nyingi kama Vitamini B6, Folic acid na nyuzinyuzi (Fibre). Zao hili hukomaa haraka sana kati ya siku 50 hadi 60 itategemeana na aina ya bamia na hali ya hewa.

AINA
Zifuatazo ni aina mbalimbali za bamia zinazolimwa nchini Tanzania; Kamini, Pusa mukhamali, Pusa sawani, parbhani kranti, Vaishali, Vagmi, Okra Clemson, Padmini, Clemson spineless, Green Emerald, White velvet na Dwarf velvet Long pod. Sifa za baadhi ya aina hizi za bamia ni kama ifuatazo;

1. Pusa sawani
Aina hii ya bamia huzaa sana na huvumilia ugonjwa wa virusi unaoitwa Vein mosaic. Aina hii inakua hadi kufikia kimo cha mita 2 hadi mita 2.5, ina matunda malefu kuanzia sm 18 hadi sm 20. Matunda yake yana rangi ya kijani iliyoiva na yana ngozi laini. Aina hii inafaa sana kwa kusafirisha nje ya nchi (Mainly for export).


2. Clemson spineless
Aina hii hufikia kimo cha mita 1.2 hadi mita 1.5, matunda yake yana urefu wa sm 15, yana rangi ya kijani.


3. Green Emerald
Aina hii hufika kimo cha mita 1.5 na matunda yake huwa na urefu wa sm 18 hadi sm 20, yana rangi ya kijani iliyopauka na yana urefu wa mviringo.


4. White velvet
Aina hii ina kimo cha wastani wa mita 1.5 hadi mita 1.8, matunda yake yana urefu wa sm 18, yana ngozi laini na weupe wa kung'aa.


5. Dwarf Green Long Pod
Aina hii inakua hadi kufikia urefu wa sentimita 90 au mita 0.9. Matunda yake yana mibinuko na urefu wa sm 18 hadi 20.


MAZINGIRA
Zao la bamia huota na kuzaa vizuri kwenye muinuko hadi mita 1600 kutoka usawa wa bahari. Pia hupendelea udongo wa aina mbalimbali wenye mbolea za asili na wenye pH kuanzia 5.8 hadi 6.5. Udongo wenye pH 5.8 hadi 6.5 ni ule ambao mazao mbalimbali huota vizuri kama Mahindi, maharage, alizeti, karanga n.k. Udongo huo usitwamishe maji na uwe na rutuba ya kutosha. Kama ardhi yako haina rutuba ya kutosha basi weka mbolea za asili.

Zao hili hupendelea maeneo yenye joto la wastani la nyuzi joto 24°C hadi 30°C, bamia inavumilia kidogo sana maeneo yenye baridi chini ya nyuzi joto 24°C , kwa sababu hupelekea mmea kudumaa. Zao hili hupendelea mvua za wastani na linavumilia ukame.

KUPANDA
Bamia hupandwa moja kwa moja shambani, ingawa mara nyingine hupandwa kwenye kitalu halafu baadae hupandikizwa shambani. Kiutaalamu zao hili hupandwa moja kwa moja shambani kwa sababu mbegu zake ni kubwa tofauti na mbegu za nyanya au nyanya chungu ambazo ni ndogo ndogo. Ili kupata matokeo mazuri ya uzalishaji pandia mbolea za asili kama samadi au mboji au changanya samadi na mbolea ya kiwandani ya kupandia.

Ili kuharakisha uotaji wa bamia, loweka mbegu za bamia kwenye maji ya baridi usiku mzima au kuanzia mida ya jioni au usiku mpaka asubuhi, halafu uzipande. Kama ardhi yako ina unyevu wa kutosha labda ni kipindi cha masika na mvua zinanyesha vizuri unaweza ukapanda bila kuloweka. Nchini Tanzania bamia hupandwa moja kwa moja shambani. Kiasi cha mbegu kinachohitajika kwa hekta moja (ekari mbili na nusu) ni kilo 8 hadi 10 za mbegu.

Nafasi ya kupanda bamia ni kama zifuatazo; sm 45 kwa sm 45 au sm 50 kwa sm 30 au sm 60 kwa sm 15 (Mstari hadi mstari kwa shina hadi shina). Kina cha kusia mbegu za bamia ni sm 1.5.

KUTUNZA SHAMBA
Kama ilivyo kwenye mazao mengine zao la bilinganya linahitaji huduma ya kutosha kama kuweka mbolea, kuhakikisha shamba lina unyevu wa kutosha, kupiga palizi, kudhibiti wadudu waharibifu na magonjwa. Yafuatayo ni maelezo ya kina kuhusu namna ya kutunza shamba vizuri;

Matumizi ya mbolea
Zao la bilinganya linahitaji rutuba ya kutosha ila kuongeza uzalishaji, mbolea za viwandani kama DAP, UREA, NPK na CAN zinaweza kutumika kuboresha ukuaji na uzalishaji wa zao hili. Pia unaweza ukatumia mbolea mbalimbli za majani kama Booster na nyinginezo

Kudhibiti Magugu
Hakikisha unapalilia shamba lako vizuri kwani magugu yanavutia uwepo wa wadudu waharbifu na magonjwa. Jambo lingine la msingi ni kwamba wakati wa palizi usiweke udongo mwingi au matuta kwenye mashina ya bamia, kwani udongo ukiwa mwingi husababisha ugonjwa wa kuoza mizizi.

Pia unaweza ukatumia dawa mbalimbali za magugu kuua magugu shambani, inakupasa uwe muangalifu na ufwate maelekezo ya kitaalamu wakati wa kutumia dawa hizi kwani ukikosea jinsi ya kutumia unaweza ukaangamiza mimea yako shambani. Ukinunua dawa hizi za magugu muone au wasiliana na mtaalamu wa kilimo au Afisa kilimo wa eneo lako ili akupe ushauri namna ya kutumia dawa hizi.


Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

Previous Post Next Post