Ufahamu Ugonjwa wa saratani ya Matiti kwa Wanawake (Understand Breast Cancer in Women)

Imehaririwa: October 31, 2019

Saratani ya matiti (Breast cancer) ni aina ya saratani ambayo hutokea kwenye tishu za matiti. Aina zote za saratani hutokea wakati kuna mabadiliko ya vinasaba (mutations) ambavyo hudhibiti ukuaji wa seli, mabadiliko haya ya vinasaba (mutations) huzifanya seli hai kujigawanya na kuongezeka (multiplication) katika utaratibu usiofaa na usioweza kudhibitiwa.

Saratani ya matiti hutokea kwenye seli au tishu za matiti hususani kwenye matezi (Glands) yanayotoa maziwa yanayoitwa 'lobules', pia hutokea kwenye mirija (ducts) inayochukua maziwa kutoka kwenye matezi ya maziwa kupekeka kwenye chuchu (nipple). Vilevile saratani huweza kutokea kwenye tishu za matiti zenye mafuta au kwenye tishu zingine.

Seli za saratani husambaa kwenye titi na kuvamia seli zingine zisizo athirika pia husambaa na huvamia matezi yaliyopo kwenye makwapa (lymph nodes). Matezi hayo (Lymph nodes) ni njia ya awali inayosaidia kusafirisha seli hizo za kansa kwenda maeneo mengine ya mwili.

Kielelezo hapo chini kinaonyesha titi la mama lisilokuwa na saratani


Kielelezo kinachofuata hapo chini kinaonyesha titi la mama lenye saratani (Cancer)




AINA ZA SARATANI YA MATITI
Kuna aina nyingi za saratani ya matiti, zifuatazo ni baadhi ya saratani za matiti;

1. Ductal Carcinoma In Situ
Ni aina ya saratani ya matiti ambayo seli za saratani huanzia ndani ya mirija inayotoa maziwa (ducts) ambayo huchukua maziwa kutoka kwenye tezi za maziwa kupeleka kwenye chuchu. Aina hii ya saratani haisambai maeneo mengine hubakia humo humo kwenye mirija (non-invasive).

2. Invasive Ductal Carcinoma
Ni aina ya saratani ya matiti ambayo seli za saratani huanzia ndani ya mirija inayosafirisha maziwa (ducts) ambayo huchukua maziwa kutoka kwenye tezi za maziwa kupeleka kwenye chuchu. Aina hii ya saratani husambaa na kuvamia tishu zilizopo karibu (Invasive).

3. Triple Negative Breast Cancer
Ni aina ya saratani ambayo seli za saratani kwenye uvimbe wa titi huwa ni hasi (negative) kwa homoni ya Progesterone, Estrogen na Neu receptors (HER2).

4. Inflammatory Breast Cancer
Ni aina ya saratani ambayo haitengenezi uvimbe bali huathiri ngozi ya titi, aina hii ya saratani hutokea mara chache sana.

5. Metastatic Breast Cancer
Ni aina ya saratani ambayo imesambaa maeneo mengine ya mwili kuanzia kwenye matiti kwenda maeneo kama mapafu, mifupa, ubongo n.k.

6. Breast Cancer During Pregnancy
Ni aina ya saratani inayogundulika wakati wa ujauzito.


VISABABISHI
Saratani ya matiti hutokea ambapo seli za matiti huanza kukua isivyokawaida, seli hizo hujigawanya haraka sana (multiplication) na kuongezeka kuliko seli hai zingine, hali inayopelekea seli hizo za saratani kutengeneza mikusanyiko ya mafungu mafungu. Sehemu zilipokusanyika seli hizo hutengeneza vivimbe na baadae saratani hiyo huenea kutoka kwenye matiti kwenda kwenye matezi yaliyopo kwenye makwapa, baada ya hapo huenea sehemu zingine za mwili.

Saratani ya matiti mara nyingi huanzia kwenye matezi ya maziwa (lobules) na kwenye mirija (ducts) inayotoa maziwa kutoka kwenye tezi za maziwa kupeleka kwenye chuchu. Pia saratani hii huweza kutokea kwenye seli au tishu zilizopo sehemu nyingine ndani ya titi.

Watafiti wamegundua kwamba Homoni za mwili, Mienendo ya maisha na Mazingira huweza kuongeza hatari ya mtu kupata ugonjwa huu. Bado kuna changamoto kuwa baadhi ya watu ambao hawana mazingira hatarishi ya kupata ugonjwa huu lakini inagundulika wanao ugonjwa huu. Tafiti mbali mbali zinaeleza kwamba kutakua na uhusiano mkubwa kati ya vinasaba vya mwili (genetic makeup) na mazingira.

MAMBO HATARISHI YANAYOONGEZA UWEZEKANO WA KUPATA UGONJWA HUU (RISK FACTORS)
Haya ni mambo yoyote au hali yoyote itakayoongeza uwezekano wa mwanamke kupata saratani ya matiti, ingawaje sio wanawake wote wanaopata saratani hii husababishwa na mambo haya (risk factors). Wanawake wengi wanaopata saratani hii huwa hakuna sababu mahsusi zilizowapelekea wao kupata ugonjwa huu. Yafuatayo ni baadhi ya mambo hatarishi ambayo huweza kuongeza uwezekano wa kupata ugonjwa huu;

1. Kuwa Mwanamke
Wanawake ndio wenye uwezekano mkubwa wa kupata ugonjwa huu kuliko wanaume.

2. Historia ya tatizo lolote la matiti
Kama una historia ya kufanyiwa upasuaji wowote wa titi kama 'breast biopsy' huweza kuongeza hatari zaidi ya kupata saratani ya matiti.

3. Historia ya kupata saratani ya matiti
Kama umeshawahi kupata saratani hii kwenye titi moja basi kuna uwezekano mkubwa wa titi lingine kupata saratani hii.

4. Historia ya familia kupata ugonjwa huu
Kama wanafamilia wako (mama yako, dada zako n.k.) wameshawahi kupata ugonjwa huu hususani katika umri mdogo basi kuna uwezekano mkubwa wa wewe kupata ugonjwa huu. Ingawaje wanawake wengi wanaogundulika na ugonjwa huu wanakuwa hawana historia yoyote ya wanafamilia wao kuwa na saratani hii.

5. Vinasaba (Genetic makeup)
Vinasaba (DNA) vilivyoharibiwa (gene mutations) na vinavyoweza kusababisha saratani hii huweza kurithiwa kutoka kwa wazazi kwenda kwa mtoto. Vinasaba hivi vinavyosababisha saratani hujulikana kitaalamu kama BRCA1 and BRCA2, vinasaba hivi huongeza hatari ya mtu kupata saratani ya matiti na saratani zingine. Pia TP53 ni aina ya kinasaba ambacho huongeza uwezekano wa mtu kupata ugonjwa huu.

6. Kuwa mazingira yenye mionzi (X-rays)
Kama ulishawahi kupata matibabu ya mionzi (x-rays) kwenye kifua chako wakati ukiwa mdogo au baada ya kubalehe (young adult), inaongeza hatari ya wewe kupata ugonjwa huu.

7. Unene kupita kiasi
Unene kupita kiasi huongeza uwezekano wa wewe kupata ugonjwa huu.

8. Kuanza kupata hedhi wakati wa umri mdogo
Kupata hedhi wakati wa umri mdogo chini ya miaka 12 hoengeza hatari ya msichana huyu kupata ugonjwa huu.

9. Ukomo wa hedhi wakati wa umri mkubwa
Ukichelewa kupata ukomo wa hedhi na ukapata ukomo huo wakati wa umri mkubwa huongeza hatari ya wewe kupata ugonjwa huu.

10. Kupata mtoto wa kwanza wakati wa umri mkubwa
Mwanamke anayepata mtoto wa kwanza baada ya miaka 30 huweza kuongeza uwezekano wa yeye kupata saratani ya matiti.

11. Kutokuwahi kupata ujauzito
Mwanamke ambaye hajawahi kupata ujauzito hadi kufikia umri wa utu uzima (baada ya miaka 30 na kuendelea) huweza kuongeza hatari ya kupata ugonjwa huu kuliko mwanamke ambaye amepata ujauzito mara moja au zaidi.

12. Kunywa pombe kupita kiasi
Kunywa pombe kupita kiasi huweza kuongeza hatari ya mwanamke kupata saratani hii.

NB:
Haya ni baadhi ya mambo hatarishi ambayo huweza kuongeza hatari ya wewe kupata ugonjwa huu, ingawaje sio mara zote mambo haya huweza kuongeza hatari hiyo kwani kuna baadhi ya wanawake hupata saratani hii nje ya mambo niliyoyaeleza hapo juu.


DALILI ZA UGONJWA HUU
Katika hatua za awali za saratani ya matiti huwezi kuona dalili yoyote, hii ina maana kwamba vivimbe vya saratani vilivyopo kwenye matiti huwa ni vidogo sana na huwezi kuvigundua kwa kuminya titi. Ikiwa utahisi vivimbe hivyo vigumu vigumu kwa kuminya titi huenda ikawa mojawapo ya dalili za ugonjwa huu ingawaje sio mara zote kwamba vivimbe huashiria ugonjwa huu. Ugonjwa huu huwa una hatua zake (stages), hatua hizi nitazieleza baada ya kuelezea dalili za ugonjwa huu.

Dalili za ugonjwa huu hutegemea aina mahsusi ya visababishi vyake, mara nyingi dalili hizi hufanana lakini baadhi huwa tofauti. Zifuatazo ni dalili za ugonjwa huu ambazo huwakumba wanawake wengi;

1. Kuwa na vivimbe au vitu vigumu vigumu kwenye titi ambavyo havikuwai kutokea hapo kabla, vivimbe hivi mwanamke atavihisi kwa kuminya titi lake.

2. Maumivu ya matiti, japokua sio maumivu yote ya matiti huashiria saratani hii.

3. Kuwa na vieneo kwenye titi vyenye rangi nyekundu kuzidi eneo lote la titi.

4. Kuvimba titi zima au sehemu ya titi

5. Kutokwa na majimaji kwenye titi yaliyotofauti na maziwa.

6. Kutokwa na damu kwenye chuchu

7. Kubanduka kwa ngozi ya titi au kwenye chuchu, pia kunaweza kukawa na mipasuko kwenye ngozi ya titi au kwenye chuchu.

8. Mabadiliko ya ghafla ya muonekano au ukubwa wa titi.

9. Kupinda kwa chuchu

10. Mabadiliko ya muonekano wa ngozi ya matiti yako

11. Uvimbe kwenye makwapa.

NB:
Ukionekana una baadhi ya dalili nilizozieleza hapo juu, haitamaanisha kwamba una saratani ya matiti, unaweza ukawa nayo au usiwe nayo. Unaweza ukawa na baadhi ya dalili hizo lakini usiwe na saratani hii, kwa mfano; Maumivu ya matiti, wanawake wengi wamekuwa wakipata maumivu ya matiti hususani wakati wa mabadiliko ya homoni zao, kupindi cha hedhi n.k. Pia kuwa na vivimbe (lump) kuna vivimbe vingine vinatokea na kuisha vyenyewe inakuwa sio saratani, vilevile vivimbe hivyo vinaweza kuashiria saratani ya matiti.

Jambo la msingi hapo ni kwamba mara uonapo dalili hizo nilizozieleza hapo juu fika hospitali mara moja kamuone daktari ili ufanyiwe uchunguzi na kubaini kama ni saratani kweli au ugonjwa wa kawaida.

HATUA ZA UKUAJI WA SARATANI YA MATITI
Ni muhimu pia kufahamu hatua za ukuaji wa saratani hii kuanzia hatua ya kwanza hadi ya mwisho. Hatua za saratani hii hugawanywa kulingana na ukubwa wa uvimbe pamoja na namna ilivyoenea kutoka kwenye matiti kuelekea kwenye matezi ya kwenye makwapa (Lymph nodes) na kuelekea sehemu nyingine za mwili. Hatua za ukuaji wa saratani hii umegawanywa katika hatua 5 yaani kuanzia 0 hadi 4, lakini hatua hizi huweza kugawanywa zaidi katika hatua ndogo ndogo. Hatua hizo tano ni kama zifuatazo;

Hatua ya 0
Hatua hii hujulikana kama 'Ductal carcinoma in situ' (DCIS), hutokea wakati seli za saratani huanza kujikusanya na kubakia kwenye mirija (ducts) ya kusafirisha maziwa kutoka kwenye tezi za maziwa kupeleka kwenye chuchu. Katika hatua hii seli za saratani zinakua hazijaenea kwenye tishu za karibu.

Hatua ya 1
Mwanzoni mwa hatua hii vivimbe vyenye seli za saratani huanza kukua na kufikia sm 2, wakati huu seli za saratani zinakua hazijavamia matezi yoyote (Lymph nodes).

Hatua ya 2
Katika hatua hii vivimbe vyenye seli za saratani huwa na ukubwa wa sm 2 na huanza kuenea na kuvamia matezi ya karibu (Lymph nodes)

Hatua ya 3
Katika hatua hii vivimbe vyenye seli za saratani huanza kukua tena na kufikia sm 5 na huenea kwenye matezi ya karibu (Lymph nodes) yaliyopo kwenye makwapa (maeneo ya mabega).

Hatua ya 4
Katika hatua hii seli za saratani huanza kuenea kutoka kwenye matezi yaliyopo kwenye makwapa (Lymph nodes) na kuelekea maeneo mengine ya mwili kama kwenye mifupa, mapafu, Ini, ubongo n.k.

>> Video zifuatazo zinaonyesha jinsi saratani ya matiti inavyokua tangu hatua za awali na kusambaa sehemu zingine za mwili




Video Credit: Covenant Health


UCHUNGUZI
Kama nilivyosema hapo awali kwamba mara uonapo dalili nilizozieleza hapo juu fika hospitali mara moja ili ufanyiwe uchunguzi. Uchunguzi huu hufanywa baada ya daktari wako kugundua dalili hatarishi za ugonjwa huu. Yafuatayo ni baadhi ya maelezo yanayohusu uchunguzi ambao daktari wako anaweza kuufanya;

1. Uchunguzi wa titi (Breast exam)
Daktari wako atachunguza vivimbe kwenye matiti (lumps) na dalili zingine

2. Kupiga X-ray (Mammogram)
Hii ni aina x-ray ambayo maranyingi hutumika kwa uchunguzi wa awali wa matiti, hutengeneza picha ya x-ray itakayosaidia kugundua vivimbe au hali yoyote tofauti kwenye titi.

3. Ultrasound
Kipimo hiki huweza kusaidia kutofautisha kati ya vivimbe na maji maji mengine yaliyotofauti kwenye titi.

4. MRI scan
MRI ni kifupi cha 'Magnetic resonance imaging', kipimo hiki hutumia mionzi maalumu kumpiga picha mgonjwa sehemu yoyote ya mwili au mwili mzima ili kugundua tatizo linalomsumbua. Kwa upande wa saratani ya matiti uchunguzi hufanyika ili kugundua ni kwa kiasi gani saratani imeenea mwilini mwako.


Picha: MRI Scanner

Picha: Mashine ya MRI Scanner, mwanamke akiandaliwa kufanyiwa uchunguzi

5. Biopsy
Kipimo hiki huhusisha oparesheni ya kuchukua sampuli ya tishu za titi kwa ajili ya uchunguzi wa maabara. Uchunguzi huu utaonyesha kama kuna seli za saratani au lah, kama kuna seli za saratani, je ni aina gani ya saratani? na je, aina hiyo ya saratani ina uhusiano wowote wa homoni za mwili?, majibu ya maswali haya yatamsaidia daktari kufanya maamuzi mengine.

NB:
Maelezo haya ya uchunguzi siyo muongozo, bali daktari wako ataamua nini cha kufanya kulingana na kiwango cha ugonjwa ulionao.

MATIBABU
Matibabu ya saratani ya matiti hufanywa kwa kutegemea mambo yafuatayo;

1. Aina ya saratani ya matiti
2. Hatua ya saratani ilipofikia (Stages)
3. Umri wa mgonjwa
4. Afya yake kwa ujumla
5. Uhusiano wa saratani hiyo na homoni za mgonjwa

Matibabu ya saratani ya matiti ni kama ifuatavyo;

1. Surgery (Upasuaji)
Kama kutakua na uhitaji wa upasuaji, upasuaji utafanyika kulingana na hali ya ugonjwa na maamuzi ya daktari kadiri atakavyoiona hali ya mgonjwa. Zifuatazo ni aina za upasuaji;

1.1. Lumpectomy
Upasuaji huu unahusisha kuondoa uvimbe wa saratani na kiasi kidogo cha tishu zenye afya kuzunguka uvimbe huo. Hii itasaidia kuepusha saratani hiyo kusambaa maeneo mengine ya mwili. Upasuaji huu hufanyika kama uvimbe huo wa saratani utakuwa ni mdogo na ambao ni rahisi kutenganisha na tishu zinazozunguka uvimbe huo.

1.2. Mastectomy
Upasuaji huu unahusisha kuondoa matezi ya maziwa (lobules) yenye saratani, mirija ya kupitisha maziwa (ducts) yenye saratani na baadhi ya ngozi zenye saratani.

1.3. Sentinel node biopsy
Upasuaji huu unahusisha kuondoa tezi moja (Lymph node), hii itasaidia kuzuia saratani hii kusambaa kwenye maeneo mengine ya mwili. Matezi haya (Lymph nodes) ndio sehemu ambazo ikifika saratani kutokea kwenye matiti husambazwa maeneo mengine ya mwili.

1.4. Axillary lymph node dissection
Upasuaji huu unahusisha kuondoa matezi kadhaa (Lymph nodes) yenye saratani yanayopatikana kwenye maeneo ya makwapa (armpit). Matezi haya ya kwenye makwapa ndio kitovu cha kusafirisha seli za saratani kwenye maeneo mengine ya mwili kama mifupa, ini, mapafu, ubongo n.k.

1.5. Reconstruction
Upasuaji huu hufanyika baada ya kufanya upasuaji kati ya mojawapo nilioeleza hapo juu. Hii ni hatua ya kurekebisha muonekano wa titi kama ikivyokua mwanzoni, au lifanane na muonekano wa titi jingine.


2. Radiation therapy (Tiba ya mionzi)
Hii ni tiba ya mionzi, mionzi hiyo huelekezwa kwenye titi sehemu yenye seli za saratani, mionzi hii huteketeza na kuharibu seli zote zenye saratani. Tiba hii ya mionzi inaweza kufanywa kwa mwanamke aliyefanyiwa upasuaji wa matiti ikiambatana na tiba ya kemikali (Chemotherapy). Hii itasaidia kuua seli zote za saratani zilizobakia.

3. Chemotherapy (Tiba ya kemikali)
Hii ni tiba ya kemikali (cytotoxic drugs) inayolenga kuua seli za saratani ili kuepusha kusambaa kwa saratani kwenda maeneo mengine ya mwili.

4. Hormone blocking therapy
Hii ni tiba ya homoni hususani kwa aina ya saratani yenye uhusiano na homoni za mwili (hormone sensitive breast cancers). Saratani hizi zenye uhusiano wa homoni zipo za aina mbili nazo ni Estrogen receptive (ER)-positive na Progesterone receptor (PR)-positive cancers.

Tiba hii ya homoni hudhibiti homoni zinazosababiaha saratani na mara nyingi hufanyika baada ya upasuaji pia inaweza ikafanywa kabla ya upasuaji, tiba hii husaidia kufanya vivimbe vya saratani kusinyaa.

Pia tiba hii huweza kuwa chaguo mahsusi kwa mgonjwa ambaye hawezi kufanyiwa upasuaji (surgery), tiba ya kemikali (chemotherapy) au tiba ya mionzi (radiotherapy), ila lazima aina hiyo ya saratani iwe yenye uhusiano homoni.

Mfano wa tiba hizi za homoni ni kama zifuatazo;

(a) Tamoxifen
(b) Aromatase inhibitors
(c) Ovarian ablation or suppression
(d) Luteinizing hormone-releasing hormone agonist drug inayoitwa 'Goserelin', ambayo huondosha mayai ya uzazi.

NB:
Tiba hii ya homoni huweza kuathiri uwezo wa mwanamke kupata ujauzito hapo baadae, kwa hiyo itumike pale ambapo njia zinginezo za matibabu zimeshindikana.

5. Biological treatment (Tiba ya kibaolojia)
Hizi ni dawa mahsusi zinazoua seli za saratani kwa aina mahsusi ya saratani, mfano wa hizo dawa ni kama; trastuzumab (Herceptin), lapatinib (Tykerb), na bevacizumab (Avastin). Daktari atatumia dawa hizi kulingana na namna atakavyoona inafaa.

NB:
Matibabu hayo niliyoyaeleza hapo juu, daktari wako ataamua kutumia aina yoyote ya matibabu kulingana na ukubwa wa tatizo la mgonjwa.

KUJIKINGA
Hakuna njia ya uhakika ya kujikinga na ugonjwa huu, lakini ukidhibiti baadhi ya mienendo ya maisha inaweza kupunguza atari ya wewe kupata saratani hii na aina nyimgine ya saratani. Zifuatazo ni baadhi ya njia za kujikinga na ugonjwa huu;

1. Epuka kunywa pombe kupita kiasi
2. Kula chakula kizuri chenye virutubisho kamili pamoja na matunda
3. Fanya mazoezi ya mwili
4. Kama umejifungua mtoto hakikisha unanyonyesha sana, usibanie maziwa. Kadiri unavyonyonyesha ndivyo unavyopunguza atari ya kupata saratani ya matiti. Katika jamii zetu kuna baadhi ya wanawake hawapendi kunyonyesha watoto wao, wanadai kwamba wakinyonyesha matiti yao yatalala, halafu watazeeka mapema. Haya ni mawazo potofu sana eti kufikiri "matiti yatalala, alafu atazeeka mapema", kadiri unavyoyabania maziwa ndivyo unavyoongeza atari ya kupata saratani ya matiti.

5. Jitahidi na Omba MUNGU upate ujauzito wa kwanza kabla ya miaka 30 au ikifikia miaka 30, kuchelewa kupata ujauzito baada ya miaka 30 na kuendelea kunaweza kukaongeza atari ya kupata saratani hii.


HITIMISHO
Saratani hii inavyoanza kwa hatua za awali, muhusika hawezi kuona dalili zozote, dalili zinaanza kuonekana baada ya vivimbe vya saratani kuanza kujitengeneza. Kama ilivyo kwa magonjwa yote ya saratani ikiwemo saratani ya matiti, kadiri unavyoigundua mapema ndivyo inavyokua rahisi kufanyiwa matibabu mapema na kupona kabisa. Ukichelewa kuigundua halafu ikaenea na kukomaa, inakua changamoto kufanyiwa matibabu, pia itaathiri maeneo mengine ya mwili kama ubongo, mapafu, ini, mifupa n.k. Cha msingi hapo ni kwamba mara uonapo dalili za ugonjwa huu kama nilizozieleza hapo juu, fika hospitali mara moja ukamuone daktari akufanyie uchunguzi.

MWISHO WA MAKALA HII


Kama una maoni au ushauri wowote kukusiana na makala hii basi usisite kutuachia maelezo yako hapo chini, Karibu sana!.

Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

Previous Post Next Post