Ufugaji wa Kuku wa kienyeji - Sehemu ya Tano (Indigenous Chicken Farming - Part Five)


SEHEMU YA TANO

6. NDUI YA KUKU (FOWL POX)
Ugonjwa husababishwa na virusi, huathiri ngozi ya kuku. Kuku wanakua na mabaka mabaka usoni hususani upanga wa juu na wa chini.

Ugonjwa huu umegawanyika makundi mawili; Hali ya ukavu (dry form) na Hali ya unyevu (Wet form). Hali ya ukavu huwa na muonekano wa vivimbe vigumu vidogovidogo kwenye maeneo ya mwili wa kuku yasiyo na manyoya kama Kichwa, miguu, sehemu ya hajakubwa n.k). Hali ya unyevu huwa na uwepo wa vidonda visivyopona maeneo ya mdomoni, koo la chakula na koo la hewa. Hali hii husababisha kuku kutopumua vizuri, Kuku wanaweza kupata mojawapo ya kundi la ugonjwa huu au yote makundi mawili.

Dalili za ugonjwa
  • Vivimbe vigumu vidogovidogo kwenye maeneo ya mwili wa kuku yasiyo na manyoya kama Kichwa, miguu, sehemu ya hajakubwa n.k).
  • Kuku kupumua kwa taabu.




Namna Ugonjwa unavyosambazwa
  • Ugonjwa huu husambazwa kwa kugusana moja kwa moja kati ya kuku mgonjwa na kuku asiyeumwa au kupitia Mbu. Pia ukurutu uliotoka kwa kuku mgonjwa huwa ni mojawapo ya chanzo cha kusambaza ugonjwa.
  • Virusi wa ugonjwa huu huingia kwenye mishipa ya damu ya kuku kupitia Macho, Ngozi, vidonda, au kupitia koo la hewa. Mbu wanabeba virusi hivi baada ya kufyonza damu ya kuku mwenye ugonjwa huu. Ushahidi wa kisayansi unasema kwamba Mbu aliyebeba virusi hivi huathirika kwa maisha yake yote. Mbu ndio wasambazaji wa kwanza wa ugonjwa huu. Mbu wa aina nyingi husambaza ugonjwa huu mara nyingi wakati wa kipindi cha baridi.

Namna ya kudhibiti
  • Ugonjwa huu hauna tiba, hivyo unazuiwa kwa chanjo. Ugonjwa huu unasambaa polepole kwahiyo ukipiga chanjo unazuia maambukizi haraka sana. Chanjo hii inawekwa kwenye mabawa ya kuku kwa sindano.
  • Pia unaweza kudhibiti ugonjwa huu kwa kuua na kuangamiza mazalia ya Mbu. Ingawaje kama ugonjwa umesambaa kwa kiasi kikubwa ni muhimu kupiga chanjo.
  • Weka maji ya kuosha viatu (Footbath), ili kuzuia vimelea vya nje kuingizwa ndani ya banda.
  • Punguza idadi ya watu wanaotembelea bandani
  • Kila unapotembelea bandani au kufanya kazi, hakikisha unaanzia kwenye kuku wadogo au vifaranga halafu unamalizia kwenye kuku wakubwa. Hii itasaidia kupunguza vimelea vya magonjwa kusambaa kutoka kwa kuku wakubwa kwenda kwa wadogo.
  • Safisha vifaa vyote bandani kwa kutumia kemikali (Disinfectants) ya kuzuia ukuaji wa vimelea.
  • Kitu cha msingi kwa ugonjwa huu ni kwamba Usiwape chanjo kuku wako kama ugonjwa haujaingia kwenye eneo lako au kwenye banda lako, kwa hiyo hakikisha unapiga chanjo baada ya ugonjwa kuingia.

7. MAHEPE (MAREK'S DISEASE)
Majina mengine ya ugonjwa huu ni kama Acute leukosis, Neural leukosis, Range paralysis na Gray eye (Kama macho yameathirika).
Ugonjwa huu hufanana na ugonjwa unaoitwa Lymphoid Leukosis, lakini tofauti ni kwamba; Ugonjwa wa Marek's hutokea kwa kuku wenye umri wa wiki 12 hadi 25, wakati ugonjwa wa Leukosis huwapata kuku wakiwa na umri wa wiki 16.

Ugonjwa wa Marek's ni aina ya Kansa ya ndege (Kuku), Husababishwa na virusi wanaoleta uvimbe ndani ya mishipa ya neva za fahamu, hatimae kuku wanapalalaizi viungo na kulemaa. Vilevile uvimbe hutokea kwenye macho na kusababisha mboni za jicho kubadilika hatimae macho kupofuka.

Uvimbe uliopo kwenye viungo mbalimbali vya mwili kama Ini, Figo, Nyongo, Kongosho, Mapafu, Misuli, Ngozi na viungo vingine, husababisha mwili wa kuku kutofanya kazi vizuri na kudhoofu. Kwa hali hiyo kuku wenye ugonjwa huu huwa na dalili zifuatazo;

Dalili za ugonjwa
  • Kupumua kwa shida
  • Sehemu za nyama zilizoshika manyoya huvimba
  • Wanaharisha kinyesi cha kijani
  • Hali ikiwa mbaya sana, kuku wanadhoofu na kukonda sana pia upanga wa juu na chini wa kichwa hupauka na kuwa na magamba.
  • Wanapalalaizi viungo hususani miguu
  • Mboni ya macho hubadilika isivyokawaida hatimae kuku hushindwa kuona kabisa







Namna Ugonjwa Unavyosambazwa
Ugonjwa huu husambazwa kwa njia ya hewa ndani ya banda. Virusi wa ugonjwa huu hutoka kwa kuku wagonjwa kutoka kwenye manyoya ya kuku yaliyonyofoka, vumbi ndani ya banda, kinyesi na Mate au majimaji ya kuku. Kuku walioathirika hubeba virusi ndani ya damu kwa maisha yao yote na ndio chanzo cha kuambukiza kuku wengine wenye afya.

Namna ya kudhibiti
  • Ugonjwa huu hauna tiba, kwa hiyo kinachotakiwa ni kuwapatia kuku wako chanjo. Chanjo ya Ugonjwa huu inazuia utengenezaji wa uvimbe (Kansa) kwenye viungo mbalimbali vya mwili wa kuku.

8. MATATIZO YA MFUMO WA UPUMUAJI (INFECTIOUS BRONCHITIS)
Majina mengine ya ugonjwa huu ni pamoja na IB, Brionchitis, cold. Ugonjwa huu husababishwa na virusi ambavyo huathiri mfumo wa upumuaji wa kuku. Athari za ugonjwa huu hutegemeana na umri na kinga ya kuku aliyonayo, mazingira ya kuku na uwepo wa magonjwa mengine ya kuku.

Pia ugonjwa huu huathiri tishu mbalimbali za mwili ikiwemo mfumo wa uzazi wa kuku jike (Reproductive tract). Zifuatazo ni dalili za ugonjwa huu;

Dalili za Ugonjwa
  • Kuku wanakosa hamu ya kula na kunywa maji
  • Kuku wanalia kwa sauti kali, hutokwa machozi machoni na puani. Kuku wadogo hupumua kwa shida kwa kukoroma.
  • Kuku wanapumua kwa kukoroma wakati wa Usiku.
  • Uzalishaji wa mayai hupungua kadiri siku zinavyokwenda, unaweza ukaona uzalishaji wa mayai ukaongezeka baada ya wiki 5 au 6 lakini kwa kiwango kidogo sana.
  • Gamba la yai huwa rafu na majimaji ya yai huwa maji kabisa.
Picha: Kuku akikoroma na kupumua kwa shida, mdomo upo wazi anajaribu kuvuta hewa kwa mdomo

 Picha: Magamba ya mayai yapo rafu

Picha: Magamba ya mayai yapo rafu na baadhi hupasuka

Namna ugonjwa unavyosambazwa
Ugonjwa huu husambazwa kwa njia ya hewa, mifuko ya chakula, mizoga ya kuku iliyokwisha kufa kwa ugonjwa huu, banda la kuku lenye virusi vya ugonjwa huu na panya. Virusi vya ugonjwa huu hupenyeza kwenye mayai yaliyotagwa, Uzuri ni kwamba kiini cha yai hilo hufa na yai hushindwa kuanguliwa.

Namna ya kudhibiti
Ugonjwa huu hauna tiba, bali unakingwa kwa chanjo. Dawa za Antibayotiki kwa siku 3 hadi 5 zinaweza kupunguza kasi ya ugonjwa huu kwa kutibu magonjwa nyemerezi yanayosababishwa na bacteria. Dawa hizo za Antibayotiki hazitibu ugonjwa huu bali zinapunguza kasi ya ugonjwa.

<<< BOFYA HAPA KUSOMA SEHEMU YA NNE<<<


Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

Previous Post Next Post