Ufugaji wa Kuku wa kienyeji - Sehemu ya Nne (Indigenous Chicken Farming - Part Four)


SEHEMU YA NNE

3. KIDELI/MDONDO (NEW CASTLE DISEASE)
Ugonjwa huu husababishwa na virusi ambavyo huathiri mfumo wa upumuaji na neva za fahamu. Vifo vya vifaranga na kuku wakubwa huanzia asilimia 0 hadi 100%, itategemeana na kasi ya mashambulizi ya virusi hao.

Dalili za Ugonjwa
  • Uzalishaji wa mayai hupungua kwa kasi kubwa hadi kufikia sifuri (0) ndani ya siku nne.
  • Kuku wanapalalaizi shingo na kupinda
  • Kuku wanakohoa na kupumua kwa shida na wakati mwingine hutokwa na majimaji puani.
  • Kuku wanaharisha muharo wa majimaji wenye rangi ya kijani mpauko.
  • Kuku wakianza kutaga tena, mayai yao huwa na sura isiyokua ya kawaida au sura iliyopindapinda.
  • Kuku wanakohoa na kupiga chafya
  • Kuku wanakaa wakiwa wamenyong'onyea viungo vya miguu na mara nyingine wanatembea kinyumenyume.
  • Kuku wanatembea kwa kuzunguka mduara au wanainamisha vichwa vyao katikati ya miguu.
  • Kuku wanakosa hamu ya kula, hali ikiwa mbaya sana wanakaa chini na kupoteza fahamu na baadae hufa.
TAZAMA VIDEO HAPO CHINI KUONA DALILI ZA UGONJWA HUU

Video kwa Hisani ya (Video credit): www.fieldcasestudy.com

Picha: Kuku mwenye kideli aliyepalalaizi shingo

Namna Ugonjwa unavyosambazwa
  • Ugonjwa huu husambazwa kwa njia ya hewa, maji maji ya kuku kama udenda au kinyesi. Pia husambazwa kupitia vifaa mbalimbali vilivyochafuliwa na majimaji yaliyotoka kwa kuku kama udenda au kinyesi.
  • Pia Virusi vya kideli husambazwa kupitia mayai yaliyotagwa na kuku muathirika wa ugonjwa huu, Uzuri ni kwamba kiini cha yai lenye vimelea vya kideli hufa na yai kushindwa kuanguliwa.
Namna ya kudhibiti
  • Ugonjwa huu hauna tiba, bali hukingwa kwa chanjo.
  • Wapatie chanjo ya kideli kuku wako wenye umri wa wiki 3 hadi 4, pia rudia tena chanjo wakiwa na umri wa wiki 16 na wakifikia wiki 24. Baada ya hapo uwapatie tena chanjo mara uonapo kuna mlipuko wa ugonjwa kwenye eneo lako.
4. HOMA YA MATUMBO (FOWL TYPHOID)
Ugonjwa huu husababishwa na vimelea vinavyoitwa gallinarum au shigella gallinarum. Dalili za ugonjwa huonekana siku 3 hadi 4 baada kuku kuingiliwa na vimelea, pia vifo huonekana ndani ya wiki 2 tangu kuona dalili. Ugonjwa huu husambazwa kupitia kuku walioathilika, vifaa mbalimbali ikiwemo vya kuku, viatu, unyevu unyevu ndani ya banda (hususani kwenye sakafu ya banda kama mapumba ya mpunga au malanda ya mbao), n.k

Dalili za Ugonjwa
  • Kuku wanazubaa na manyoya yao yanakua hovyo hovyo tofauti na kuku wasiougua.
  • Kichwa chake hupauka, na upanga wa kichwani hulegea na kulala
  • Wanakosa hamu ya kula
  • Wanaharisha kinyesi cha rangi ya chungwa
Namna ya kudhibiti
  • Wape chanjo ya ugonjwa huu kwa kuku wenye umri wa wiki saba (7)
  • Teketeza kuku wote waliokufa kwa kuchoma moto
  • Usiruhusu watu mbali mbali kutembelea mazingira ya banda lako bila kuondosha vimelea (Disinfection) kwa kukanyaga sehemu yenye maji ya dawa (Footbath) kila wanapoingia au wanapotoka bandani.
  • Tumia dawa za oxytetracycline kama Furamax,Typhoprim hutibu ugonjwa huu.
5. PULLURUM DISEASE (MUHARO MWEUPE)
Ugonjwa huu husababishwa na vimelea vinavyoitwa Salmonella Pullurum, vimelea hivi huathiri mfuko wa mayai wa kuku jike (Ovary). Vimelea hivi pia hukaa kwenye utumbo mwembamba wa kuku. Ugonjwa huu husambaa kwa kupitia mayai yaliyotagwa na kuku aliyeathirika na ugonjwa huu pia vifaranga walioanguliwa kutokana na mayai hayo huwa na vimelea vya ugonjwa huu.

Dalili za Ugonjwa
  • Vifaranga wanalia kwa kutoa sauti kali
  • Manyoya yanavurugika
  • Sehemu ya hajakubwa ya vifaranga hulowana kinyesi
  • Kuku wakubwa hawaonyeshi dalili zozote.
  • Kwa vifaranga dalili huonekana kuanzia siku 4 hadi 10, na vifo hutokea baada ya wiki 3 tangu kuanza ugonjwa.
  • Kuku wanaharisha muharo mweupe.

Namna ya kudhibiti
  • Teketeza Kuku wote wenye ugonjwa huu
  • Safisha vifaa vyote bandani kwa kutumia kemikali (Disinfectant) itakayoua vimelea wa magonjwa, pia safisha vifaa vya kuangulia mayai (Incubators).
  • Nunua kuku au vifaranga wasiokua na magonjwa kutoka kwa wauzaji wanaodhibiti vizuri magonjwa ya kuku.
<<< BOFYA HAPA KUSOMA SEHEMU YA TATU<<<


Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

Previous Post Next Post