Ufugaji wa Kuku wa Mayai - Sehemu ya Pili (Layer Poultry Farming - Part Two)



SEHEMU YA PILI

CHANJO NA UMUHIMU WAKE
Utaratibu wa Chanjo kwa vifaranga ni Lazima, ili kuwafanya vifaranga wasikumbwe na magonjwa ya aina zote. Faida kubwa za chanjo kwa Kuku ni kama ifuatavyo;
  • Kuchanja kuku kwa wakati husaidia mwili wa kuku kuwa na uwezo mkubwa wa kuzuia magonjwa.
  • Kama ugonjwa umeingia, Idadi ya kuku watakaoathirika huwa ndogo sana
  • Kuku watakao kufa kwa ajili ya ugonjwa huwa ni ndogo.
Kuna Chanjo za aina nyingi zinazotumiwa na kuku wa mayai kama Marex, Ranikheth, Gumboro, Bruchaities, Bosonto, Salmonela n.k.

ANGALIZO KABLA YA KUTOA CHANJO
Utoaji wa chanjo una taratibu zake, Inakupasa kuzifwata kwa uangalifu taratibu hizo. Taratibu hizo ni kama ifuatavyo;
  • Wakati wa kutoa chanjo washike kuku wako vizuri
  • Wachanje kuku wako pasipo kutumia nguvu nyingi, washike taratibu.
  • Usiwape chanjo kuku waliougua, wapatie kuku wenye afya tu.
  • Fanya chanjo wakati wa hali ya hewa ya baridi (Cold weather condition)
  • Baada ya kumaliza kufanya chanjo, osha vifaa vyako vyote na Maji ya moto au dawa za kutibu vifaa kutokana na vimelea vya magonjwa (germicide medicine/antiseptic)

KUTOA CHANJO
Utaratibu wa chanjo unatakiwa uwe kama ifuayavyo kulingana na Umri wa kuku;
1. Chanjo ya Kideli (New Castle Disease): Umri wa siku 7(wiki 1)
2. Chanjo ya Gumboro: Umri wa siku 14 (wiki 2)
3. Chanjo ya Fowl typhoid: Umri wa wiki 9
4. Chanjo ya Fowl pox: Umri wa wiki 18
5. Wiki ya 19 wapatie dawa ya minyoo, inakua ni wiki moja kabla hawajaanza kutaga (Wanaanza kutaga wakifikia umri wa wiki 20), baada ya hapo endelea kuwapa dawa za minyoo kila baada ya miezi sita.

MAGONJWA MBALIMBALI YA KUKU WA MAYAI NA NAMNA YA KUWADHIBITI
Yafuatayo ni baadhi ya magonjwa ya kuku wa mayai na kuku aina nyingine kama kuku wa nyama na wengineo;

1. TRUSH
Huu ni ugonjwa wa fangasi, husababishwa na fangasi aina ya yeast  (Candida albicans). Huenezwa pale kuku wanapokula vyakula vilivyoota ukungu, pia husambazwa zaidi pale wanapokunywa maji yaliyochafuliwa na fangasi.

Dalili za Ugonjwa
  • Kuku wanazubaa na wanatulia sehemu moja pia wanakua na utando au vitu vigumugumu (Crusty) sehemu ya hajakubwa.
  • Manyoya ya kuku yanakua rafu.
  • Utaona majimaji mazito meupe ndani ya kifuko cha chakula cha kuku (Crop), Kifuko cha chakula cha kuku, kwa wale waliofuga kuku au kwa wale waliowahi kuchinja kuku, kifuko hicho cha chakula kipo katikati ya shingo na mwili wa kuku (sehemu ya kifua). Kifuko hiki cha chakula huonekana vizuri sana kama kuku ameshiba, huwa panavimba, sehemu hii huhifadhi chakula kabla ya kwenda kumeng'enywa.
  • Kuku wanapata hamu ya kula sana isivyo kawaida.
Photo Credit: www.chickenheavenonearth.com

Photo Credit: www.morningchores.com

Namna ya kuzuia na Matibabu
Ugonjwa huu hauna chanjo, ila una tiba, Tibu kuku wako kwa kutumia dawa zinazoua vimelea vya Fangasi (Anti-fungal medicine) zinazopatikana kwenye maduka ya dawa za mifugo. Ili kuzuia ugonjwa huu hakikisha unaondoa vyakula vichafu na kuwapatia vyakula safi. Kumbuka kuosha vyombo vya chakula na maji kila wakati.

2. AIR SAC DISEASE
Ugonjwa huu huathiri mfumo wa upumuaji wa kuku, husababishwa na kimelea kinachoitwa Mycoplasma gallisepticum.

Dalili za Ugonjwa
  • Kuku wanakua dhaifu na wanapunguza kutaga
  • Siku zinavyozidi kwenda, kuku wanakohoa, wanapiga chafya, wanapumua kwa shida, wanavimba sehemu za maungio ya ya miguu au mabawa (swollen joints) na baadae wanakufa.
Photo Credit: www.poultrykeeper.com

Namna Unavyoenezwa
  • Unaambukizwa baina ya kuku kupitia hewa au majimaji aliyotoa kuku kama kamasi n.k.
  • Pia huambukizwa kutoka kwa ndege wa porini.
  • Pia huambukizwa kutoka kwa Mama kuku kwenda kwa Kifaranga kupitia yai.
Namna ya kuzuia na Kutibu
Ugonjwa huu una chanjo na tiba, Tibu kuku wako kwa kutumia dawa zinazoua au zinazozuia ukuaji na kuzaliana kwa bakteria (Antibiotics) zinazopatikana kwenye maduka ya dawa za mifugo.

NB:
Kutokana na kwamba ugonjwa huu huambukizwa baina kuku na kuku, yakupasa uwe makini sana na mchunguzi, chunguza dalili hizo za kuku kwa makini, ili mara unapogundua ugonjwa huo uutibu haraka na kwa ufanisi zaidi.

<<< SEHEMU YA KWANZA


Makala na: Lusubilo Mwaijengo

Post a Comment

Previous Post Next Post