Kilimo bora cha Mihogo - Sehemu ya Tano (Growing Cassava - Part Five)


SEHEMU YA TANO

B: MAGONJWA

1. African Cassava Mosaic Disease (ACMD)
Ni miongoni mwa magonjwa yanayosumbua sana zao la muhogo, ugonjwa huu umesambaa sana maeneo mengi yanayolimwa muhogo barani Afrika na husababisha upotevu wa mavuno kwa asilimia 90%. Ugonjwa huu husambazwa na vipande vya kupandia vyenye ugonjwa na wadudu wanaoitwa Whiteflies (Bemisia tabaci).

Photo Credit: © Lett, J.M., Cirad
Picha: Mmea wa muhogo uliathiriwa na ugonjwa huu

Photo Credit: www.infonet-biovision.org   shared under Creative common license

Athari
  • Majani huwa na michilizi iliyojichora (mosaic patterns) ambayo huathiri majani na mmea kwa ujumla. Pia hali hii hoonekana katika hatua za awali za ukuaji wa jani.
  • Dalili za ugonjwa huu hutofautiana baina ya jani hadi jani, shina hadi shina na mmea hadi mmea.
  • Baadhi ya majani yaliyopo katikati ya majani mengine yaliyoathirika huonekana ni mazima na muonekano wa kupona.

Namna ya kudhibiti
  • Tumia vipande vya mashina vya kupandia visivyokua na magonjwa. Kama itashindikana kupata vipande hivyo visivyokua na magonjwa chagua mashina ya kwenye matawi, usitumie shina kuu (main stems). Utafiti umeonyesha kwamba vipande vya kupandia vinavyotokana na matawi hutoa mmea usiokua na ugonjwa huu tofauti na kutumia vipande vya shina kuu.
  • Waangamize wadudu aina ya 'Vidukari Mafuta' (Whiteflies) wanaosambaza ugonjwa huu kwa kutumia dawa mbalimbali za asili au za kemikali zinazopatikana kwenye maduka ya pembejeo za kilimo.
  • Panda aina ya muhogo inayovumilia athari za ugonjwa huu.

2. Cassava bacterial blight (Xanthomonas campestris pv. manihotis)
Huu nao ni miongoni mwa ugonjwa unaorudisha nyuma uzalishaji wa zao la muhogo. Ugonjwa huu husababishwa na bacteria.

Picha: Ugonjwa wa 'Cassava Bacterial bright'       Photo Credit: www.agrihomegh.com

Namna unavyosambazwa
  • Ugonjwa huu husambazwa kwa vipande vya mashina vya kupandia vilivyoathirika.
  • Vilevile husambazwa kwa matone ya mvua, wadudu wanaotafuna majani kama Panzi, Vifaa vinavyotumika shambani kama visu, nyembe n.k. pamoja na Wanyama wanaotembea shambani hususani wakati mvua ikinyesha au mara tu baada ya mvua kunyesha.
Athari
  • Majani yaliyoathiriwa huwa na mabaka mabaka ya mviringo na vijieneo vyenye ubichi kama kulowana (water-soaked areas).
  • Athari ikizidi mmea hupukutisha majani sana, hali inayopelekea mmea kubaki bila majani. Hali hii husababisha mashina na mizizi kuwa na rangi ya kahawia.
  • Kipindi cha unyevu hewa mwingi (Humidity) kunakua na kama vivimbe (Bacterial exudation) vilivyotokeza chini ya majani na mashina.
  • Ugonjwa huu husababisha upotevu wa mavuno kuanzia asilimia 20% hadi 100% itategemeana na aina ya muhogo, aina ya bakteria na hali ya hewa.

Namna ya kudhibiti
  • Tumia vipande vya mashina vya kupandia vilivyo visafi. Hii itasaidia kupunguza  kuzuka kwa ugonjwa huu kipindi ambapo ugonjwa huu umesambaa.
  • Kama ugonjwa huu umezuka kwa kiasi kikubwa chagua vipande vya kupandia kutoka kwenye mmea wenye afya hususani sehemu ya shina iliyokomaa. Sehemu hiyo ya shina iliyokomaa huwa ni urefu wa mita 1 kutoka usawa wa ardhi.
  • Vitibu vifaa vyako vya shamba kama visu, mara kwa mara kwa kutumia dawa ya kuua bakteria. Hii itasaidia kupuguza uenezwaji wa ugonjwa huu.
  • Panda zao la muhogo pamoja na mazao mengine kama Mahindi au matikiti, Imeripotiwa kwamba kupanda muhogo pamoja na mazao ya mahindi au matikiti husaidia kupunguza kasi ya ugonjwa huu kwa kiasi kikubwa.
  • Badirisha mazao pamoja na kupumzisha shamba.
  • Ondoa na choma masalia yote ya muhogo yenye magonjwa.

3. Brown leaf spot (Cercosporidium henningsii)
Ugonjwa huu husababishwa na kimelea jamii ya Fangasi/Kuvu kinachoitwa Cercosporidium henningsii au Cercospora henningsii, vilevile huitwa Mycospaerella henningsii.

Ugonjwa huu huyakumba majani ya chini yaliyozeeka na hali hii huonekana miezi 5 hadi 6 baada ya kupanda, majani hupukutika au kudondoka kabla ya muda wake.

Picha: Ugonjwa wa Bacterial leaf spot     Photo Credit: www.pestnet.org


Athari
  • Majani yaliyozeeka huwa na madoa ya mviringo yenye rangi ya kahawia, chini ya majani hayo huwa na rangi ya kahawia iliyochangamana na rangi ya kijivu.
  • Majani yaliyoathirika baadae hubadirika na kuwa rangi ya njano na hatimae hudondoka.
  • Kwenye maeneo yenye majimaji au unyevu mwingi, ugonjwa huu huongeza kasi na kusababisha upotevu wa mavuno hadi asilimia 20%.
NB:
Hali ya joto na yenye unyevu mwingi huongeza kasi ya ugonjwa. Vimelea vya ugonjwa huu husambazwa kwa upepo au michapo ya matone ya maji (Water splash). Pia vimelea hivi huenea na kufika umbali mrefu endapo vitabebwa kwenye vipande vya kupandia. Kwa ujumla majani yaliyozeeka huathirika sana na ugonjwa huu. Vimelea vya ugonjwa huu huendelea kuishi kwenye majani yaliyodondoka.

Namna ya kudhibiti
  • Panda kwa nafasi ya kutosha ili kuruhusu hewa kupenyeza shambani.
  • Badirisha mazao
  • Panda mapema mara tu mvua zinapoanza kunyesha ili mmea ufikie miezi 6 hadi 8 wakati wa kiangazi.
  • Wakati wa kiangazi yaondoe majani yote yenye ugonjwa ili kuzuia kusambaa kwa ugonjwa wakati mvua zimeanza.
  • Ukishavuna mihogo yako, kusanya na uchome moto masalia yote.


Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

Previous Post Next Post