Ufahamu ugonjwa wa Homa ya Ini - Sehemu ya Kwanza (Uderstanding Hepatitis disease - Part One)


SEHEMU YA KWANZA

Homa ya ini kama inavyojulikana kwa lugha ya kimombo kwa jina la 'Hepatitis', ni ugonjwa unaoathiri ini, ini huaribika na kubadirika muonekano wake na kusinyaa, pia huwa na vivimbe ambavyo hutokea baada ya mishipa ya damu kwenye ini kuharibika na kutengeneza usaa au uozo. Ugonjwa huu husababishwa na virusi pamoja na  mambo mengine ikiwemo sumu mbalimbali ziingiazo mwilini kupitia mfumo wa chakula kama Pombe na baadhi ya madawa. Pia ugonjwa unaoitwa 'Autoimmune disease' huweza kusababisha ugonjwa wa homa ya ini, ugonjwa wa 'Autoimmune disease' hutokea wakati kinga ya mwili huanza kuvamia seli hai za mwili, halii hii husababisha madhara mbalimbali mwilini ikiwemo homa ya ini.

Ini lako lipo mkono wa kulia kwako sehemu ya juu ya tumbo, Ini linafanya kazi kubwa sana inayosaidia mwili ufanye kazi vizuri. Zifuatazo ni kazi muhimu za ini kwa afya ya binadamu;
  • Kutengeneza nyongo ambayo ni muhimu wakati wa mmeng'enyo wa chakula.
  • Kuchuja au kuharibu sumu mwilini.
  • Kuondosha mwilini seli hai nyekundu zililizovunjika (bilirubin), seli hizi nyekundu zilizovunjika zikizidi mwilini husababisha ngozi, macho na mkojo kuwa na rangi ya njano pamoja na kinyesi kuwa na rangi mpauko (jaundice).
  • Kupunguza mafuta na homoni mbalimbali mwilini.
  • Kuvunjavunja wanga, mafuta na protini mwilini
  • Kuongeza kasi ya utendaji kazi wa vichocheo vya mwili (enzymes), ambavyo hufanya kazi mbalimbali muhimu za mwili.
  • Kuhifazi aina ya sukali maalumu inayoitwa Glycogen
  • Kuhifadhi madini na vitamini mbalimbali kama A, D, E, na K.
  • Kutengeneza protini za kwenye damu kama 'albumin'
  • Kutengeneza visababishi vya damu kuganda (Clotting factors).
Picha: Mfumo wa chakula wa binadamu ukionyesha viungo mbalimbali ikiwemo Ini

NB:
Hizo ni baadhi ya kazi muhimu za Ini, kwa hiyo ini lako likiharibiwa na ugonjwa huu husababisha madhara makubwa mwilini ikiwemo kifo.


VISABABISHI VYA HOMA YA INI
Kama nilivyokwisha kueleza hapo awali kwamba ugonjwa huu husababishwa na virusi (Hepatitis viruses) pamoja na mambo mengine kama matumizi ya pombe na sumu mbalimali (non-infectious hepatitis). Ufuatao ni mchanganuo wa vidababishi hivi pamoja na namna unavyoenezwa;

A: VIRUSI VYA HOMA YA INI (HEPATITIS VIRUSES/INFECTIOUS HEPATITIS)
Virusi wa homa ya ini wamegawanyika katika makundi au aina tano ambayo ni A, B, C, D na E. Aina zote hizi tano za virusi hawa husababisha vifo endapo mgonjwa asipopatiwa matibabu mapema. Aina ya A na E husambazwa na chakula au maji yaliyochafuliwa na vimelea hivi, aina ya B, C na D husambazwa na mgusano wa majimaji ya mwilini kama damu na majimaji ya uzazi. Ufuatao ni mchanganuo wa kina kuhusiana na aina tano za virusi hawa;

1. Hepatitis A virus (HAV)
Virusi hawa hupatikana kwenye kinyesi cha mgonjwa wa homa ya ini, na husambazwa kwa kula chakula au maji yaliyochafuliwa na uchafu wenye virusi hawa. Athari ya virusi hawa huwa ni ndogo, mgonjwa hupona haraka tofauti na virusi wengine. Virusi hawa husambaa sana kwenye maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu na yenye uchafu mwingi. Virusi hawa husababisa homa ya ini aina ya A (Hepatitis A).

2. Hepatitis B virus (HBV)
Virusi hawa husambazwa kupitia damu, majimaji ya uzazi (manii) na majimaji mengine ya mwili. Virusi hawa husababisha homa ya ini aina ya B (Hepatitis B). Yafwatayo ni mambo yanayoweza kusambaza virusi hawa;
  • Kwa njia ya ngono
  • Pia virusi hawa huweza kusambazwa kutoka kwa mama mjamzito kwenda kwa mtoto hususani wakati wa kujifungua
  • Pia virusi hawa huweza kusambazwa wakati wa kubadilisha au kuongeza damu endapo mgonjwa atapewa damu yenye virusi hawa.
  • Kuchangia matumizi ya vitu vyenye ncha kali kama nyembe, sindano, visu n.k kwa watu wengi, mfano kwa wale mateja wanaojidunda sindano za madawa ya kulevya huchangia sindano moja kwa watu wengi, hali inayopelekea hatari ya kupata ugonjwa huu.
  • Wahudumu wa afya wapo hatarini kupata ugonjwa huu pale wanapowahudumia wagonjwa wenye virusi hivi hususani wanapochukua sampuli za damu zao kwa kutumia sindano.

3. Hepatitis C virus (HCV)
Virusi hawa husambazwa kupitia damu, namna unavyosambazwa hufanana na virusi aina ya B (Hepatitis B virus) kama; kupitia ngono, mgonjwa kuongezewa damu yenye virusi hivi, matumizi ya sindano zilizotumika n.k. Virusi hawa husababisha homa ya ini aina ya C (Hepatitis C).

4. Hepatitis D virus (HDV)
Virusi hawa hutegemea uwepo wa virusi aina ya B kuzaliana, hii ina maana kwamba mgonjwa mwenye virusi aina ya B ana hatari ya kupata virusi aina ya D, hali inayopelekea ugonjwa kuwa mkubwa zaidi. Virusi hawa aina ya D husambazwa kupitia damu, hivyo njia mbalimali za kusambazwa hufanana na zile za virusi aina ya B na C. Kwa hiyo mtu akipata chanjo ya Hepatitis B atakua pia amejikinga na virusi wa Hepatitis D. Virusi hawa husababisha homa ya ini aina ya D (Hepatitis D).

5. Hepatitis E virus (HEV)
Virusi hawa husambazwa kupitia kula chakula au maji yaliyochafuliwa na uchafu wenye virusi hivi, kwa hiyo maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu na yenye uchafu mwingi huongeza kasi ya kusambaa ugonjwa huu kama ilivyo kwa virusi aina ya A (Hepatitis B virus). Uchafu huo hutokana na kinyesi cha mgonjwa mwenye virusi hivi, vinyesi hivi huweza kusambaa kwenye maji, chakula na vyombo kama kanuni za usafi hazitazingatiwa vyema. Virusi hawa husababisha homa ya ini aina ya E (Hepatitis E).


B: VISABABISHI VINGINE VYA HOMA YA INI (NON-INFECTIOUS HEPATITIS)
Kama nilivyoeleza hapo awali kwamba mbali na virusi mbalimbali kusababisha ugonjwa huu, kuna mambo mengine yasiyo ya kuambukiza ambayo pia husababisha ugonjwa wa homa ya ini. Ufuatao ni mchanganuo wa visababishi hivyo;

1. Matumizi ya pombe kuzidi kiasi
Kazi kubwa ya ini ni kuvunjavunja sumu zitokanazo na chakula, au kitu chochote kilichoingia mwilini kupitia mfumo wa chakula lazima kichujwe sumu na ini. Hivyo basi matumizi ya pombe kupita kiasi husababisha ini kuharibika na kushindwa kufanya kazi kwa sababu kilevi (Alcohol) kilichopo kwenye pombe huharibu seli za ini hatimae baada ya muda kupita husababisha ini kuharibika moja kwa moja.

2. Sumu
Sumu za aina mbalimbali zitokanazo na matumizi ya madawa ya tiba kupita kiasi na kuwa mazingira hatarishi yenye sumu husababisha ugonjwa huu.

3. Autoimmune disease
Hii ni hali inayotokea mwilini pale kinga ya mwili inapoanza kuvamia seli za mwili, hivyo kinga ya mwili hufikiri kana kwamba ini ni kitu cha hatari mwilini na huanza kulivamia ini kwa kuua seli zake. Hali hii husababisha ini kuanza kudhoofika taratibu mpaka litaharibika kabisa na kushindwa kufanya kazi. Kufahamu zaidi kuhusu 'Autoimmune disease' BOFYA HAPA.


DALILI ZA HOMA YA INI
Kwa baati mbaya ugonjwa wa homa ya ini hauna dalili za awali, mtu mwenye ugonjwa haonyeshi dalili kabisa anakuwa mwenye afya njema tu. Dalili zinaanza kuonekana pale ugonjwa unapokomaa wakati ini limeharibika kabisa. Virusi aina ya A na E hawana shida sana, na athari yake ni ndogo pia mgonjwa anaweza kupona bila matibabu yoyote. Kirusi aina ya D hutegemea kirusi cha B kuzaliana, hivyo ukipata chanjo ya kirusi aina ya B basi umezuia kirusi cha D. Kwa hiyo virusi hatari ni aina ya B na C, Zifuatazo ni dalili za ugonjwa wa homa ya ini, dalili hizi honekana baada ya ini kuharibika na kushindwa kufanya kazi;

1. Kukojoa mkojo wenye rangi nyeusi kama chai ya rangi
2. Kutoa kinyesi chenye rangi mpauko
3. Rangi ya ngozi hubadirika na kuwa ya njano
4. Macho huwa ya njano (sehemu nyeupe kwenye macho ndio hubadirika na kuwa njano)
5. Maumivu ya tumbo
6. Mafua makali
7. Kukosa hamu ya kula
8. Kupungua sana uzito kwa muda mfupi
9. Kuchoka sana na kuishiwa nguvu pasipo kufanya kazi yoyote.

NB:
Dalili hizi huonekana mwishoni kwa sababu virusi vya ugonjwa huu hujitengeneza taratibu pasipo muhusika kujua. Jambo la msingi hapa ni kwamba mtu yoyote mwenye afya njema anapaswa kwenda hospitali kupima kama ana virusi vya ugonjwa huu au lah, hii itakusaidia kupatiwa chanjo ya ugonjwa huu mapema hususani kwa kirusi aina ya B. Pia kama unadalili zinazofanana na nilizoziorozesha hapo juu basi unatakiwa uende hospitali mara moja ukafanyiwe uchunguzi zaidi.


UCHUNGUZI WA UGONJWA
Mara uonapo dalili zozote zinazofanana na hizo nilizoziorozesha hapo juu, fika haraka hospitali kwa uchunguzi zaidi. Daktari wako anaweza akafanya yafuatayo;

1. Kuchukua historia ya ugonjwa wako pamoja na kuchunguza muonekano wako
Historia ya ugonjwa humsaidia daktari kujua kama kuna viashiria vya wewe kuwa na ugonjwa huu au lah, kama ni ugonjwa wa homa ya ini, je, ni ule wa kuambukiza (Infectious) au usio wa kuambukizwa (non-infectious).

NB:
Jinsi unavyojieleza vizuri kwa daktari kuhusiana na ugonjwa wako ndipo unavyompa wakati mzuri daktari wako kufanya maamuzi sahihi ya namna nzuri ya kuutibu ugonjwa wako. Daktari wako anavyokuuliza chochote kuhusiana na ugonjwa wako usifichefiche 'FUNGUKA', eleza kila kitu.

Kuchunguza muonekano wako, daktari wako anaweza akabinya taratibu sehemu ya tumbo kuona kama unasikia maumivu au kuna uvimbe au kama ini limevimba. Pia atachunguza kama ngozi yako au macho yako yana rangi ya njano.

2. Kuchunguza jinsi ini lako linavyofanya kazi
Uchunguzi huu hufanywa kwa kuchukua sampuli ya damu ya mgonjwa, pale ambapo daktari alivyosikiliza historia yako pamoja na kuchunguza muonekano wako pasipo kuona tatizo. Kama ikionekana kwenye damu yako kuna vichochezi vingi (enzymes), hii itaashiria kwamba ini lako lina tatizo. Kama daktari hajaona chochote basi atafanya uchunguzi mwingine wa damu.

3. Kipimo kingine cha damu
Ikiwa ini lako limeonekana linafanya kazi vizuri, daktari wako anaweza akachukua kipimo kingine cha damu kuchunguza chanzo cha tatizo. Uchunguzi huu unahusisha kuangalia uwepo wa virusi wanaosababisha homa ya ini (Hepatitis virus), vilevile anaweza akachunguza uwepo wa 'antibodies' ambazo husababisha hali ya mwili inayoitwa 'Autoimmune disease', hali hii hutokea pale ambapo kinga za mwili huanza kuvamia seli hai za mwili ikiwemo seli za ini, hali inayopelekea ugonjwa wa homa ya ini. Kama daktari hajaona chochote atafanya kipimo kingine.

4. Kupiga Ultrasound
Pia daktari wako anaweza akatumia kipimo cha ultrasound kuchunguza tatizo lako, kipimo hiki hutoa mawimbi (ultrasound waves) ambayo hutengeneza picha ya muonekano wa viungo vyako tumboni. Uchunguzi huu utamsaidia daktari wako kuchunguza kwa makini muonekano wa ini lako pamoja na viungo jirani kwa kuchunguza yafuatayo;
  • Majimaji tumboni
  • Kuharibika kwa ini au kuvimba
  • Vivimbe vyenye usaa
  • Muonekano wa tofauti kwenye nyongo
  • Vilevile kunguza muonekano wa kongosho (Pancreas), uchunguzi utamsaidia daktari kujua kama ini lako lina tatizo au lah.

Photo Credit: © Becky Upham   Website: www.everydayhealth.com
Picha: Muonekano wa ini lenye afya (Kushoto) na ini liliharibika (Kulia)  



Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

Previous Post Next Post