SEHEMU YA PILI
5. Kipimo cha Biopsy (Liver
biopsy)
Kipimo hiki huhusisha kuchukuliwa
kwa tishu za ini kwa ajili ya uchunguzi, pia kipimo hiki huhusisha kuchukua
sampuli za tishu kwenye ngozi yako kwa kutumia sindano pasipo kufanya
oparesheni. Kipimo cha ultrasound humsaidia daktari wako wakati wa kuchukua
sampuli za tishu.
Kipimo hiki cha biopsy humsaidia
daktari wako kutambua ni kwa kiwango gani ini lako limeharibika.
NB:
Maelezo haya ya uchunguzi siyo
muongozo, bali ni mambo ambayo daktari wako anaweza akafanya kulingana na hali
ya mgonjwa aliyonayo. Kumbuka, jinsi unavyojieleza vizuri kwa daktari ndivyo
unavyompa wakati mzuri daktari wako kufanya maamuzi sahihi. Pia hata kama huna
dalili yoyote nenda kapime hospitali ili kujua kama una virusi wa homa ya ini
au lah, kama huna basi upatiwe chanjo.
MATIBABU NA NAMNA YA KUJIKINGA
Matibabu ya ugonjwa wa homa ya ini
hutegemea aina ya virusi ulivyonavyo, kama vina madhara ya muda mfupi au muda
mrefu (Acute or Chronic), kwamba baadhi ya virusi wana tiba na wengine hawana
tiba, pia baadhi ya virusi huweza kuzuiwa kwa chanjo pamoja na mwenendo mzuri
wa maisha kama kupunguza matumizi ya pombe n.k.
A: VIRUSI VYA HOMA YA INI
(HEPATITIS VIRUSES/INFECTIOUS HEPATITIS)
Yafwatayo ni matibabu ya homa ya
Ini kulingana na aina ya virusi vilivyosababisha ugonjwa huo na namna ya
kujikinga.
1. Hepatitis A virus (Hepatitis A)
Homa ya ini inyosababishwa na
virusi aina ya A haitaji matibabu yoyote kwa sababu ni ugonjwa wa muda mfupi
(short term illness). Ingawa mtu anaweza kulala ili kujipumzisha endapo ukaleta
uchovu wa mwili kwa kiwango kikubwa. Ukianza kutapika na kuharisha muone
daktari mara moja.
Namna ya kujikinga
- Chanjo ya homa ya ini aina ya A ipo, watoto wadogo wanaweza kupewa chanjo hiyo wakiwa na umri kuanzia miezi 12 hadi 18, huwa ni muendelezo wa chanjo mbili. Vilevile watu wazima wasio na mambukizi ya ugonjwa huu inapaswa wapatiwe chanjo hii, pia chanjo hii inaweza kuunganishwa na chanjo ya kirusi aina ya B kwa wakati mmoja.
- Hakikisha mazingira unayoishi au unayofanyia kazi yapo safi wakati wote pamoja na kula chakula na maji katika hali ya usafi, kwa sababu kirusi hiki aina ya A huenezwa kwa uchafu.
NB:
Jinsi ulivyo na afya yako njema au
unavyoumwa, huwezi kujua kama una virusi vya homa ya ini aina ya A au lah.
Hakikisha unakwenda hospitali kupima afya yako, ukigundulika una virusi wa homa
ini daktari ataamua ni namna gani nzuri ya kuokoa maisha yako.
2. Hepatitis B virus (Hepatitis B)
Homa ya ini inayosababishwa na
virusi aina ya B hususani ile ya muda mfupi (Acute) haitaji matibabu yoyote.
Ila homa ya ini aina ya B iliyokomaa (Chronic) ina tiba yake (antiviral
medications), Tiba hii hupewa mgonjwa kwa miezi kadhaa mfululizo au mwaka,
itategemeana na hatua ya ugonjwa wako.
Pia tiba ya ugonjwa huu inahitaji
ufwatiliaji wa karibu sana (regular medical evaluations and monitoring),
Daktari atachunguza afya ya mgonjwa baada ya matibabu kwamba anapata nafuu au
hali inazidi kuwa mbaya zaidi, ikigundulika hali inazidi kuwa mbaya daktari
ataamua namna nyingine ya kufanya.
Namna ya kujikinga
- Chanjo ya homa ya ini aina ya B ipo, watoto wote waliozaliwa inapaswa wapatiwe chanjo hii. Muendelezo wa chanjo tatu za homa hii hupewa mtoto hadi kufikia miezi sita. Vilevile chanjo hii inapaswa kupatiwa wahudumu wa afya ambao mara zote wanakuwa wakiwahudumia wagonjwa hawa. Pia watu wengine wasiowahudumu wa afya wanatakuwa wapate chanjo hii.
- Epuka kufanya ngono zembe
- Epuka kuchangia vitu vyenye ncha kali kama sindano, nyembe n.k.
- Wahudumu wa afya wahakikishe damu anayoongezewa mgonjwa imepimwa virusi vya homa ya ini.
NB:
Jinsi ulivyo na afya yako njema au
unavyoumwa, huwezi kujua kama una virusi vya homa ya ini aina ya B au lah.
Hakikisha unakwenda hospitali kupima afya yako, ukigundulika una virusi wa homa
ini daktari ataamua ni namna gani nzuri ya kuokoa maisha yako.
3. Hepatitis C virus (Hepatitis C)
Tiba ya ugonjwa wa homa ya ini
aina ya C ipo, Dawa hizo (Antiviral medications) hutibu vizuri ugonjwa huu kwa
hali yoyote ya ugonjwa aidha ulio wa muda mfupi au uliokomaa (Acute or
Chronic), ingawaje inahitaji ufwatiliaji wa karibu sana wa kimatibabu ili
kubaini kama dawa hiyo inafanya kazi vizuri au lah.
Namna ya kujikinga
- Mpaka sasa hakuna chanjo ya Homa ya Ini aina ya C.
- Epuka kufanya ngono zembe
- Epuka kuchangia vitu vyenye ncha kali kama sindano, nyembe n.k.
- Wahudumu wa afya wahakikishe damu anayoongezewa mgonjwa imepimwa virusi vya homa ya ini.
NB:
Jinsi ulivyo na afya yako njema au
unavyoumwa, huwezi kujua kama una virusi vya homa ya ini aina ya C au lah.
Hakikisha unakwenda hospitali kupima afya yako, ukigundulika una virusi wa homa
ini daktari ataamua ni namna gani nzuri ya kuokoa maisha yako.
4. Hepatitis D virus (Hepatitis D)
Mpaka sasa hakuna dawa ya kutibu
homa ya ini aina ya D.
Namna ya kujikinga
Homa ya ini aina ya D hukingwa
kwa kupata chanjo ya homa ya ini aina ya B. Kama umefwatilia maelezo yangu ya
hapo awali nilisema kwamba kirusi aina ya D hutegemea kirusi aina ya D
kuzaliana, hivyo ukizuia kirusi aina ya B basi umezuia kirusi aina ya D.
NB:
Jinsi ulivyo na afya yako njema au
unavyoumwa, huwezi kujua kama una virusi vya homa ya ini aina ya D au lah.
Hakikisha unakwenda hospitali kupima afya yako, ukigundulika una virusi wa homa
ini daktari ataamua ni namna gani nzuri ya kuokoa maisha yako.
5. Hepatitis E virus (Hepatitis E)
Mpaka sasa hakuna tiba mahsusi ya
homa ya ini aina ya E kwa sababu ugonjwa huu aina ya E hutokea kwa mda mfupi
(Acute). Ugonjwa huu hupona wenyewe pasipo matibabu yoyote, ingawaje mgonjwa
mwenye homa ya ini aina ya E anashauriwa kupumzika vya kutosha, kunywa maji
mengi, kula vizuri vyakula vyenye lishe bora na kuepuka kunywa pombe. Kwa
mwanamke mjamzito mwenye ugonjwa huu anahitaji uangalizi wa karibu sana.
Namna ya kujikinga
Hakikisha mazingira unayoishi au
unayofanyia kazi yapo safi wakati wote pamoja na kula chakula na maji katika
hali ya usafi, kwa sababu kirusi hiki aina ya E huenezwa kwa uchafu.
NB:
Jinsi ulivyo na afya yako njema au
unavyoumwa, huwezi kujua kama una virusi vya homa ya ini aina ya E au lah.
Hakikisha unakwenda hospitali kupima afya yako, ukigundulika una virusi wa homa
ini daktari ataamua ni namna gani nzuri ya kuokoa maisha yako.
B: MATIBABU YA VISABABISHI VINGINE
VYA HOMA YA INI (NON-INFECTIOUS HEPATITIS)
1. Kutumia pombe kupita kiasi
Punguza matumizi ya pombe, kumbuka kadiri unavyotumia pombe
sana ndivyo unazidi kulidhoofisha ini lako.
2. Sumu zitokanazo na madawa
Epuka kutumia madawa hovyo hovyo pasipo kufwata ushauri wa
daktari, kadiri unavyoendelea kunywa madawa mengi bila kufwata utaratibu wa
wataalamu wa afya ndivyo jinsi unavyolidhoofisha ini lako.
3. Autoimmune hepatitis
Daktari wako ataona namna gani inafaa kuitibu aina hii ya
homa ya ini, tujikumbushe kidogo; hii ni aina ya homa ya ini ambayo kinga ya
mwili hufikiri kana kwamba ini ni kitu kibaya mwilini na kuanza kushambulia
seli za ini mpaka kulizoofisha kabisa. Zifwatayo ni baadhi ya dawa ambazo
daktari wako anaweza kuzipendekeza;
(a) Dawa aina ya Corticosteroids
kama Prednisone au Budesonide
Dawa hii ni hususani wakati wa
hatua za awali za ugonjwa, huwa ni nzuri asilimia kubwa ya wagonjwa
wanazozitumia hupona.
(b) Azothioprine (Imuran)
Pia dawa hii hufanya vizuri inaweza ikatumika pamoja na dawa
aina ya Corticosteroids au ikatumika peke yake.
(c) Dawa zingine za kutibu aina hii ya homa ya ini ni pamoja na mycophenolate (CellCept), tacrolimus (Prograf) na
cyclosporine (Neoral) pia zinaweza kutumika kama mbadala wa dawa aina ya
'Azathioprine'
NB:
Dawa nilizozieleza hapo juu ni baadhi tu, daktari wako ndie
atakaeamua dawa gani inafaa kwako, pia kutegemeana na hali ya ugonjwa wako.
HITIMISHO
Kama umesoma na kuelewa vizuri makala hii mshirikishe
mwenzako ili na yeye aufahamu ugonjwa huu, ugonjwa huu ni hatari na unaua.
Hakikisha unaenda hospitali kupima afya yako, ili kubaini kama una maambukizi
ya virusi vya homa ya ini au lah. Kama una maoni au ushauri wowote kuhusiana na
makala hii usisite kuacha maoni yako hapo chini. Karibu sana!.
*MWISHO WA MAKALA HII*
Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo
Post a Comment