Zifahamu kanuni mbili muhimu za kuepuka umasikini



Kati ya maeneo muhimu katika maisha yako ambayo unatakiwa kuyawekea uzito na kipaumbele katika safari yako ya mafanikio, ni eneo la kifedha. Watu wengi wana nia na mipango mizuri ambayo imekwama kwa sababu hawana fedha za kufanya wanachotaka.

Hata hivyo kwa upande mwingine kuna ambao kwa nje ukiwaangalia utaona wana kipato kikubwa, kazi nzuri na mshahara mzuri, lakini ukweli ni kwamba hali zao za kifedha ni za kukimbizana kutoka mshahara hadi mshahara au wanategemea kipato cha kuingiza kila siku na siku ikitokea wameumwa, basi hawaingizi chochote. Kwa maneno mengine, ikitokea bahati mbaya wakapoteza kazi wanayofanya kwa miezi mitatu tu, hawataweza kuishi kwa amani kwani hawana kipato wala vitegauchumi vya kuwapatia kipato cha ziada.

Mafanikio ya kifedha ni matokeo ya kufanya uamuzi thabiti, lakini pia ni matokeo ya kuamua kuishi maisha ya nidhamu ya fedha ambayo wengi wameshindwa.

Hivi umewahi kujiuliza kwa nini hali yako kifedha iko hivyo? Na je, una mpango wa kubadilisha hali yako au wewe ni aina ya watu ambao hutegemea bahati itatokea kisha watafanikiwa? Kuna watu ambao walishawahi kupata pesa nyingi, lakini leo ni masikini. Kuna wengine waliwahi kufanikiwa sana kibiashara, lakini leo wamefilisika.

Mafanikio ya kifedha yana kanuni ambazo ni lazima uzizingatie ili uweze kukua na kufanikiwa. Zifuatazo ni kanuni mbili muhimu ambazo unatakiwa kuzizingatia katika kujenga uwezo wako wa kufanikiwa.


KANUNI YA KWANZA
Kanuni ya kwanza ni kuwa na bajeti. Kanuni hii inalenga kukufanya ujiulize swali la msingi; Fedha zangu huwa zinakwenda wapi? Watu wengi wanapata pesa ila hawawezi kabisa kueleza huwa zinatumika kwa matumizi gani. Hii ndiyo maana ukianza kutafakari fedha ambazo zimepita mkononi mwako tangu mwaka huu uanze na ukiangalia mambo uliyofanya utashangaa. Kama wewe ni mfanyakazi uliyeajiriwa hebu jiulize, tangu umeanza ajira jumla umepokea mshahara wa shilingi ngapi?.

Ukishapata jibu, hebu angalia mambo uliyofanya hadi sasa kwa kulinganisha na fedha zilizopita mikononi mwako.

Mafanikio ya kifedha siyo matokeo ya kiwango cha pesa unachopata bali ni matokeo ya kiwango cha pesa unachoweza kukibakiza mkononi mwako na jinsi utakavyoweza kukizalisha. Kila mwezi hakikisha una bajeti ya matumizi yako ambayo unakusudia, kwa kufanya hivyo utajenga nidhamu ya kutotumia pesa kwa mambo ambayo siyo muhimu.

Uzuri ni kwamba huhitaji kuwa mtaalamu ili kutengeneza bajeti, unachotakiwa ni kuorodhesha mahitaji yako na kuweka kiwango cha pesa unazotarajia kutumia. Kisha unaweka vipaumbele kwa maeneo ambayo unaona ni muhimu zaidi kwanza kabla ya mengine.

Ukianza kuwa makini na kufwatilia pesa zako zinaenda wapi, utagundua kuwa kuna fedha nyingi ambazo unazipoteza bila mwenyewe kujua kwa kununua na kutumia katika vitu visivyo vya lazima. Kujiwekea bajeti ni pamoja na kuweka kiwango kidogo cha pesa ambacho utakua unakiweka kama akiba katika maisha yako kila wakati unapopata pesa. Watu wengi ukiwaambia waweke akiba huwa wanakimbilia kusema kuwa hawana kipato cha kutosha, lakini watu wanaofanikiwa kifedha huwa wanaanza kuweka akiba kwa kiwango kidogo kisha wanaendelea kuongeza kadiri kipato chao kinavyokua. Akiba hii ndiyo baadae huitumia kuwekeza au kununua vitu vitakavyowaingizia pesa zaidi.

Leo ningependa upate muda kisha uandike kipato chako na matumizi yako ya mwezi. Hii itakupa picha kwa mwezi unatumia kiasi gani kufanyia kitu gani. Swali la muhimu hapa ni kuwa fedha zako huwa zinaenda wapi?

Huwezi kufanikiwa kama haujui fedha zako huwa zinakwenda kutumika kwa mambo gani.


KANUNI YA PILI
Kanuni ya pili ni ile ambayo ilitungwa na mwandishi nguli wa Uingereza, Cyril Northcote Parkinson ambayo ilipewa jina lake; "Kanuni ya Parkinson". Kanuni hii husema kuwa; "Katika hali ya kawaida mwanadamu anapoona kipato chake kimeongezeka, basi na yeye huongeza matumizi ili yafikie kumaliza ongezeko la kipato kipya alichokipata".

Kwa sababu hiyo, hata kama mtu ataongezwa kipato mara kumi, utashangaa bado anaishi kwa shida kama vile kipato hakijaongezeka. Ili ufanikiwe ni lazima ufanye juhudi za maksudi kuikiuka kanuni hii.

Unatakiwa ufanye uamuzi katika maisha yako kuwa hutabadilisha kwa haraka aina ya maisha unayoishi ili ongezeko la kipato ulilopata liwe na faida kwako. Watu wengi wakiongeza kipato, basi wanabadilisha nguo, gari hata nyumba ilimradi tu wanataka kuwathibitishia watu kuwa vipato vyao vimeongezeka.

Kama kweli unataka kufanikiwa kifedha ni lazima uhakikishe kuwa mabadiliko ya maisha yako hayaendi kwa kasi zaidi ya kipato chako. Hii ni kusema kuwa kwa kila ongezeko ambalo unalipata hakikisha hubadilishi staili ya maisha itakayosababisha utumie chote kilichoongezeka. Badala yake tumia kile kinachoongezeka kuwekeza.

Watu ambao kanuni hii imewaathiri ndio wale ambao kila wakati wanalazimika kuishi juu ya kipato chao. Ni rahisi kujua kama unaishi juu ya kipato chako kwa kuangalia aina ya madeni na mikopo uliyonayo. Kama wewe una madeni na mikopo ambayo yote imelenga kutatua shida za kila siku au kwa ajili ya fasheni, basi ujue kuna tatizo katika mfumo wako wa matumizi.

Hapa nazungumzia kama wewe huwa kila wakati unakopa kwa ajili ya kununua nguo, kulipa kodi ya nyumba, kununua simu ya kisasa, viatu n.k., basi ujue kuna tatizo katika mfumo wako wa kifedha na unahitaji kubadilika kabla umasikini haujakuvamia.

Shukrani nyingi zimuendee Mwandishi wa makala hii ndugu JOEL NANAUKA wa gazeti la Ijumaa Wikienda toleo la tarehe 23 - 29/09/2019.

Kama umependa makala hii usisite kumshirikisha mwenzako kwa kubofya viunganishi hapo chini vya mitandao ya kijamii kama Facebook, Twitter, Whatsapp n.k. Karibu sana kwa makala zingine na zijazo, kuwa na siku njema!.

Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

Previous Post Next Post