Zao la Pilipili kichaa 'Hot
pepper' au 'Chilli pepper' (Capsicum frutescens) hulimwa maeneo mengi
ulimwenguni ikiwemo nchini Tanzania. Matunda ya pilipili hutumika kwa matumizi
mbali mbali kama chakula au kama tiba (medicinal properties) na kuimarisha afya
ya mraji. Kwa upande wa chakula pilipili hutumika kama kionjo cha vyakula
mbalimbali kama Supu, kachumbali, nyama choma, nyama rosti, maharage, mboga za
majani, kutengenezea chilli sauce n.k. Kwenye chakula pilipili huongeza radha
maridhawa kabisa, ndio maana mtu aliyezoea kula vyakula vyenye pilipili huwa
hafurahii chakula kisichokua na pilipili.
Kwa upande wa tiba
pilipili/pilipili kichaa ina vitamini nyingi (Capsaicin compounds) ikiwemo
niacin, pyridoxine, riboflavin, na thiamine n.k. Uwepo wa vitamini hizi
pilipili hutumika katika kutengenezea madawa (Ointment) ya kuondoa maumivu ya
viungo na misuli. Kufahamu faida nyingi za kiafya za kutumia pilipili BOFYA
HAPA.
MAZINGIRA
Zao la pilipili/pilipili kichaa
hupendelea mazingira yenye joto la wastani kuanzia nyuzijoto 18°C - 30°C, joto likiwa chini ya
nyuzijoto 16°C
au zaidi ya nyuzijoto 30°C
huathiri utengenezaji wa matunda. Pia kitu muhimu cha kutilia maanani hapa ni
kwamba pilipili kichaa hufanya vizuri maeneo yenye joto. Kadiri joto linavyokua
kubwa (mpaka kufikia nyuzi joto 30°C)
ndivyo jinsi pilipili inavyozidi kuwa kali na yenye ubora zaidi. Ili kupata
pilipili yenye ubora inatakiwa joto lisipungue chini ya nyuzi joto 15°C.
Pia mwanga wa jua ni muhimu sana
kwa ukuaji wa mazao mengi ikiwemo zao la pilipili kichaa, hakikisha unapanda
zao hili mazingira yenye mwanga wa kutosha, usipande mazingira yenye kivuri,
zao hili halitafanya vizuri.
Zao hili hufanya vizuri kwenye
udongo tifutifu usiotwamisa maji na wenye kiasi cha tindikali kuanzia pH 5.5 -
7.5
Vilevile hufanya vizuri kwenye
maeneo yenye muinuko wa mita 1500 kutoka usawa wa bahari.
Kiasi cha mvua kinachohitajika kwa
mwaka ni mm 600 hadi mm 1250. Pia njia mbalimbali za umwagiliaji zinaweza
kutumika kuzalisha zao hili kama kutumia mifereji (Stream irrigation), njia ya
matone (Drip irrigation), mithiri ya mvua (Sprinkler irrigation) n.k. Chamsingi
hapo ni kwamba hakikisha shamba lako lina unyevu wa kutosha wakati wote, maji
yakizidi shambani au kukiwa na ukame uzalishaji utaathirika kwa kiwango
kikubwa.
AINA ZA PILIPILI KICHAA
Kuna aina nyingi za mbegu za
kisasa za pilipili kichaa, ingawaje wakulima wengi wamekuwa wakipanda mbegu
zilizotoka kwenye matunda ya pilipili yaliyovunwa kwenye maeneo yao. Ni muhimu
kupanda mbegu zilizothibitishwa kitaalamu (Certified seeds) kwa sababu huzaa
vizuri. Kama utaamua kutumia mbegu za matunda ya pilipili ulizopanda hakikisha
unavuna matunda ya pilipili yaliyokomaa na kuiva vizuri, kisha zikaushe,
zitwange kupata mbegu na zihifadhi mahara pakavu. Mbegu hizo hubakia na uwezo
wake wa kuota (viability) kwa miaka 2 hadi 3 tangia kuziandaa pasipokutumia
njia zozote za uhifadhi cha msingi tu hakikisha zinahifadhiwa mahara pakavu.
Baada ya miaka 3 mbegu hizo hupoteza uwezo wake wa kuota.
Kuna aina nyingi za pilipili
kichaa ambazo huzalishwa duniani kote, aina hizi za pilipili huwa na majina
tofauti kulingana na eneo husika. Zifuatazo ni aina za pilipili kichaa
zinazopandwa ulimwenguni kote na baadhi ya hizo hupandwa nchini Tanzania.
1. African Bird's eye
Hii ni aina ya pilipili inayotokea
barani afrika, hufikia urefu wa sm 2.5 na huzaa sana, zikikomaa na kuiva huwa
na rangi nyekundu au dhambarau. Ni kali, kiwango chake cha ukali ni Scoville Heat Units (SHU) 175,000.
2. Aji Amarillo (The Sunny yellow
chili pepper)
3. Aji Cito
Aina hii ni kali sana inatokea nchini Peru, hufanana na
Pilipili aina ya Lemon drop. Ni kali, kiwango chake cha ukali ni Scoville Heat Units (SHU) 80,000-100,000.
4. Aji Cristal
Aina hii huwa ndogo, zikikomaa na
kuiva huwa na rangi ya njano iliyochangamana na nyekundu, hutokea nchi ya
Chile. Ni kali, kiwango chake cha ukali ni Scoville Heat Units (SHU) 30,000.
5. Aji Habanero (Habanero)
Aina hii ni kali sana na ina radha ya matunda kwa mbali,
hukomaa kwa siku 70 (zikiwa kijani) au siku 85 (zikiwa zimeiva na kuwa njano).
Pilipili hizi hufikia urefu wa sm 7.5 Ni kali kiasi, kiwango chake cha ukali ni Scoville Heat Units (SHU) 5,000-10,000.
6. Aji Limo
Aina hii pia hutokea nchini Peru, hufikia urefu wa sm 5 -
7.5 (Inchi 2 - 3), zina rangi nyekundu, njano, rangi ya chungwa au zambarau au
nyeupe. Ni kali, kiwango chake cha ukali ni Scoville Heat Units (SHU) 30,000-50,000.
7. Aji Panca
Aina hii ya pilipili hutokea
nchini peru, hupandwa sana maeneo ya pwani ya nchi hii, zina rangi nyekundu
hufikia urefu wa sm 7.5 - 12 (Inchi 3 - 5). Ni kali kidogo sana, kiwango chake cha ukali ni Scoville Heat Units (SHU) 500.
8. Aji Pineapple
Aina hii ina matunda yenye rangi
ya njano inayovutia sana na hufikia urefu wa sm 5 - 7.5 (Inchi 2 - 3). Hukomaa
zikiwa za njano lakini zikiiva huwa na rangi ya njano. Ni kali, kiwango chake cha ukali ni Scoville Heat Units (SHU) 20,000.
9. Aji Sivri
Aina hii huzalishwa nchini Uturuki
hufanana na pilipili aina ya cayenne, huzaa sana hutoa matunda kuanzia 50 na
kuendelea kwa mche mmoja. Ni ndefu zinafikia urefu wa sm 12 - 25 (Inchi 5 -
10), na zina maumbile ya kubonyea bonyea na zinavyokua hujikunja. Ni kali, kiwango chake cha ukali ni Scoville Heat Units (SHU) 5,000 – 30,000.
NB:
Neno 'Aji' humaanisha aina ya pilipili zinazotokea Amerika
ya kusini.
10. Aleppo (Halaby)
Aina hii hutokea nchini Syria, zimepewa jina la jiji
linaloitwa 'Aleppo' nchini Syria, pia huzalishwa sana nchini Uturuki. Ni kali kidogo, kiwango chake cha ukali ni Scoville Heat Units (SHU) 10,000.
Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo
Post a Comment