Zao la maembe (Mango), Mangifera indica, hulimwa meneo mengi ulimwenguni ikiwa ni pamoja na nchini Tanzania. Tunda hili lina virutubisho muhimu kwa afya ya binadamu, zao hili lina matumizi mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuliwa jinsi lilivyo likiwa limeiva, kutengenezea juisi, mabaki ya matunda huweza kulishia mifugo, majani machanga ya mparachichi hutumika kulishia mifugo hususani ng’ombe, mbuzi, kondoo n.k
AINA
Kuna aina mbali mbali za maembe kulingana na maeneo husika, mara nyingi kuna aina ya kisasa na yale ya kienyeji, maembe ya kisasa huchukua muda mfupi kukomaa na kuanza kula matunda wakati yale ya kienyeji huchukua muda mrefu kukomaa na kuanza kula matunda.
MAZINGIRA
Maembe hupendelea maeneo ya kitropiki yenye joto la wastani kuanzia nyuzijoto 24ºC hadi 28ºC, mwembe ukishaota na kukua hustahimili ukame wakati wa kiangazi. Vilevile mwembe huhitaji muda wa kiangazi au kipindi cha baridi kiasi kutoa maua na kutengeneza matunda. Mvua ikinyesha wakati wa kutoa maua huathiri mmea kutengeneza matunda. Maeneo ya kitropiki ambayo hakuna kubadirika kwa mnyesho wa mvua au hali joto, mwembe unaweza usitoe matunda kabisa. Hii ina maana kwamba ili mwembe uweze kutoa maua na matunda inatakiwa kuwepo na msimu wa kiangazi na masika, hali hii pia itasaidia kuleta mabadiliko ya joto ili kutengeneza maua na matunda.
Pia maembe hufanya vizuri kwenye muinuko kuanzia m 0 hadi m 1000 kutoka usawa wa bahari, muinuko zaidi ya m 1200 kutoka usawa wa bahari maembe hayafanyi vizuri kunakua na uzalishaji hafifu sana. Kiasi cha mvua kinacho hitajika na maembe ni mm 1500 kwa mwaka, ingawaje pia kwa maeneo yenye mvua ndogo kiasi cha mm 650 kwa mwaka, maembe hufanya vizuri japo mavuno hayatazidi maeneo yenye mvua nyingi (mm 1500 kwa mwaka).
Maembe hupendelea udongo wa aina mbalimbali wenye rutuba, wenye kina kirefu na usiotwamisha maji, epuka udondo wenye kina kifupi, wenye mawe mawe au changarawe na
Wenye bezi nyingi (alkaline soils). Pia zao hili hupenda udongo wenye tindikali kiasi cha pH 5.5 hadi 7.5
Miche michanga inatakiwa imwagiliwe mara tu kiangazi kitakapoanza, Miti iliyokomaa inahitaji kipindi cha ukavu angalau kwa miezi mitatu ili kuanza kutoa maua, baada ya matunda kuanza kutengenezwa ni wakati mahsusi wa kumwagilia miti yako ili matunda yakue vyema.
KUANDAA MBEGU NA KUPANDA
Mwembe hupandwa kwa kutumia mbegu na vikonyo (vegetatively), baadhi ya aina za maembe hupandwa kwa kutumia mbegu na baadhi kwa kutumia vikonyo. Kuna makundi mawili ya maembe kulingana na hali hii kama ifuatavyo;
1) Polyembryonic cultivars
Aina hii mbegu zake huwa na viini zaidi ya kimoja na hupandwa kwa kutumia mbegu ambapo hutoa mche unaofanana vyema na mwembe husika. Mara nyingi miembe hii huwa ni ya kienyeji
2) Monoembryonic cultivars
Aina hii mbegu zake huwa na kiini kimoja, ikipandwa kwa kutumia mbegu hutoa miche dhaifu isiyofanana na mwembe husika. Kwa hiyo aina hii hupandwa kwa kutumia vikonyo (vegetative). Kuna faida nyingi za kupanda maembe kwa kutumia vikonyo kama; kutoa miti inayokua na kutoa matunda mapema, miti midogo n.k
Mbegu za maembe hupoteza uwezo wake wa kuota haraka sana, tumia mbegu zenye afya kutoka kwenye matunda yaliyokomaa na mazuri. Osha mbegu hizo na zianike kivulini kwa siku chache, baada ya kukauka zipande kwenye kitalu kwa nafasi ya sm 15 x sm 30 na kimo cha sm 5. Wakati wa kupanda hakikisha pembe ya mbegu yenye mduara mzuri iangalie juu ili kutengeneza miche iliyonyooka.
Pia ili kuharakisha uotaji, gamba la nje linaweza kuondolewa kabla ya kupanda. Mara baada ya mbegu kuota, baada ya wiki 4 na kimo cha sm 10 mbegu hizo huamishwa kwenye vyombo au tyubu vyenye ujazo wa lita 4
KUFANYA GRAFTING/BUDDING
Miche huwa tayari kufanyiwa grafting baada ya kufikia unene wa penseli na kimo cha sm 20 kutoka usawa wa ardhi. Grafing ni kitendo cha kuunganisha miche miwili ya jamii moja kwa lengo la kuboresha uzalishaji na ubora. Miche iliyooteshwa huuanganishwa na vikonyo viliyotoka kwenye miembe iliyobora au ya kisasa. Miche iliyofanyiwa budding huwa tayari kupandikizwa baada ya miezi 4 tangu kufanyiwa budding. Kufahamu zaidi namna ya kufanya grafting/budding tazama video ifuatayo;
Video Credit: Grafting Lesson Official youtube channel
KUPANDIKIZA
Kabla ya kupandikiza hakikisha shamba lako limeandaliwa vizuri, lisiwe na vichaka au magugu ya aina yoyote, liwe safi pia kama litalimwa itakua vyema zaidi. Miche ipandikizwe mara tu mvua za masika zinavyoaanza kunyesha. Nafasi inayotakiwa kwa maembe ni mita 9 x mita 9 au mita 13 x mita 13, pia unaweza ukabana nafasi hadi mita 6 x mita 4 au mita 5 x mita 5. Chimba mashimo yenye ukubwa wa sm 90 x sm 90 x sm 90 yaani urefu sm 90, upana sm 90 na kina cha sm 90, wakati wa kuchimba tenganisha udongo wa juu na wa chini.
Udongo wa juu uchanganywe na samadi iliyooza vizuri kiasi cha ndoo 2 kubwa za lita 20 na pia uchanganywe na mkono mmoja au miwili ya mbolea aina ya minjingu rock phosphate kasha rudisha mchanganyiko huo ndani ya shimo. Baada ya hapo pandikiza mche wako wa mwembe na sindilia vyema kisha tandaza juu udongo wa chini uliotolewa kwenye shimo hapo awali. Baada ya kupanda mwagilia maji vizuri, kwa mwaka wa kwanza hakikisha unamwagilia maji miti yako hususani wakati wa kiangazi.
Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo
Post a Comment