Kilimo Bora cha Soya - Sehemu ya Tatu (Growing Soyabean - Part Three)


SEHEMU YA TATU

B: MAGONJWA

Miongoni mwa magonjwa mabaya sana ya soya ni pamoja na 'Soyabean rust' ambao husababishwa na kimelea anaeitwa Phakopsora pachyrhizi, ugonjwa huu hupunguza mavuno mpaka asilimia 90%. Yafuatayo ni maelezo ya kina kuhusiana na magonjwa mbali mbali ya soya. 

1. Soybean rust (Phakopsora pachyrhizi)
Ugonjwa huu husababishwa na vimelea wa fangasi aina ya Phakopsora pachyrhizi. Vimelea hao husambaaa zaidi pakiwa na unyevu kwenye majani kwa muda mrefu, pia wakati huo pakiwa na joto wastani chini ya nyuzijoto 28°C Dalili za ugonjwa huu ni pamoja na uwepo wa madoa yenye kipenyo cha mm 2 - 5 chini ya majani yenye rangi kijani mpauko, kahawia iliyochangamana na njano, kahawia iliyochangamana na weusi au kahawia iliyochangamana na wekundu. Vilevile madoa hayo huonekana kwenye shina la jani, matunda ya soya (pods) na mashina. Katika hatua za awali za ugonjwa huu dalili huweza kufananzaa ugonjwa mwengine unaoitwa Bacteria postules (Bean blight) 

Mara nyingi dalili za ugonjwa huu huanza kuonekana katikati na mwishoshoni mwa ukuaji wa mmea, kwa sababu unyevu wa muda mrefu na kipindi cha baridi husaidia vimelea hawa kusambaa zaidi. Vimelea wa ugonjwa huu hawaenezwi kupitia mbegu, ugonjwa huu huathiri ukuaji wa mmea na hupunguza uzalishaji mpaka asilimia 90%. 

© Reid Frederick, USDA Agricultural Research Service, Bugwood.org 
Picha: Soyabean rust

© Edward Sikora, Auburn University, Bugwood.org
Picha: Soyabean rust

Namba ya kudhibiti 
  • Panda aina ya soya inayovumilia ugonjwa huu.
  • Badirisha mazao kwa kupanda mimea jamii nyingine tofauti na mikunde
  • Ondoa mimea yote michanga yenye dalili za ugonjwa huu ndani ya siku 7 tangu uone dalili
  • Teketeza mimea yote iliyoathirika na ifukie nje ya shamba au ichome moto

2. Soybean mosaic Virus (Potyvirus SMV)
Ugonjwa huu husababishwa na virusi, virusi hawa husambazwa kutoka mmea mmoja hadi mwingine kupitia majimaji ya mmea (sap). Maji maji hayo hufyonzwa na wadudu waharibifu aina ya aphids (Vidukari mafuta), hii ina maana kwamba wanavyokua wanahama kutafuta chakula kutoka mmea mmoja hadi mwingine ndivyo husambaza ugonjwa huu. Pia ugonjwa huu husambazwa kupitia mbegu, hii ina maana kwamba mbegu iliyotoka kwenye mmea uliyoathirika huweza kusababisha ugonjwa kwa mmea mwingine baada ya kupanda mbegu hiyo. 

© Craig Grau, Bugwood.org
Picha: Soyabean rust

© Albert Tenuta, Ontario Ministry of Agriculture, Food and Rural Affairs, Bugwood.org
Picha: Soyabean rust

Dalili za ugonjwa
  • Mmea hudumaa na matunda yake huwa bapa pasipokua na mbegu ndani 
  • Majani huwa na rangi ya kijani iliyochangamana na nyeusi pia huwa vivimbe vivimbe vyenye maji maji. 
  • Mbegu zilizotoka kwenye mmea ulioathirika huwa na rangi iliyochangamana (mabaka mabaka) ya kahawia au nyeusi. 
  • Mbegu za mmea ulioathirika huwa mdogo sana na uotaji wake ni hafifu sana tofauti na mbegu zilizotoka kwenye mmea usio na ugonjwa. 
Namna ya kudhibiti 
  • Tumia mbegu bora zilizothibitishwa kitaalamu na zisizokua na magonjwa. 
  • Waangamize wadudu wanaosambaza ugonjwa huu (Aphids/Vidukari mafuta) kwa kutumia dawa za asili kama juisi ya mbegu au majani ya mwarobaini (Pulizia juisi ya mbegu za mwarobaini kwa mchanganyiko wa gramu 30 - 50 kwa lita 1 ya maji wakati wa kipindi cha awali cha ukuaji wa mmea), kama utakosa dawa za asili basi tumia dawa za kiwandani, sharti zingatia matumizi sahihi ya dozi ili kupunguza mlundikano wa sumu kwenye mmea wako. 
  • Panda aina ya soya inayohimili athari za ugonjwa huu. 
  • Ondoa na choma moto masalia yote ya mimea iliyoathirika

3. Bean yellow mosaic virus (BYMV) 
Ugonjwa huu nao husababishwa na virusi, pia virusi hawa husambazwa na wadudu waharibifu aina ya Aphids (Vidukari mafuta), wadudu hawa wanavayofyonza maji maji ya mmea na kuhamia kwenye mmea mwingine ndipo hueneza maambukizi. Pia ugonjwa huu huenezwa kwa njia ya mbegu zenye ugonjwa (seed borne) 

© Dr Parthasarathy Seethapathy, Amrita School of Agricultural Sciences, Amrita Vishwa Vidyapeetham, Bugwood.org 
Picha: Bean yellow mosaic virus

Dalili za Ugonjwa 
  • Mmea hauonyeshi kudumaa kama ilivyo kwa ugonjwa wa (SMV) 
  • Majani machanga huwa na mabaka mabaka ya rangi ya njano au mara nyingine kunakua na kama mkanda wa rangi ya njano juu ya majani. 
  • Madoa madoa yenye rangi mithiri ya kutu, huonekana juu ya rangi ya njano ya majani yaliyokomaa. 
Namna ya kudhibiti 
  • Tumia mbegu za soya zilizothibitishwa kitaalamu na zisizokua na magonjwa 
  • Waangamize wadudu wanaosambaza ugonjwa huu (Aphids / Vidukari mafuta) kwa kutumia mbegu za mwarobaini kama nilivyoelekeza hapo juu.

4. Soybean bacterial blight (Pseudomonas savastonoi pv. glycinea
Ugonjwa huu husababishwa na vimelea wa bakteria, vimelea hawa husambazwa kupitia upepo wenye matone ya mvua, pia wakati wa kulima shamba kipindi ambacho majani yanakua na unyevu mwingi na kupitia kupanda mbegu zenye ugonjwa (seed borne). 

© Howard F. Schwartz, Colorado State University, Bugwood.org
Picha: Soyabean bacteria blight

Dalili za ugonjwa 
  • Mabaka au michirizi yenye rangi nyeupe huonekana kwenye mashina, mashina ya majani (petioles) na matunda (Pods). 
  • Mabaka madogo yenye maji maji yenye rangi ya njano au kahawia mpauko huonekana kwenye majani. Baada ya hapo sehemu za katikati za madoa hayo hukauka na kubadirika rangi kutoka nyekundu iliyochangamana kwenda nyeusi na huzungukwa na mstari wenye rangi ya njano iliyochangamana na kijani. 
  • Majani machanga huathiriwa zaidi, huharibiwa, hudumaa na kuwa na rangi ya njano iliyochangamana na kijani. 
  • Mabaka haya huongezeka ukubwa kipindi cha mvua na hali ya ubaridi baadae huwa tishu zilizokufa. 
Namna ya kudhibiti 
  • Tumia mbegu za soya zilizothibitishwa kitaalamu na zisizokua na magonjwa. 
  • Panda aina ya soya inayohimili athari za ugonjwa huu 
  • Hakikisha shamba lako lipo safi wakati wote. 

5. Wildfire disease of soybeans (Pseudomonas syringae pv. tabaci) 
Ugonjwa huu husababishwa na vimelea wa bakteria aina ya Pseudomonas syringae, una uhusiano na athari za ugonjwa wa Mnyauko bakteria (Bacteria blight) na Bacteria pustule. Ugonjwa huu huenezwa kupitia mbegu iliyoathirika (seed borne) na mabaki ya mimea yenye ugonjwa. 




Dalili za ugonjwa 
  • Majani huwa na madoa yenye rangi ya kahawia mpauko (huwa na tishu zilizokufa) huzungukwa mstari mpana wa rangi ya njano. 
  • Kwenye mazingira yenye unyevu wa wastani madoa hayo huongezeka ukubwa na kusababisha maeneo makubwa yenye tishu zilizokufa kwenye majani. 
Namna ya kudhibiti 
  • Tumia mbegu zilizothibitishwa kitaalamu na zisizokua na magonjwa 
  • Hakikisha shamba lako ni safi wakati wote 
  • Panda aina ya soya inayohimili athari za ugonjwa huu 

6. Soybean downy mildew (Peronospora manshurica
Ugonjwa huu husababishwa na vimelea wa fangasi aina ya Peronospora manshurica. huongezwa kasi na uwepo wa joto la wastani na unyevu mwingi shambani. ugonjwa huu huathiri majani, matunda (pods) na mbegu zake. 

© Daren Mueller, Iowa State University, Bugwood.org
Picha: Soyabean down mildew

© Daren Mueller, Iowa State University, Bugwood.org
Picha: Soyabean downy mildew

Dalili za ugonjwa 
  • Rangi ya njano iliyochangamana na kijani huonekana sehemu ya juu ya majani. ugonjwa ukizidi maeneo yaliyoathirika hubadirika rangi na kuwa ya kijivu iliyochangamana na kahawia au kahawia yenye weusi yakizungukwa na mstari wa njano uliochangamana na kijani. 
  • Majani yaliyoathirika hudondoka yakiwa bado machanga 
  • Madoa ya kwenye majani hutengeneza fangasi pakiwepo joto la wastani na unyevu mwingi. 
Namna ya kudhibiti 
  • Tumia mbegu za soya zilizothibitishwa kitaalamu na zisizokua na magonjwa. 
  • Panda aina ya mbegu zinazohimili athari za ugonjwa huu. 

7. Pod and stem blight (Diaporthe phaseolorum pv. sojae
Ugonjwa huu husababishwa na vimelea wa fangasi aina ya Diaporthe phaseolorum, huongezwa kasi na uwepo wa unyevu mwingi shambani, pia huenezwa kupitia mbegu zenye ugonjwa na masalia ya mimea shambani yenye ugonjwa. 

© Clemson University - USDA Cooperative Extension Slide Series , Bugwood.org
Picha: Pod and steam blight

© Daren Mueller, Iowa State University, Bugwood.org
Picha: Pod and steam blight

Dalili za Ugonjwa 
  • Vidoa vidogovidogo vya fangasi wenye rangi nyeusi huonekana kwenye mashina na matunda (Pods), kwenye matunda fangasi hawa hutawanyika lakini kwenye mashina hujipanga kwa mstari. 
  • Ugonjwa huu huua mmea kipindi cha mwisho cha ukuaji wake 
Namna ya kudhibiti 
  • Hakikisha usafi wa shamba (ondoa magugu shambani), choma moto masalia yote ya mimea iliyoathirika 
  • Badirisha mazao kwa kupanda mazao mengine tofauti na mimea jamii ya mikunde kama mazao ya nafaka (mahindi, mtama n.k), mazao ya mfuta (alizeti, ufuta n.k) 
  • Tumia mbegu za soya zilizothibitishwa kitaalamu na zisizokua na magonjwa. 
  • Panda aina za mbegu zinazohimili athari za ugonjwa huu.

8. Bacterial postule (Xanthomonas axonopodis pv. glycines) 
Ugonjwa huu husababishwa na vimelea wa bakteria aina ya Xanthomonas axonopodis, huenezwa kupitia mbegu zenye ugonjwa na mabaki ya masalia ya mimea yenye magonjwa. Ugonjwa huu hufanana kidogo na 'bacterial blight' kwa hatua za awali lakini tofauti yake ni kwamba; Bacterial blight huwa na mabaka yenye maji maji ambayo baadae hukauka, wakati 'bacterial postules' huwa na vivimbe vyenye maji maji yaliyovunda ambavyo hutokea chini ya jani. 

© Daren Mueller, Iowa State University, Bugwood.org
Picha: Bacteria Pustule

Dalili za ugonjwa 
  • Dalili hufanana na zile za bacterial blight kwa kipindi cha awali huwa na madoa madogo yenye rangi ya njano iliyochangamana na kijani na katikati huwa na rangi ya kahawia iliyochangamana na wekundu. Baadae vivimbe (Postules) vyenye maji hutokea katikati ya doa hususani chini ya jani. 
Namna ya kudhibiti 
Udhibiti wa ugonjwa huu hufanana na ule wa bacterial blight kama ifuatavyo; 
  • Hakikisha usafi wa shamba (ondoa magugu), choma moto masalia yote ya mimea iliyoathirika. 
  • Tumia mbegu za soya zilizothibitishwa kitaalamu na zisizokua na magonjwa.
  • Panda aina ya mbegu zinazohimili athari za ugonjwa huu. 

9. White mould (Sclerotinia sclerotiorum
Ugonjwa huu husababishwa na vimelea wa fangasi aina ya Sclerotinia sclerotiorum, ugonjwa huu huongezwa kasi na uwepo wa joto la wastani na mvua au unyevu mwingi shambani kabla ya mmea kutoa maua au matunda, huathiri mashina na matunda (pods). 

© Daren Mueller, Iowa State University, Bugwood.org 
Picha: White mould

© Daren Mueller, Iowa State University, Bugwood.org
Picha: White mould

Dalili za ugonjwa 
  • Kuoza sehemu ya chini ya shina, uozo huo hufunikwa na fangasi weupe kama pamba (mycelium), baadae juu ya fangasi hao huota vitu vidogo vidogo vyeusi (sclerotia). vilevile vitu hivi vyeusi huonekana ndani ya shina likikatwa. 
  • Mbegu nazo huathirika ndani ya matunda ya soya yenye ugonjwa, kama athari itaanza mapema basi mbegu za soya huwa bapa na husinyaa, mara nyingine baadhi ya mbegu ndani ya matunda ya soya huoza na kuwa fangasi wenye rangi nyeusi (black sclerotia) 
  • Mmea ulioathirika hufa mapema, mara nyingine kabla ya kutengeneza mbegu, athari huanza wakati mmea unatoa maua. 
Namna ya kudhibiti 
  • Tumia mbegu zilizothibitishwa kitaalamu na zisizokua na magonjwa. 
  • Panda aina za mbegu zinazohimili athari za ugonjwa huu. Aina za soya zinazokomaa mapema (Eary maturity) mara nyingi huepuka athari za ugonjwa huu kwa sababu hutoa maua mapema. Tofauti na aina zinazochelewa kukomaa (Late maturity) huwa na magonjwa mengi hii inatokana na wingi majani na na kuchelewa kutoa maua. 
  • Epuka kupanda soya kwenye shamba lililopandwa maharage (mazao jamii ya mikunda), alizeti n.k, Badirisha mmazao. 
  • Epuka kupanda kwa kubana nafasi chini ya sm 76 kwa aina za soya zinazoathiriwa sana pia kwenye shamba lenye historia ya ugonjwa huu.
  • Epuka kumwagilia maji mengi mimea yako mpaka utoaji wa mimea utakapokoma. 
  • Hakikisha usafi wa shamba (ondoa magugu kila yanapoonekana) 

10. Damping-off diseases na Anthracnose (Colletotrichum truncatum na Glomerella glycines
Magonjwa haya mawili husababishwa na vimelea wa fangasi aina ya Colletotrichum truncatum na Glomerella glycines hufanya kazi kwa pamoja na kuleta haya magonjwa mawili. Magonjwa yote haya mawili huongezwa kasi na uwepo wa mazingira yenye unyevu mwingi na joto la wastani, pia huenezwa kupitia mbegu zenye ugonjw na huathiri mashina na matunda (Pods) hususani mmea ukikaribia kukomaa. 

© Daren Mueller, Iowa State University, Bugwood.org
Picha: Anthracose (Colletotrichum truncatum)

© XB YANG
Picha: Damping-off

Dalili za ugonjwa 
  • Kuoza kwa mbegu kabla ya kuota au kufa kwa miche baada ya kuota. 
  • Maeneo yaliyoathirika huwa na mabaka meusi yaliyobonyea wakati wa unyevu mwingi mabaka haya hufunikwa na mlundikano wa mbegu za fangasi (spores) zenye rangi ya pinki. 
  • Mbegu za soya zenye ugonjwa huu zikipandwa, nyingi huoza chini ya udongo. Zinazobahatika kuota huwa na mabaka yaliyobonyea na yenye rangi ya kahawia kwenye majani. Baadae mabaka hayo huenea mpaka kwenye shina. Magonjwa haya huathiri sana mimea michanga kuliko ile iliyokua. 
Namna ya kudhibiti 
  • Badirisha mazao kwa kupanda mazao mengine tofauti na ile ya jamii ya mikunde. 
  • Kama unamwagilia, hakikisha hutumii maji mengi kwani unyevu ukizidi huongeza kasi ya ugonjwa huu. 
  • Panda aina za soya zinazohimili athari za ugonjwa huu. 
  • Tumia mbegu za soya zilizothibitishwa kitaalamu na zisizokua na magonjwa. 

11. Purple seed stain (Cercospora kikuchii) 
Ugonjwa huu husababishwa na vimelea wa fangasi aina ya Cercospora kikuchii, fangasi hawa hutengeneza mbegu (spores) kwenye miche michanga iliyoathirika, mbegu hizi za fangasi huwa ndio chanzo cha maambukizi kwenye majani, mashina na matunda (Pods). mbegu hizi za fangasi husambazwa kwa upepo na michapo ya mvua (rain splash). 

© Gerald Holmes, Strawberry Center, Cal Poly San Luis Obispo, Bugwood.org
Picha: Purple seed stain 

© Gerald Holmes, Strawberry Center, Cal Poly San Luis Obispo, Bugwood.org
Picha: Purple seed stain

Dalili za ugonjwa 
  • Madoa yenye rangi ya dhambarau huonekana kwenye mbegu, lakini pia vimelea hao wa fangasi huvamia majani, mashina na matunda (Pods). Kwenye mbegu huwa na rangi kuanzia dhambarau iliyopauka mpaka dhambarau iliyokolea pia madoa hayo hutofatiana ukubwa kuanzia doa dogo hadi doa lenye lenye kufunika mbegu nzima. 
  • Mipasuko huonekana juu ya mbegu sehemu zenye rangi, hali husababisha ngozi ya mbegu kuwa rafu na muonekano mbaya. 
  • Endapo utapanda mbegu zenye ugonjwa basi vimelea wa fangasi wataanza kukua kutoka kwenye mbegu kwenda kwenye majani ya mche na baadae kwenye shina. 
Namna ya Kudhibiti 
  • Tumia mbegu za soya zilizothibitishwa kitaalamu na zisizokua na magonjwa. 
  • Panda aina za soya zinazohimili athari za ugonjwa huu. 
  • Epuka umwmwagiliaji wa juu (Over head irrigation), kwani huongeza kasi ya ugonjwa. 

MAVUNO 
Soya huwa tayari kuvunwa kuanzia siku 70 (miezi 2 na siku 10) hadi siku 180 (miezi 6) itategemeana na aina ya soya. Mbegu za muda mfupi hukomaa siku 70 wakati mbegu za muda muda mrefu hukomaa hadi siku 180. 

Muda gani uvune zao hili la soya inategemeana na mahitaji yako, aidha kwa matumizi ya mboga mboga (zikiwa na ubichi) au zikiwa zimekauka. Kuvuna zikiwa na ubichi hakikisha zimekomaa vyema na mbegu zikiwa zimejaa vizuri kwenye matunda (Pods). Kuvuna zikiwa zimekauka hakikisha zimekauka vyema, majani yawe yamezeeka na kubadirika rangi kuwa njano na kwa kila mmea angalau tunda moja (pod) na zaidi libadirike rangi na kuwa kahawia au nyeusi. 

Wakati wa kuvuna zikiwa zimekauka, zikate usawa wa ardhi au zivute kwa mkono kisha zikusanye kwenye turubai safi kwa ajili ya kutwangwa na kupepetwa ili kupata maharage ya soya. 

Uzalishaji wa wakulima wengi wadogo huwa ni wastani wa Kilo 500 - 1000 kwa Hekta moja (sawa na kilo 200 - 400 kwa ekari 1), kwango hiki ni sawa na Magunia 5 - 10 ya kilo 100 kwa Hekta moja (sawa na magunia 2 - 4 ya kilo 100 kwa Ekari 1). Kama utahudumia mazao yako vizuri kwa kufwata kanuni za kilimo bora, unaweza ukazalisha hadi kufikia kiasi cha Kilo 3000 kwa Hekta moja (sawa na kilo 1200 kwa Ekari 1), kiwango hiki ni sawa na Magunia 30 ya kilo 100 kwa Hekta moja (sawa na Magunia 12 ya kilo 100 kwa Ekari 1). 

NB: Hekta 1 = Ekari 2.5 

Picha: Mavuno ya soya


KUHIFADHI GHALANI 
Baada ya kuvuna, kutwanga na kupepeta ni wakati wa kuhifadhi mazao yako. Kipindi hiki ndipo wakulima wengi wanafanya makosa sana, wanahifadhi mazao yasiyokauka vizuri. Hali hii hupelekea mazao ya kuvunda au kubungua mapema hivyo kupata hasara kubwa. 

Kuepuka changamoto hii mkulima anashauriwa kukausha soya zake hadi kufikia unyevu chini ya asilimia 12%, wakulima wengi wadogo hawana vifaa vya kupima unyevu, lakini mkulima anashauriwa kutumia njia rahisi ya kuchagua mbegu kadhaa na kuzitafuna, atakaposikia sauti ya kuvunjika basi mbegu zako zimekauka vyema. Kama unatafuna mbegu na husikii sauti yoyote basi mbegu zako bado mbichi na unatakiwa uzikaushe vizuri. 

Hifadhi maharage yako ya soya mahara pasafi na pakavu kuepuka kubunguliwa. Maharage ya soya yatakayotumika kwa mbegu inatakiwa yasikae ghalani zaidi ya mwaka mmoja tangu kuvunwa na kuhifadhiwa, hii ni kwa sababu ya kupoteza uwezo wake haraka wa kuota. 


*MWISHO WA MAKALA HII*

Kama una maoni au ushauri wowote kuhusiana na makala hii, usisite kuacha ujumbe wako hapo chini, Karibu sana kwa makala zingine.

Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

Previous Post Next Post