Kilimo Bora cha Mapapai - Sehemu ya Kwanza (Growing Pawpaw - Part One)


Zao la Papai (Carica papaya) hulimwa maeneo mengi nchini Tanzania, Afrika mashariki, Afrika na Duniani kote kwenye maeneo ya kitropiki na yenye kitropiki kiasi. Zao hili lina umuhimu sana kwa afya, lina virutubisho muhimu kama; Wanga, mafuta, protini, Kalsiamu (Ca), Madini ya Chuma (Fe), Vitamini A na C. Zao hili hutumika kwa matumizi mbalimbali kama; Chakula; Kuliwa kama tunda, Kutengenezea kachumbali, juisi, jamu, jelly, jamu yenye malimao au machungwa (marmalade), Pipi n.k, Matunda mabichi huweza kuliwa kama mboga pia majani yake hutumika kama mboga.

Pia zao hili hutumika kama tiba; tunda la papai lina kemikali muhimu (alkaloid) inayoitwa Carpaine ambayo hutibu maradhi ya moyo (Heart depressant), hutibu Amiba (amoebicide), kusafisha mfumo wa mkojo (diuretic). 

Baadhi ya nchi mbalimbali duniani hutumia matunda mabichi ya papai yakiwa bado kwenye miti yao kutoa utomvu wenye kichocheo (enzyme) kinachoitwa Papain. Utomvu huu hutumika kwenye viwanda mbalimbali kama; Viwanda vya (bia, soda, juisi n.k.), vyakula na madawa ya binadamu. Pia utomvu huu hutumika kulainisha nyama, pia kwenye maandalizi ya dawa za kutibu maradhi ya mfumo wa chakula na kutibu vidonda sugu vinavyooza (gangrenous wounds). 

Vilevile utomvu huu hutumika kutibu ngozi za wanyama kwenye viwanda vya ngozi, kusafisha hariri (Silk) na kulainisha pamba.


MAZINGIRA
Zao la papai hupendelea maeneo yenye joto kuanzia nyuzi joto 21 - 33°C na mvua ya kutosha. Muinuko kutoka usawa wa bahari unaofaa kwa zao hili ni kuanzia m 0 hadi m 1600 kutoka usawa wa bahari, ingawaje zao hili hufanya vizuri kwenye muinuko chini ya m 1000 kutoka usawa wa bahari. 

Ubora na wingi wa mavuno huwa mdogo maeneo yenye muinuko mkubwa kwa sababu ya baridi inayochelewesha mmea kukua na kuiva matunda pia kupoteza ubora wa tunda. Baridi ikizidI sana mmea hufa, vilevile matunda huwa na radha nzuri endapo yatazalishwa msimu joto la wastani na mwanga wa jua wa kutosha. 

Zao hili pia huitaji mvua kiasi cha mm 1200 kwa mwaka, ili kiasi hiki cha maji kitoshe na kiweze kutumika vizuri ni vyema kuwa na mbinu mbadala za kuhifadhi maji kama; kumwaga mbolea za Samadi kuzunguka shina la mti kiasi cha debe mbili kwa shina moja. Pia matumizi ya matandazo (mulching) kama nyasi kavu zisizokua na miiba na majani ya migomba, matandazo haya hulazwa kuzunguka shina la mti, sharti yasiguse mti. Mbinu hizi mbili husaidia kutunza unyevu kwa muda mrefu. 

Hakikisha shamba lako limezungukwa na miti ya kuzuia upepo (windbreaks), upepo mkali ni hatari kwa zao hili hususani kama imepandwa kwenye ardhi yenye kichanga. 

Zao hili hupendelea udongo tifutifu usiotwamisha maji, pia uwe na rutuba ya kutosha ikiwa pamoja na uwepo wa uvundo wa mbolea za asili (Samadi na mboji). Kiasi cha tindikali ya udongo kinachohitajika ni kuazia pH 6.0 - 6.5. Mmea huu hauvumilii maeneo yanayotwamisha maji hata kama maji yatakaa kwa muda mfupi Kuna uwezekano wa miti yako kufa. 


AINA 
Kuna makundi matatu ya mapapai kulingana na jinsia au maua yao kama ifuatavyo; 

(a) Papai Jiike (pstillate) 
Hii ni aina ya papai ambayo maua yake yana sehemu ya kike (pistil) pekee. 

(b) Papai Dume (staminate) 
Hii ni aina ya papai ambayo maua yake yana sehemu ya kiume (stamen) pekee. 

(c) Papai Dume Jiike (hermaphrodite) 
Hii ni aina ya papai ambayo maua yake yana sehemu ya kike (pistil) na kiume (stamen). 

Aina hizi za papai huonyesha utofauti kipindi cha kutoa maua, matunda yanayotoka kwenye mipapai jike huwa ni matamu sana na ya mviringo kuliko yale yenye jinsia mbili (hermaphrodite) 

Mbali na makundi hayo matatu ya mapapai, zifuatazo ni baadhi ya aina za mapapai yanayopandwa sana nchini Tanzania, Afrika mashariki na duniani kote kwa ujumla; 

1. Kiru 
Aina hii hutokea nchini Tanzania huzaa matunda makubwa, pia huzalisha sana kichocheo cha papain. 

2. Honey Dew 
Aina hii hutokea nchini India, ina urefu wa kati huzaa matunda yenye ukubwa wa kati. 

3. Mountain 
Aina hii hulimwa maeneo yenye miinuko au yenye baridi (high altitudes), huzaa matunda madogo ambayo hufaa kwa jamu na kuliwa kama tunda. Vilevile jina hili hutumika kwa aina ya papai zenye umbile la kati, tamu na zenye rangi ya njano kwa ndani. 

4. Solo 
Aina hii hutokea jimbo la Hawaii nchini Marekani, huzaa matunda madogo ya mviringo na matamu. Maua yake yana sehemu ya kike na kiume (hermaphrodite) 

5. Sunrise Solo 
Aina hii hutokea jimbo la Hawaii nchini Marekani, huzaa matunda yenye ngozi laini na yenye umbile kama kibuyu pia ni matamu, yana uzito wa gramu 400 hadi 650 na huzaa sana. Ukiyapasua ndani yana rangi nyekundu iliyochangamana na njano. 

6. Sunset 
Aina hii pia hutokea jimbo la Hawaii nchini Marekani, tabia zake hufanana na "Sunrise Solo" 

7. Waimanalo 
Aina hii pia hutokea jimbo la Hawaii nchini Marekani, huzaa matunda ya mviringo yenye ngozi laini na yenye kung'aa pia wana shingo fupi. Ukiyapasua ndani yana rangi ya njano, yana ujazo na ni matamu. 


KUANDAA SHAMBA 
Hakikisha shamba lako lipo maeneo yenye miti karibu, angalau kwa kiasi fulani, hii ni kwa ajili ya kuzuia upepo mkali. Lima shamba lako vizuri kwa kina cha kutosha ili kuondoa magugu na kulainisha udongo. Vile vile shamba likilimwa vizuri husaidia kuharibu makazi ya wadudu waharibifu ikiwa ni pamoja na kuharibu mayai yao, hii huwa nzuri endapo baada ya kulimwa shamba lipigwe na jua angalau kwa wiki moja. 


KUPANDA 
Zao hili hupandwa kwa mbegu, mbegu huoteshwa kwanza kwenye kitalu / viriba halafu baadae huamishiwa shambani. Kiasi cha mbegu 3 hadi 4 hupandwa kwenye makopo au viriba. Njia nyingine, mbegu hupandwa kwenye kitalu, kitalu hiki ni vyema udongo ukatibiwa ili kupunguza uvamizi wa minyoo wadogo wanaoathiri mizizi (Nematodes) pia kupunguza athari ya ugonjwa wa fangasi unaoua miche michanga (damping-off). 

Namna ya kutibu udongo nitawaelekeza kwenye makala zangu zinazokuja. Njia nyingine ya kupunguza minyoo na ugonjwa huu kwenye kitalu ni namna ya kuandaa kitalu chako vizuri, fanya yafuatayo; 

1. Chagua eneo la kitalu lisilokua na historia ya kupandwa mazao ya mboga mboga kwa msimu huo kama maharage, soya, kunde, mbaazi n.k 

2. Lima vizuri eneo lako unalotaka kuanzisha kitalu 

3. Acha udongo wako upigwe na jua angalau kwa wiki moja. 

4. Wakati wa kuandaa kitalu changanya udongo wako vizuri na samadi iliyovunda vyema. Samadi huwa inachanganywa kiasi cha ndoo kubwa ya lita 20 kwa mita ya eneo moja (m2 1). Ukitumia Samadi isiyovunda vizuri au kutochanganya vizuri na udongo, huongeza kasi ya minyoo waharibifu (nematodes) 

NB: 
Kwa mazao yote yanayoanzia kwenye kitalu, madhaifu au magonjwa mengi huanzia kwenye kitalu, kadiri utakavyoandaa kitalu chako vizuri ndivyo jinsi utakavyopunguza magonjwa na wadudu waharibifu. 

Kitalu kikishaandaliwa mbegu hupandwa, mbegu hizo huota baada ya wiki 2 hadi 3 tangu kupandwa. Wiki ya tatu miche huwa na majani 2 - 3, miche hiyo huhamishwa kwenye makopo au viriba vikubwa kiasi cha miche 3 hadi 4 hupandwa kwenye kopo au kiriba kimoja. 

KUPANDIKIZA 
Miche huwa tayari kupandikizwa ikifikia miezi 2 tangu kupandwa, wakati huo huwa na majani 3 - 4 na hufikia urefu wa sm 20. Ni vyema miche ikapandikizwa mapema mwanzoni mwa mvua za masika zinapoanza kunyesha. Wakati wa kupandikiza hakikisha hauvurugi mizizi, pia usipandikize miche yenye umri zaidi ya miezi ya 2, kwani haikui vizuri. 

NAFASI YA KUPANDIKIZA 
Kama ilivyo kwa mazao mengine zao la papai huitaji nafasi nzuri ili kuongeza uzalishaji. Nafasi inayofaa kwa zao hili ni m 2 x m 3 (yaani mita 2 shina hadi shina na mita 3 mstari hadi mstari) au m 1.5 x m 2.5 (yaani mita 1.5 shina hadi shina na mita 2.5 mstari hadi mstari), nafasi hii ni sawa na miche 667 kwa ekari 1 / miche 1667 kwa hekta 1 (kwa nafasi ya m 2 x m 3) pia miche 1067 kwa ekari 1 / miche 2667 kwa hekta 1. 

Kwa nafasi hiyo kila shina kutakua na miche 3, ikifikia hatua ya kutoa maua, miche hii itapunguzwa na kubakiza mche mmoja wenye jinsia ya kike (female) au yenye jinsia mbili (hermaphrodite), mche wenye jinsia ya kiume huondolewa kwa sababu hautazaa matunda pia unaweza kubakiza miche michache kwa ajili ya kuchavusha. 

Japo kutambua papai jike au dume au jinsia mbili huwezekana kwa kuchunguza maua baada ya miche kukua, pia inawezekana kuitambua miche michanga kabla haijatoa maua kwa kuchunguza mizizi yake kama ifuatavyo; Papai dume: miche yake huwa na mzizi mkubwa wa katikati mrefu na mizizi midogo ya pembeni michache (long & skinny tap root and less bush roots). Papai Jike: miche yake huwa na mzizi mdogo na mfupi wa katikati na mizizi midogo mingi ya pembeni (more bushy roots & a shorter tap root).

Ifuatayo ni namna ya kuyatambua mapapai dume, jike au yenye jinsia mbili kupitia maua;

(a) Papai Dume (Maua yake marefu)


(b) Papai Jike
(Maua yake mafupi)


(c) Papai yenye Jinsia mbili



Pia kwa uchavushaji papai dume moja huweza kuchavusha mapapai jike 25 hadi 100. 

Kabla ya kupandikiza hakikisha umechimba mashimo yenye upana sm 60, urefu sm 60 na kina sm 60. Changanya udongo uliotoka shimoni na ndoo moja kubwa ya Samadi au mboji iliyooza vizuri, ongezea na mkono mmoja wa mbolea ya minjingu (Minjingu rock phosphate) na changaza vizuri. 

Baada ya hapo rudishia mchanganyiko wa udongo huo ndani ya shimo, kisha chimba kidogo katikati ya shimo halafu ondoa miche yako ndani ya kopo au kiriba kisha chomeka taratibu katikati ya shimo, jaziriza udongo kuzunguka mche (miche 2 - 3), sindilia kiasi kwa mkono kisha mwagilia maji. Pia weka matandazo ya majani makavu kuzunguka mche, hii itasaidia kuongeza joto kwenye mizizi na kupunguza upotevu wa maji (kutunza unyevu). 


KUCHANGANYA NA MAZAO MENGINE 
Zao la papai hupendelea eneo la shamba lililowazi na mwanga wa jua wa kutosha, ingawaje huweza kupandwa ndani ya shamba la nazi au inaweza kupandwa ndani ya shamba ya miembe, michungwa au milimao. Vile vile mazao ya muda mfupi huweza kupandwa ndani ya shamba mipapai kama Maharage, vitunguu, kabeji n.k. 

KUHUDUMIA SHAMBA 
Zao la papai huathiriwa sana na magugu, hakikisha unaondoa magugu mara tu yanapoonekana, pia ni vyema ukaweka matandazo kuzunguka mipapai ili kutunza unyevu na kuzuia magugu kuota. 

Kwa kipindi cha kiangazi ni vyema ukamwagilia miche yako angalau mara moja kwa wiki, hii itasaidia kuzuia mipapai kupukutisha maua yake na kuimarisha ukuaji wakati wa kiangazi. 

Papai ni zao linalokua haraka sana,hivyo huitaji kiwango kikubwa cha virutubisho. Matumizi ya samadi na matandazo kuzunguka mpapai husaidia sana kuongeza virutubisho kwenye udongo. Upungufu wa madini ya Calcium (Ca) kwenye udongo huzohofisha ukuaji wa mmea na utengenezwaji wa matunda, pia huchochea mmea kudondosha matunda. Dhibiti hali hii kwa kuweka madini ya chokaa (CaCo3) kupelekea kiwango cha tindikali (pH) kufikia 6.0.

>>> SEHEMU YA PILI

Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

Previous Post Next Post