KILIMO CHA NYANYA
SEHEMU YA 2
KUTAYARISHA SHAMBA
Matayarisho ya shamba yaanze mwezi mmoja kabla ya kupandikiza. Katua ardhi katika kina cha kutosha hadi kufikia sentimita 30. Lainisha udongo kwa kuvunja mabonge makubwa kwa kutumia jembe.
Weka mbolea za asili wiki mbili kabla ya kupandikiza. Kiasi kinachohitajika ni tani 20 kwa hekta (sawa na ndoo moja hadi mbili) kwa kila eneo la mita mraba moja. Mbolea hii iwekwe katika kila shimo la kupandia na ichanganywe vizuri pamoja na udongo.
KUPANDIKIZA
Upandikizaji wa miche shambani hufanyika hadi baada ya wiki nne hadi sita kutegemea hali ya hewa. Siku 10 hadi 14 za mwisho kabla ya kupandikiza, izoeshe miche hali ngumu ambayo inalingana na ile ya shamba la kudumu. Wakati huu ipatie miche maji kidogo na iondolee kivuli. Mwagilia kitalu siku moja kabla ili kurahisisha ung'oaji wa miche na kuepuka kukata mizizi.
Pia ni muhimu kumwagilia shamba siku moja kabla ya kupandikiza. Iwapo mbolea za asili hazikutumika wakati wa kutayarisha shamba unashauriwa kuweka mbolea ya mchanganyiko (N.P.K 5:10:5) kiasi cha gramu tano (sawa na kifuniko kimoja cha soda) kwa kila shimo wakati wa kupandikiza.
Pandikiza miche wakati wa asubuhi au jioni ili kuepuka jua kali linaloweza kunyausha miche. Wakati wa kupandikiza hakikisha mizizi haipigwi na jua, kwa kuiweka katika ndoo au chombo chochote chenye udongo wenye unyevu. Pandikiza miche katika kina cha sentimita mbili hadi tatu zaidi ya ilivyokua kwenye kitalu ili kupata mizizi mipya. Kisha shindilia udongo kiasi na vizuri kuzunguka mche na mwagilia maji.
Nafasi:
Nafasi zinazotumika kupandikiza miche shambani hutegemea aina ya nyanya, njia ya kumwagilia na hali ya hewa, kwa mfano:-
Aina fupi ya nyanya hupandikizwa kwa sentimita 50 kutoka mstari hadi mstari, na sentimita 50 kutoka mche hadi mche. Aina hii haihitaji kuegeshwa kwenye miti.
Aina ndefu ya nyanya inayohitaji kuegeshwa kwenye mti hupandikizwa katika nafasi ifuatayo:- Kutoka mstari hadi mstari sentimita 60 na mche hadi mche ni sentimita 50.
KUTUNZA SHAMBA
Kuweka Matandazo
Baada ya kuhamishia miche shambani, weka matandazo ili kuhifadhi unyevu na kuzuia magugu. Matandazo pia husaidia mmomonyoko wa udongo na kutunza rutuba. Vilevile hupunguza uzito wa matone ya mvua na kuweka matunda katika hali ya usafi.
Kusimika Miti na Kuegesha Mimea
Kazi ya kusimika miti na kuegesha mimea hufanyika wiki ya pili baada ya kupandikiza. Miti ya kuegesha mimea iwe imara, na ambayo haiozi haraka. Simika miti kiasi cha umbali wa sentimita tano kutoka kwenye mmea. Wakati wa kusimika mti hakikisha kwamba mmea unakuwa upande wa ndani ili kuzuia mmea usiumie wakati wa kuchuma au kunyunyiza dawa. Kisha kwa kutumia mkono shindilia mti sentimita 20 hadi 50 kwenda chini ya ardhi. Mti uwe na urefu wa mita moja na nusu hadi mbili na unene wa sentimita mbili hadi tatu.
Kufunga Nyanya Kwenye Mti
Aina ndefu ya nyanya ni lazima ifungiwe kwenye mti ili kuzuia mmea usitambae chini. Mimea iliyofungwa kwenye mti hurahisisha unyunyiziaji wa dawa, umwagiliaji na uchumaji wa matunda. Ili kupata mazao yaliyo bora na makubwa ondoa matawi yote na kuacha mashina mawili. Yafungie mashina hayo kwenye mti ili mimea iweze kutambaa na kuwa wima. Funga kamba katika umbo la nane chini ya kila jani la tatu na Kila baada ya sentimita 20 hadi 25.
Kupunguza Matawi
Kupunguza matawi ni muhimu na hasa kwa aina ndefu kama vile Money Maker. Kazi hii hufanyika mara moja kwa wiki. Wakati mzuri wa kupunguzia ni asubuhi. Ondoa matawi yote na acha shina moja au mawili. Usitumie kisu kupunguza matawi bali matawi yavunjwe kwa kutumia mkono. Utumiaji wa kisu hueneza magonjwa yanayosababishwa na virusi na bacteria.
Kuondoa Majani
Ondoa majani yote yanayoonyesha dalili za magonjwa au kushambuliwa na wadudu na yale yote yaliyozeeka ili kupunguza hali ya unyevu na kuruhusu hewa ya kutosha kwa mimea. Ondoa majani mawili au matatu yaliyo chini ya ngazi ya kwanza ya matunda kisha yachome au yafukie.
Kukata Kilele
Kwa kawaida aina ndefu ya nyanya huzaa ngazi zaidi ya sita za matunda, lakini mmea una uwezo wa kubeba ngazi tano hadi sita tu. Hivyo ni muhimu kukata sehemu ya juu ya mmea (kilele) ili kusimamisha ukuaji wake. Kata kilele mimea ifikiapo ngazi hizo. Jani moja liachwe juu ya ngazi ya mwisho (ya tano au ya sita).
Machipukizi yote yanayojitokeza pembeni hayana budi kuondolewa ili kupata matunda makubwa na yatakayoiva upesi.
Palizi
Palizi katika shamba la nyanya ifanywe kwa uangalifu ili kuepuka kukata mizizi. Punguza palizi ya mara kwa mara kwa kuweka matandazo kuzuia uotaji wa magugu. Wakati wa kupalilia, pandishia udongo kwenye shina.
Kumwagilia
Kwa kawaida nyanya hutoa mavuno mengi wakati wa kiangazi kuliko wakati wa masika. Mwagilia maji ya kutosha mara mbili kwa wiki hasa matunda ya kwanza yanapoanza kutunga. Kumwagilia maji mengi sana au kidogo sana kunasababisha matunda yawe na hitilafu na kupasuka. Wakati wa mwanzo epuka kumwagilia maji mengi ili mimea isididimie.
Kuweka Mbolea ya Kukuzia
Mbolea ya kukuzia huwekwa mara mbili. Mara ya kwanza weka gramu tano za S/A au CAN kwa kila mche katika wiki ya pili hadi ya nne baada ya kupandikiza. Rudia tena kuweka kiasi hicho hicho wakati matunda ya ngazi ya kwanza yanapoanza kuiva.
Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo
Post a Comment