KILIMO CHA NYANYA
SEHEMU YA KWANZA
Nchini Tanzania zao la nyanya hulimwa katika mikoa yote. Nyanya hutupatia vitamini A, B, na C. Vile vile zina madini aina ya chuma na chokaa.
MAZINGIRA
Nyanya hustawi katika udongo wa aina nyingi ilimradi uwe mwepesi na usiotwamisha maji. Udongo unaofaa zaidi ni ule wa kitifutifu na wenye mboji nyingi. Hali kadhalika udongo wenye uchachu wa wastani ni mzuri kwa kilimo cha zao hili.
Joto lifaalo kwa ustawishaji wa nyanya ni kutoka nyuzi joto 18 hadi 30 za Sentigredi (18 - 30 °C). Joto likizidi husababisha matawi ya matunda kuwa machache. Vilevile joto jingi, mwanga kidogo, pamoja na hali ya unyevuunyevu husababisha magonjwa mengi kuenea na mmea kuwa na majani mengi na matunda kidogo. Joto kidogo hufanya mimea kutoa matawi mengi na matunda madogo ambayo huchelewa kukomaa.
Zao hili hupendelea mvua za wastani pamoja na kipindi kirefu cha jua. Hali ya mvua nyingi pamoja na baridi kali husababisha kuenea kwa magonjwa na wadudu waharibifu.
AINA
Aina nzuri za nyanya ni zile zinazotoa mavuno mengi na bora, zinazostahimili magonjwa, zinazokomaa mapema, zenye ladha nzuri na umbo la kuvutia. Zifuatazo ni aina bora za nyanya zinazolimwa hapa nchini, Aina hizi zimegawanyika katika makundi mawili kutegemea ukuaji wake;
(a) Aina fupi:
Dwarf germ, Cal - J, Amateur, Red Cloud, Roma, Reza na Columbian.
(b) Aina ndefu:
Money Maker, Marglobe, Beef Master, Mandel, Tengeru 97 na Tanya.
KUOTESHA MBEGU
Mbegu za nyanya huoteshwa kwanza kwenye kitalu na baadaye kuhamishiwa shambani. Matayarisho ya kitalu hufanyika wiki moja au mbili kabla ya kupanda mbegu. Tengeneza tuta lenye upana mita moja na urefu wowote. Vunja mabonge makubwa kwa kutumia jembe. Weka mbolea za asili zilizooza vizuri kiasi cha ndoo moja hadi mbili katika eneo la mita mraba moja. Changanya mbolea hii na udongo vizuri. Sawazisha kwa kutumia reki au kifaa chochote.
Mwagilia kitalu siku moja kabla ya kupanda, kisha sia mbegu katika mistari yenye nafasi ya sentimita 10 hadi 15 kutoka mstari hadi mstari. Kiasi cha mbegu kitakachotosha eneo hilo la mita mraba moja ni gramu tatu hadi tano (sawa na nusu kijijo cha chai mpaka kijiko kimoja). Kiasi hiki cha mbegu huweza kutoa miche inayoweza kutosha kupandikiza katika eneo la mita mraba 100. Kiasi cha mbegu kinachohitajika kwa hekta moja nu gramu 300 hadi 500.
Weka matandazo kama vile nyasi kavu na majani ya migomba kisha mwagilia maji asubuhi na jioni mpaka mbegu zitakapoota. Mbegu huota baada ya siku tano hadi 10. Ondoa nyasi mara baada ya mbegu kuota na endelea kumwagilia hadi miche itakapohamishwa. Jenga kichanja ili kuzuia jua kali na matone ya mvua yanayoweza kuharibu miche michanga.
Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo
Post a Comment