Mara nyingi matatizo madogo madogo
yanayohusiana na lishe huwakumba wajawazito wengi wakati wote wa ujauzito wao
au baadhi tu ya vipindi, itategemeana hali ya mjamzito mwenyewe. Matatizo hayo
madogo madogo ni pamoja na; Kichefuchefu na kutapika, Kutoa haja ngumu,
Kiungulia, na kupenda au kutopenda baadhi ya vyakula.
Ufuatao ni mchanganuo wa matatizo
haya madogomadogo na namna ya kukabiliana nayo;
1. Kichefuchefu na Kutapika
Baadhi ya wajawazito huwa na
kichefuchefu na kutapika sana wakati wakiwa na mimba changa hususani kipindi
cha asubuhi wanapoamka au wakati mwingine.
Namna ya kudhibiti hali hii
- Kula vyakula vikavu kama mikate ya ngano, wali mkavu n.k
- Kula chakula kidogo na mara nyingi kwa siku (Frequent meals).
- Epuka kula vyakula venye harufu mbaya na ya kukera.
2. Kutoa haja kubwa ngumu
Hali ya kutoa haja kubwa ngumu huwakumba wajawazito wengi, hali
hii huchangiwa na mabadiliko ya homoni na mtoto anavyoongezeka kukua huongeza
mgandamizo juu ya utumbo wa mama hali inayopelekea mjamzito kupata haja ngumu.
Namna ya kudhibiti hali hii
- Fanya mabadiliko kidogo kwenye chakula chako; Kula vyakula vyenye nyuzinyuzi nyingi kama Ugali wa dona, Mbogamboga na Matunda.
- Kunywa maji mengi kiasi cha Lita mbili au vikombe nane kwa siku.
- Fanya mazoezi madogo madogo wa kiasi kama kutembea kwa mguu umbali fulani.
- Usithubutu kutumia dawa yoyote ile ya kuondoa hali hii pasipo kumuona daktari.
3. Kiungulia na kujaa gesi
tumboni
Wakati mimba ikiwa changa mjamzito hukumbana na adha ya
tumbo lake kujaa gesi baada ya kula au Kubeua (Kutoa gesi iliyopo tunboni
kupitia mdomo) mara nyingi. Vilevile mjamzito hupata shida ya kiungulia. Hali
hii huwa mara nyingi haisababishwi na chakula ulichokula bali ni kutokana na
mabadiliko ya homoni za mwili pamoja kuongezeka kwa mgandamizo kwenye tumbo la
chakula la mama inayotokana kukua na kuongezeka kwa mtoto.
Namna ya kudhibiti hali hii
- Tulia na kula taratibu
- Tafuna chakula chako taratibu
- Kula kiasi kidogo cha chakula na kwa mara nyingi
- Kunywa kinywaji wakati wa kula
- Epuka kula vyakula vyenye mafuta au vilivyokaangwa na vigumu kumeng'enywa husababisha gesi na kiungulia.
- Usilale chali, lala kwa ubavu aidha wa kushoto au wa kulia. Kulala chali nako kunapelekea kupata kiungulia
- Baada ya kula chakula subiri saa moja ndipo ulale.Kama unataka ufanye mazoezi, baada ya kula subiri masaa mawili ndipo ufanye mazoezi.
NB:
*Kufahamu Lishe bora kwa wajawazito Bofya hapa
*Kufahamu Mambo yasiyopaswa kufanya wakati wa ujauzito Bofya hapa
Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo
Post a Comment