Ufugaji wa Kuku wa Mayai - Sehemu ya Tano (Layer Poultry Farming - Part Five)


SEHEMU YA TANO

NAMNA YA KUTENGENEZA CHAKULA CHA KUKU WA MAYAI
Kutengeneza chakula cha kuku wa mayai, si jambo la mzaha mzaha, kwamba unachanganya changanya tu hovyo hovyo, inakupasa uwe makini sana kuhakikisha unaweka virutubisho vyote vinavyofaa kwa kuku wa umri husika. Kama utaona huwezi kukidhi vigezo vya kutengeneza vyakula hivi, basi unaweza ukanunua kwenye makampuni mbalimbali yanayotengeneza vyakula hivi kwa kuzingatia ubora na yanayopatikana ulimwenguni kote. KUFAHAMU NAMNA YA KUTENGENEZA CHAKULA CHA KUKU WA MAYAI NA WA NYAMA BOFYA VIUNGANISHI HIVI; SEHEMU YA KWANZA, SEHEMU YA PILI NA SEHEMU YA TATU

KUWAPATIA MAJI YA KUNYWA
Afya bora ya kuku hutegemea sana jinsi unavyowapa maji safi na salama. Inatakiwa uwapatie kuku wako maji ya kutosha kulingana na uhitaji. Pia yatibu maji ya kunywa ya kuku ili kuua bacteria wa kwenye maji kwa kutumia dawa ya Klolini  (Chlorine) au Bliching powder. Chagua sehemu nzuri ya kuweka chombo cha maji ya kunywa ndani ya banda la kuku. Wapatie maji ya baridi wakati wa joto kali na wapatie maji ya vuguvugu wakati wa baridi kali.

NB:
Ukifwata maelekezo yote ya hapo juu kwa uangalifu, utaiona faida kubwa ya kufuga kuku wa mayai.

HUDUMA ZINGINE MUHIMU KWA KUKU WA MAYAI
Yafwatayo ni mambo mengine muhimu yanayopaswa kufanya ili kuboresha ongezeko la uzalishaji wa mayai.
  • Hakikisha banda lako la kuku linakua na hewa ya kutosha na mwanga.
  • Kuku mmoja wa mayai anahitaji wastani wa gramu 120 (Kilo 0.12) za chakula kwa siku.
  • Weka vyombo vya chakula na maji vya kutosha, Wastani wa kuku 50 wanatosha kwa chombo kimoja cha chakula au cha maji. Kwa mfano kama una kuku 200, utaweka vyombo vya maji vinne (4) na vyombo vya chakula vinne (4).
  • Wapatie kuku wako kiasi kidogo cha mchanga laini wakifikia wiki 20 (muda wa kuanza kutaga mayai). Mchanga husaidia kuongeza kasi ya mmeng'enyo wa chakula.
  • Weka viboksi au sehemu za kutagia maeneo yenye giza, kusanya mayai mara tatu kwa siku. Kiboksi au sehemu moja ya kutagia  hutosha kuku watano (5).
  • Wawekee matandazo masafi Juu ya sakafu kama maranda ya mbao au mapumba ya mpunga ili kuleta joto na kupunguza unyevu utokanao na kinyesi.
  • Wapatie mboga za majani kuku wako mara kwa mara ili kuwaongezea vitamini, njia nzuri ya kuwapa ni kufunga mafungu ya mbonga madogo madogo na kuyaning'iniza kwa kamba, kuku watakua wanakula kwa kuyadonoa yakiwa juu. Usifunge mafungu hayo ya mboga umbali mrefu kuzidi kimo chao, funga usawa wa kimo chao.
  • Weka vitamini kwenye maji yao ya kunywa.
  • Wakate midomo kuku wako wakiwa na umri wa wiki 12 (wiki 8 kabla ya kuanza kutaga, kuku wa mayai huanza kutaga wakiwa na wiki 20). Usiwakate midomo wakati wameanza kutaga, utawapa mshtuko na utapunguza kasi ya kutaga mayai.
  • Kuku wa mayai wakishazeeka (Kuanzia umri wa wiki 50 na kuendelea) hupunguza kiwango cha kutaga mayai, kwa hiyo wakati huu unatakiwa kuwaondoa kuku wote bandani kama kiwango cha kutaga mayai kimeshuka chini ya asilimia 40%.
NB:
Kuku wa mayai wakifikia umri wa wiki 20, asilimia 5% ya kuku huanza kutaga. Umri wa wiki 21, asilimia 10% kuku huanza kutaga. Wakifikia umri wa wiki 26 hadi 30 hutaga mayai sana, ingawaje inaweza ikawa tofauti kutokana na aina ya kuku.

  • Baada ya kuku hawa kutaga mayai sana (umri wa wiki 26 hadi 30), husimama kutaga mayai kwa siku chache, Baada ya siku chache hizo kupita uzalishaji wa mayai hupungua taratibu.
  • Baadae Kiwango cha kutaga mayai na ukubwa wa mayai huongezeka taratibu.
  • Kuku wataendelea kukua mpaka watakapofikia umri wa wiki 40. Uzito na ukubwa wa mayai huongezeka hadi kuku wakifikia umri wa wiki 50.

NAMNA YA KUTAMBUA TABIA ZA KUKU WANAOTAGA VIZURI
  • Angalia kuku wenye upanga wenye rangi nyekundu mpauko kichwani (Comb) na kidevu chenye rangi nyekundu mpauko (Wattles)
  • Kuku wanaotaga vizuri wanakua na macho angavu
  • Upana katikati ya nyonga unatakiwa uwe angalau upana wa vidole viwili vya mkononi au zaidi, upana huu hutosha sana kwa mayai kupita.
  • Midomo ya kuku na makucha ya miguuni huwa na rangi mpauko (bleached)
  • Sehemu ya nyuma ya kuku (sehemu ya hajakubwa) lazima iwe na unyevu unyevu wakati wote kuwezesha mayai kuteleza kwa urahisi wakati yanatoka.

NAMNA YA KUTUNZA MAYAI VIZURI
  • Tunza mayai mbali na joto hususani jikoni wanakotumia kuni au mkaa, kwa sababu kutakua na joto litakaloathiri mayai. Joto hilo linaharibu kiini cha yai kwa kutengeneza mazingira ya kutotoresha, hali hii huharibu kiini cha yai na kukiua kabisa hususani kwa mayai yaliyorutubishwa na jogoo. Pia kwa mayai haya ya kuku wa mayai ambayo hayajarutubishwa na jogoo hupaswi kuyatunza sehemu zenye joto jingi, kwani ubora wake utaharibika.
  • Tunza mayai yako kwa kuweka sehemu nyembamba ya yai kutizama chini na sehemu pana kutizama juu, ndio maana trei zote za mayai zina mfumo huo, zina sehemu iliyochongoka, ina maana kwamba sehemu nyembamba ya yai ndio inapaswa ianze.
  • Safisha mayai yaliyochafuka kwa kutumia kitambaa laini na kikavu, chonde chonde usioshe mayai kwa kutumia maji.
  • Usitunze mayai yako juu ya kabati ambapo joto la dari linaweza kuathiri mayai na kuyaharibu. Tunza mayai yako chini ya sakafu na unaweza ukapanga trei zako hadi kufikia kimo cha urefu wako, ili kuhusu hewa sehemu ya juu kupenya kwa urahisi.
  • Tunza mayai yako sehemu yenye ubaridi kiasi (sawa na Joto la ndani ya nyumba, Room temperature) na pawe na usalama.

KUMBUKUMBU MUHIMU ZINAZOTAKIWA KUREKODIWA NA KUHIFADHIWA
  • Kufahamu gharama ya kuanzisha mradi wako kuanzia banda, kuku, chakula, madawa, vifaa n.k hii itakusaidia kujua kama unapata faida au lah.
  • Takwimu za uzalishaji wa mayai kama Idadi ya mayai yaliyozalishwa kwa siku, kwa wiki, kwa mwezi, kwa robo mwaka na kwa mwaka.
  • Kiasi cha chakula kilichotumika kwa siku, kwa wiki, kwa mwezi, kwa robo mwaka na kwa mwaka.
  • Idadi ya kuku wako
  • Idadi ya vifaa ulivyonavyo (vizima na vibovu), hii itakusaidia kufanya ukarabati wa vifaa hivyo au kununua vipya.
  • Takwimu za matibabu ya kuku kama aina ya dawa zilizotumika, idadi ya kuku waliopatiwa tiba, waliopona, walio bado wagonjwa n.k
  • Takwimu za Idadi ya vifo vya kuku vilivyotokea kama ni vya ghafra na vinavyohusisha kuku wengi kwa mkupuo au vifo vinavyohusisha kuku mmoja mmoja.
  • Takwimu za magonjwa mbalimbali yanayowakumba kuku wako.
  • Takwimu za muda wa kuwapatia kuku wako dawa maalumu zinazotolewa kila baada muda fulani, kwa mfano dawa za minyoo na chanjo.
  • Takwimu za mauzo ya mayai, kwa siku, kwa wiki, kwa mwezi, kwa robo mwaka na kwa mwaka. Hii itakusaidia kujua kama unapata faida au lah baada ya kutoa gharama za kuanzisha na kuendeleza mradi.

*MWISHO WA MAKALA HII*

Kama una maswali, maoni au ushauri kuhusiana makala hii, usisite kutuachia maelezo yako hapo chini, Karibu sana! 

Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

Previous Post Next Post