Kilimo bora cha Karanga - Sehemu ya Sita (Growing Groundnuts - Part Six)


SEHEMU YA SITA

4. Aspergillus crown rot (Aspergillus niger) /Kuoza mbegu au miche
Ugonjwa huu husababishwa na vimelea vya fangasi aina ya Aspergillus niger, vimelea hivi huambatana na vimelea vingine vya fangasi aina ya Aspergillus flavus.


Picha: Kuoza mbegu au miche          Photo Credit: www.semanticscholar.org

Athari/Dalili
  • Vimelea hivi husababisha mbegu na miche ya karanga kuoza, Ardhi ikiwa na unyevu na pakiwa na vimelea hivi basi mbegu iliyopo ardhini huvamiwa na kufa kutokana na kuoza.
  • Mbegu iliyooza ikitolewa ardhini huonyesha kufunikwa na masizi meusi.
  • Maeneo kuzunguka miche ikiyoathirika hufunikwa na vitu vyenye rangi nyeusi (Black fungal spores).
  • Vilevile ugonjwa huu huathiri mimea mikubwa, baadhi ya matawi ya mmea au mmea mzima hunyauka. Matawi yaliyonyauka huondoshwa kirahisi kwenye mashina.
  • Matunda ya karanga yaliyoathirika huonyesha vitu vyeusi mithiri ya masizi. Kimelea kingine jamii ya Aspergillus flavus husababisha kuharibika kwa mbegu zikiwa ardhini.
  • Kimelea hiki aina ya Aspergillus flavus, kikivamia mbegu hutengeneza sumu inayoitwa Aflatoxin (Sumu kuvu) ambayo husababisha vifo au ugonjwa unaotokana na sumu hiyo baada ya kuliwa na binadamu au wanyama.
  • Kimelea hiki aina ya Aspergillus flavus hutengeneza sumu kuvu (Aflatoxin), na mara nyingi hutokea sana wakati wa kuhifadhi karanga stoo kuliko wakati wa ukuaji shambani.
Namna ya kudhibiti
  • Epuka kuongeza kiwango cha unyevu kupita kiasi shambani, hii itasaidia kupunguza athari ya vimelea hawa.
  • Ukishavuna karanga zako hakikisha unazikausha vizuri juani hadi kufikia unyevu wa asilimia 10%, hii itasaidia kuepusha kuvamiwa na Sumu kuvu (Aflatoxin).
  • Vuna karanga zako kwa uangalifu kuepusha kuzipasua, kwani vimelea hivi huweza kupenyeza ndani ya gamba la karanga.
  • Ng'oa mimea yote iliyoathirika na uichome moto, hii itasaidia kupunguza vyanzo vya vimelea hawa.

5. Bacterial wilt (Ralstonia solanacearum) /Mnyauko bakteria
Ugonjwa huu husababishwa na bakteria aina ya Ralstonia solanacearum, huukumba mmea mzima. Ugonjwa huu husababisha hasara kubwa ya mazao endapo kama ugonjwa utaanza mapema.

Picha: Karanga zenye ugonjwa na zisizokua na ugonjwa

Athari/Dalili
Mmea huonyesha dalili za kukosa maji na hunyauka haraka pasipo kubadirika rangi ya majani kuwa njano hususani katika kipindi ambacho joto ridi huwa kubwa. Mmea mzima hunyauka ukiwa na rangi yake ya kijani.

Namna ya kudhibiti
Epuka kupanda karanga kwa misimu kadhaa mfululizo, bali Badirisha mazao kwa kupanda mazao mengine tofauti na karanga kama mazao jamii ya nafaka kama Mahindi, mtama ulezi n.k.


6. Groundnut rosette disease
Huu ni ugonjwa unaosababishwa na virusi, virusi hawa husababisha aina tatu za ugonjwa huu ambazo nazitaja kwa majina ya kitalamu nayo ni; Chlorotic rosette, Groundnut green rosette na Groundnut mosaic. Virusi hawa husambazwa na wadudu wanaoitwa Vidukari mafuta (Aphids)

Photo Credit: www.infonet-biovision.org shared under Creative Commons License (CC BY)

Athari/Dalili
  • Majani ya karanga huwa rangi njano,  pia huwa na madoamadoa yenye rangi tofauti, na mistari iliyojichora (Mosaic symptoms)
  • Mmea hudumaa na matawi huaribika.
  • Majani yaliyokomaa huwa na rangi ya kijani iliyochangamana na weusi, pia majani hupungua ukubwa na hujikunja kuelekea chini. Kama mmea umeathiriwa tangu ukiwa mdogo unaweza usitengeneze karanga.
Namna ya kudhibiti
  • Panda karanga zako mapema wakati wa mvua na kwa nafasi iliyokaribiana kiasi.
  • Panda aina ya mbegu inayohimili ugonjwa huu
  • Mimea yote iliyoathirika ingo'oe na ichome moto.

Picha: Shamba la karanga lililotunzwa vizuri

MAVUNO
Karanga huwa tayari kwa mavuno baada ya siku 85 hadi 130 tangu kupanda, itategemeana na aina ya mbegu. Kwa mbegu zinazoota sehemu moja (Bunch cultivars) hukomaa kuanzia siku 85 hadi 100 na kwa mbegu zinazotambaa (Runner cultivars) hukomaa kuanzia siku 110 hadi 130 tangu kupanda.

Kabla ya kuanza kuvuna ni vyema ukajirizisha kama karanga zako zimekomaa vizuri kwa kuchimba shina moja halafu chunguza ukomavu wake. Karanga zilizokomaa vizuri huwa na sifa zifuatazo;

1. Gamba la karanga huwa gumu, kavu na lenye rangi ya Kahawia (Brown)
2. Ukibangua karanga mbegu za ndani huwa na rangi ya kijivu.
3. Ukitikisa karanga zenye mbegu ndani utasikia sauti ya mtikisiko.


Picha: Karanga zilizokauka vizuri

Hakikisha unachimba vizuri karanga wakati wa kuvuna ili kuepusha kuzitoboa na kuziacha zingine kwenye udongo, vuna zikiwa na mashina yake. Ukishavuna zikaushe siku 2 hadi 3 kisha zitoe kwenye mashina halafu tena kausha karanga zenyewe siku 7 hadi 10 hadi zifikie unyevu wa asilimia 10%.

Picha: Kuvuna karanga

Bangua karanga kwa mkono au kwa kutumia mashine, karanga zilizovunjika au chafu ziondoe ili kubakiza karanga zenye ubora. Hakikisha karanga zako zimekauka vizuri ili kuepusha karanga kuvunda au kuoza na kupata sumu kuvu (Aflatoxin). Sumu kuvu hii ni kemikali ambazo ni hatari kwa afya ya binafamu na wanyama, na huathiri Ini. Karanga zitakazotumika kama mbegu kwa msimu ujao, inatakiwa zisibanguliwe, zibanguliwe wakati msimu wa kupanda umefika.

Tunza karanga zako vizuri baada ya kuzikausha kwani zikichangamana na uchafu au uvundo, hutengeneza sumu kuvu (Aflatoxin).

Kama mazingira ya kuvuna yana unyevu, Sumu kuvu (Aflatoxin) hujitengeneza kwenye mbegu za karanga ambayo ni hatari kwa afya ya wanyama na binadamu, husabanisha ugonjwa wa ini.

Kama shamba lako utalitunza vizuri utaweza kuvuna mpaka Tani 1.6/Ekari (Tani 4/Hekta).


*MWISHO WA MAKALA HII*

Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

Previous Post Next Post