SEHEMU YA KWANZA
Zao la Muhogo (Cassava) hulimwa
sana nchini Tanzania, afrika mashariki, Afrika na Duniani kwa ujumla hususani
kwa maeneo ya pwani ya Bahari au Maziwa mbalimbali.
Zao hili ni muhimu sana kwa
matumizi ya chakula pia humfaa mkulima mdogo mdogo kwa sababu huitaji utaalamu
kidogo wa uzalishaji pamoja pembejeo kidogo.
Pia zao hili huvumilia ukame,
linaweza kutoa mavuno yanayorizisha hata kama kukiwa na ukame sana. Pia umuhimu
wake mwingine ni kwamba, mihogo inaweza kukaa kwenye udongo miezi kadhaa bila
kuharibika, hivyo inaweza kutumika kama akiba ya chakula wakati wa njaa.
MAZINGIRA
Zao la muhogo hupendelea maeneo
yenye hali ya joto, ndio maana maeneo ya pwani ya bahari au maziwa hufaa sana
kwa zao hili. Zao hili hustawi vema kwenye muinuko wa ardhi kuanzia mita 0 hadi
1500 kutoka usawa wa bahari.
Hali ya joto linalohitajika kwa
zao hili ni nyuzi joto 20°C
hadi 30°C. Zao hili hufanya
vizuri kwenye maeneo yenye mvua kiasi cha mm 500 hadi 6000 kwa mwaka. Kiwango
mahsusi cha mvua kinachohitajika ni mm 1000 hadi 1500 kwa mwaka ila pasiwepo na
ukame sana kwa wakati huo.
Zao la muhogo hupendelea udongo
tifutifu wenye kichanga (Sandy loams). Zao hili huweza kutoa mavuno hata kwenye
udongo ulioathiriwa na mmomonyoko wa udongo ambapo mazao mengine hayakukubali.
Hivyo udongo wenye changalawe au kokoto haufai kwa zao hili, pia udongo
usiopitisha na unaotwamisha maji kama mfinyanzi nao haufai.
Pia zao hili hupendelea udongo wenye tindikali kiasi cha pH
5.5 hadi 7.5, kiwango kikishuka chini ya pH 5.5 huo udongo haufai kwani kunakua
na Asidi nyingi. Pia kiwango kikiongezeka zaidi ya pH 7.5 huo udongo haufai
kwani kunakua na bezi nyingi (Alkaline). Kiwango cha tindikali kikipungua au
kikiongezeka zaidi ya pH 5.5 - 7.5, basi zao la muhogo hudumaa na kupunguza
uzalishaji. Vilevile zao la muhogo halifai kwenye udongo wenye Rutuba sana
kwani litatoa majani mengi kuliko matunda ya muhogo.
AINA
Kuna aina mbalimbali za muhogo zinazopandwa nchini Tanzania.
Wakulima wengi hupanda mbegu za kienyeji, siku zijazo nitakuletea mbegu bora za
muhogo zilizofanyiwa utafiti nchini Tanzania.
KUANDAA SHAMBA
Kabla ya kuandaa shamba hakikisha eneo lako linakidhi vigezo
vya kilimo hiki kama ifuatavyo;
- Eneo la kupanda muhogo liwe sehemu tambalale au lenye mteremko kiasi (Gently sloping land). Maeneo yenye mtelemko mkali (Steep slopes) hayafai kwa sababu ni rahisi kutokea mmomonyoko wa udongo.
- Maeneo ya mabonde hayafai kwa kilimo hiki kwani maeneo haya hutunza maji hivyo hali ya kuwepo kwa maji husababisha mizizi ya mihogo kutokukua vema.
- Pia ni vyema kupata historia ya shamba kama; aina ya mazao yaliyopandwa msimu uliopita, magonjwa na wadudu waliokuwepo n.k. Hii ina maana kwamba shamba lilopandwa muhogo kwa misimu kadhaa mfululizo halifai kupanda tena muhogo kwa sababu magonjwa na wadudu walewale wa muhogo wataendelea kuongezeka. Badirisha mazao, ingawaje zao la muhogo linaweza kupandwa kwa misimu kadhaa mfululizo kwenye eneo moja pasipo kupunguza uzalishaji, tofauti na mazao mengine. Ili kuongeza uzalishaji inampasa mkulima kubadilisha mazao kwa kupanda mazao mengine tofauti na muhogo au mazao mengine jamii ya mizizi kama; maharage, kunde, mazao ya nafaka n.k
Baada ya kupata eneo zuri
linalofaa, lima vizuri shamba lako kwa kina cha kutosha. Zao la muhogo hupandwa
kwa kawaida au kwenye matuta. Kupanda kwenye matuta kunafaa sana kwenye maeneo
yenye mvua nyingi kuanzia mm 1200 na kuendelea kwa mwaka.
Kupanda kwa matuta hakutoi mavuno
mengi tofauti na kupanda kawaida, ingawaje kupanda kwa matuta husaidia sana kwa
maeneo yenye miteremko ili kuzuia mmomonyoko wa udongo.
KUPANDA
Zao la muhogo hupandwa kwa kutumia
mashina ya mmea wa muhogo uliokomaa kwa kukata vipande vipande vyenye urefu wa
sm 20 - 30 na kipenyo cha mm 20 - 25. Panda vipande vyako mwanzoni mwa mvua za
kwanza.
A: Kuandaa vipande vya mashina
Vipande hivyo vya kupanda lazima
viwe na macho au mafundo 5 hadi 8, pia vipande hivyo lazima vitoke kwenye mmea
wa muhogo wenye afya na wenye umri wa miezi 8 hadi 14.
"Cutting cassava stems into mini-stems prior planting" flickr photo by IITA Image Library shared under a Creative Commons (BY-NC) license
Picha: Kuandaa vipande vya kupandia
Vipande hivyo inatakiwa viwe
vimekomaa na vimetoka sehemu ya katikati ya shina, sehemu iliyokomaa hutoa
mavuno mengi kuliko sehemu yenye mashina machanga. Vilevile mashina malefu ya
kupandia hutoa mavuno mengi kuliko mashina mafupi.
Vitibu vipande hivyo vya mashina
kwa maji ya vugu vugu, ili kuua na kutibu magonjwa mbalimbali yaliyopo kwenye
mashina. Kinachofanyika vipande hivi vya mashina hudumbukizwa kwenye maji ya
vugu vugu kwa dakika 5 hadi 10. Namna ya kuandaa maji hayo ya vugu vugu;
Changanya maji ya moto yaliyochemka na maji ya baridi kwa uwiano wa 1:1, yaani
kama umechemsha maji ya moto kiasi cha ndoo moja ya lita 10 basi uchanganye na
maji ya baridi kiasi kicho hicho cha lita 10.
Inatakiwa vipande hivyo vya
mashina vipandwe haraka iwezekanavyo mara tu baada ya kuandaliwa, ili kuepusha
kuharibika kabla ya kupandwa.
Photo Credit: IITA genebank Website: www.cropgenebank.sgrp.cgiar.org
B: Kupanda
Mihogo hupandwa kwa nafasi ya mita
1 shina hadi shina na mita 1 mstari hadi mstari (mita 1 x mita 1), ina maana kutakua na
vipande 10000 kwa hekta 1 au vipande 4000 kwa ekari moja.
Vipande vya mashina ya muhogo
hupandwa kwa wima au kwa kuchegama (at an angle), wakati wa kupanda hakikisha
macho ya vipande hivyo (buds) yameangalia juu. Ina maana usigeuze vipande hivyo
kuwa juu - chini kwani kutakua na uzalishaji mdogo wa mihogo.
Upandaji wa wima au kuchegama
hutegemea aina ya udongo na hali ya unyevu wa udongo, kwa mfano ukipanda
vipande vyako wakati wa kiangazi au masika inatakiwa uvichomeke ardhini kwa
kuchegama (at an angle) na sehemu kubwa ya macho iwe ardhini na ufukie udongo
vizuri. Kama ni udongo wa kichanga inatakiwa vipande hivyo vipandwe wima, hii
itasaidia mmea kuwa na mizizi mirefu.
NB:
Haitakiwi upande vipande vyako kwa ulalo (Horizontal), kwa sababu kutazaliwa mashina mengi na mizizi itakua juu juu, hali itakayopelekea urahisi wa kuharibiwa na panya au ndege.
Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo
Post a Comment