Kilimo bora cha Mihogo - Sehemu ya Pili (Growing Cassava - Part Two)


SEHEMU YA PILI

USAFI WA SHAMBA
Kufanya palizi ni muhimu sana kwa mazao yote ikiwemo zao la muhogo. Ni muhimu kufanya palizi angalau kila baada ya wiki 3 hadi 4 hadi kufikia miezi 2 hadi 3 baada ya kupanda. Baada ya miezi 3 toka kupanda majani ya muhogo yanakua yamekua sana na kufunika shamba, hivyo kupunguza kasi ya kuota majani, muda huo palizi haina umuhimu sana.

MATUMIZI YA MBOLEA
Ingawa zao la muhogo hufanya vizuri hata kwenye udongo wenye rutuba kidogo, Inahitajika mbolea ya kutosha ili kuleta mavuno mengi. Ili kupata mavuno mengi ni muhimu kuhakikisha kuna mbolea ya kutosha kwenye udongo.

Kirutubisho cha Fosforasi (Phosphorus) ni muhimu sana kwa ukuaji wa mizizi. Dalili za ukosefu wa kirutubisho hiki ni pamoja na; Mmea kudumaa, Majani huwa na rangi ya dhambarau iliyochangamana na wekundu. Mbolea ya mboji (Compost) husaidia kuongeza kiwango cha Fosforasi kwenye udongo, kama utakosa mbolea ya mboji tumia mbolea jamii ya Rock Phosphate kama mbolea ya 'MINJINGU'.

Kirutubisho cha Potassium huitajika sana na zao la muhogo husaidia kukomaza mazao haraka Dalili za ukosefu wa kirutubisho hiki ni pamoja na; Mmea hudumaa, Sehemu za mwisho za majani (Tips and Edges of lowest leaves) hukauka hususani kwa majani ya chini na majani hubadilika na kuwa rangi nyeusi iliyopauka. Kirutubisho hiki cha Potassium hupatikana kwenye mbolea ya mboji (Compost) na majivu ya mimea mbalimbali iliyochomwa.

Mara nyingi wakulima wadogo wadogo wa muhogo nchi nyingi za Afrika hawatumii mbolea za viwandani na mbolea za asili hii ni kutokana kutomudu kupata mbolea hizo hususani za viwandani pamoja na pembejeo zingine kama madawa ya wadudu na magonjwa n.k., mbolea za asili hupatikana kwenye maeneo yao, tatizo ni kukosa elimu ya matumizi ya mbolea hizo.

Hakikisha unahudumia mimea yako vizuri ili iwe na afya nzuri kwani mimea yenye afya haiathiriwi sana na wadudu waharibifu pamoja na magonjwa.

Kwa ujumla zao la muhogo hufanya vizuri sana kwa kutumia mbolea ya samadi, Mbolea hii ya samadi inatakiwa iwekwe wakati wa kuandaa shamba ili kuongeza rutuba ya udongo, kuboresha muonekano wa udongo (Soil structure) na kuongeza uwezo wa udongo kushikilia au kutunza maji.

Kama maeneo uliyopanda muhogo ni makame au kwenye miteremko, weka matandazo ya nyasi kavu juu ya udongo ili kupunguza upotevu wa unyevu wakati wa jua kali.


WADUDU WAHARIBIFU NA MAGONJWA

A: WADUDU WAHARIBIFU

1. Cassava mealybug (Phenacoccus manihoti)
Hawa ni wadudu wenye rangi ya pinki, mwili wao umefunikwa na utando (wax). Wakiwa wakubwa wanakua na urefu wa mm 0.5 - 1.4. Wadudu hawa majike wanaishi kwa siku 20 na wanataga wastani wa mayai 400. Wanazaliana mwaka mzima na husambazwa shambani kutoka mmea mmoja hadi mwingine kwa upepo.

Picha: Cassava mealybug       Photo Credit: www.pestnet.org

Athari
  • Wanafyonza maji maji yenye chakula kwenye majani na kwenye mashina. Wakati wa kufyonza majimaji hayo wanaacha sumu ndani ya mmea, sumu hiyo husababisha matawi ya juu ya mmea kulemaa na kudumaa. Hatimae matawi hayo ya juu hukusanyika pamoja (Bunchy tops).
  • Urefu wa mafundo ya mashina hupungua na mashina huharibika, athari ikizidi mmea hufa kuanzia sehemu ya juu ya matawi ya mmea (Plant tip) ambapo wadudu hawa huwepo na kuzaliana.
  • Wadudu hawa husababisha mmea kupukutisha majani na mashina yake kuharibika, hali inayopelekea kutofaa tena kwa matumizi ya vipande vya kupandia (Stem cuttings).
  • Mavuno ya muhogo hupungua kwa kiasi kikubwa kwa wastani wa asilimia 80%. Wadudu hawa huathiri sana kipindi cha kiangazi kuliko masika.

Namna ya kuwadhibiti
  • Panda mapema mara tu mvua zinapoanza ili kuufanya mmea wa muhogo kukua vizuri kabla ya kiangazi kufika. Mmea wenye afya hustahimili magonjwa na wadudu.
  • Funika mimea yako na nyasi kavu juu ya udongo (matandazo) 'Mulching', ili kupunguza upotevu wa maji hususani kwa udongo wa kichanga.
  • Epuka kutumia vipande vya mashina vyenye magonjwa na wadudu kwa kupandia. Kabla ya kupanda vilowanishe vipande hivyo kwenye maji ya vugu vugu kwa dakika 5 - 10. Jinsi ya kuandaa maji hayo; changanya maji ya moto na maji ya baridi kwa kiwango kinachofanana. Njia hii itasaidia kuua wadudu na magonjwa ili kuepuka kusambaa kwa mmea mpya utakaoota.
  • Epuka kutumia madawa ya kemikali ya kuua wadudu kwa mazao yaliyopandwa kuzunguka shamba la muhogo. Ingawa wakulima wengi wa zao la muhogo barani Afrika hawatumii madawa ya kemikali kuuwa wadudu au magonjwa, kemikali hizi zikitumiwa kwenye mashamba yaliyojirani na shamba la muhogo huwangamiza wadudu rafiki wanakula au kuwadhibiti wadudu hawa (Mealybugs).
  • Tumia mbolea za samadi, mboji au mbolea zingine, Mbolea hizo pamoja na matandazo 'Mulching' husaidia kupunguza kiwango cha wadudu hawa. Hii ni kwa sababu mmea wa muhogo ukipata virutubisho vizuri na ukapata afya nzuri hutengeneza kinga au dawa (antibiotic properties) dhidi ya wadudu hawa, hali inayopelekea kupunguza uharibifu na idadi yao.

<<< SEHEMU YA KWANZA


Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

Previous Post Next Post