Kilimo bora cha Mihogo - Sehemu ya Tatu (Growing Cassava - Part Three)


SEHEMU YA TATU

2. Larger grain borer (Prostephanus truncatus)
Hawa ni wadudu wanaoathiri mihogo baada ya kuhifadhiwa stoo, ndio wale wanaobungua mahindi yaliyohifadhiwa. Mihogo mikavu (Makopa) iliyotengenezwa na kuhifadhiwa hubunguliwa na wadudu hawa. Huleta hasara mpaka asilimia 70%.

Adult of Prostephanus truncatus.

Namna ya kuwadhibiti
Tumia dawa za asili kama Mwarobaini au majani yaliyokauka ya Lantana au Eucalyptus. Mimea hii 'Lantana' na 'Eucalyptus' ifahamu kwa kutizama picha zake hapo chini. Imethibitika kwamba ukihifadhi mihogo yako mikavu (Makopa) pamoja na majani mengi kiasi yaliyokauka ya 'Lantana' au 'Eucalyptus' husaidia kuwafukuza wadudu hawa.

A: MAJANI YA MWAROBAINI (NEEM LEAVES)

Picha: Majani ya mwarobaini    Photo Credit: www.indiamart.com


B: MAJANI YA LANTANA (LANTANA CAMARA)

Picha: Majani ya Lantana   

Picha: Matunda ya Lantana


CEUCALYPTUS (MAJANI YA MTI WA MKARATUSI)

Picha: Majani ya mti wa mkaratusi

3. Ndege pamoja na wanyama wengine
Wanyama hawa kwa ujumla wao kama Ndege, Panya, Nyani, Nguruwe, Ng'ombe, Mbuzi, Kondoo n.k huathiri sana zao la muhogo kwa namna tofauti tofauti inategemeana na aina ya mnyama mwenyewe.

Namna ya kuwadhibiti
  • Jenga wigo kuzunguka shamba lako ili kuwazuia wanyama kama Nguruwe, Nyani, Ng'ombe, Mbuzi n.k
  • Funika na udongo mihogo yote iliyotokeza juu ya ardhi.
  • Hakikisha usafi wa shamba lako, fanya palizi kwa wakati ili kuharibu makazi ya panya.
  • Vuna mihogo yako mara tu inapokomaa.

4. Cassava green spider mite (Mononychellus tanajoa or M. progresivus)
Hawa ni wadudu wadogo sana jamii ya buibui, wakiwa wadogo huwa na rangi ya kijani wakiwa wakubwa huwa na rangi ya njano. Mdudu jike aliyekua huwa na ukubwa wa mm 0.8. Wadudu hawa hukaa chini ya majani machanga, mashina machanga na kwenye maotea (buds) pia huonekana kama madoa madogo madogo yenye rangi ya kijani iliyochangamana na njano.

Picha: Spider mites akiwa kwenye jani la muhogo, na pembeni yake ni mayai  Photo Credit: www.infonet-biovision.org  shared under Creative common license

Athari
  • Sehemu ya chini ya majani machanga hubadilika rangi na kuwa njano (Pinpricks).
  • Madoa madoa hayo hubadilika na kua sehemu kubwa ya jani yenye rangi ya njano (Chlorosis). Hali hii hutokana kuharibika au kutokuwepo kwa Umbijani (Chlorophyll)
Picha: Majani ya muhogo yaliyoathiriwa na wadudu hawa  Photo Credit: www.infonet-biovision.org  shared under Creative common license

NB:
Athali/Dalili hizi hufanana na dalili za ugonjwa wa virusi wa muhogo uitwao 'African cassava mosaic disease', inatakiwa usichanganye. Majani yaliyoathiliwa na wadudu hawa hudumaa na kulemaa. Athari ikizidi sana majani ya juu ya mmea mwishoni hufa na kuanguka, wadudu hawa huathiri sana mmea kipindi cha kiangazi. Athari ya wadudu hawa ikizidi hupunguza kiwango cha mavuno kwa asilimia 20 - 80%.

Namna ya kuwadhibiti
  • Panda aina ya muhogo inayovumilia athari ya wadudu hawa.
  • Tumia maji ya vuguvugu kutibu vipande vya kupandia. Jinsi ya kuandaa maji hayo, changanya maji ya moto na maji ya vuguvugu kwa kiwango kinachofanana. Viloweke vipande hivyo kwenye maji ya vuguvugu kwa dakika 5 - 10 kabla ya kupanda.
  • Panda mapema mara tu mvua zinapoanza kunyesha, hii itasaidia mmea kukua vizuri na kuwa na uwezo wa kuhimili athari za wadudu hawa.
  • Panda Mbaazi pamoja na Muhogo, imethibitika kwamba ukipanda zao la mbaazi (pigeon pea) pamoja na muhogo athari ya wadudu hawa hupungua kwa kiasi kikubwa na mavuno huongezeka. Nafasi ya kupanda muhogo ni mita 1 kwa mita 1, kwa hiyo kama umeamua kupanda mazao mseto (Muhogo na zao jingine), inatakiwa uongeze upana wa mstari hadi mita 2, ili mbaazi zikae katikati.

5. Red spider mites (Oligonychus gossypii and Tetranychus spp.)
Hawa ni wadudu wadogo jamii ya bui bui wana rangi nyekundu, huvamia zao la muhogo hasa kwa majani yaliyozeeka, mdudu mkubwa ana urefu wa mm 0.6.

Picha: Mdudu huyu akiwa peke yake

Athari
  • Madoa madoa yenye rangi ya njano huonekana kwenye majani yaliyokomaa.
  • Hutengeneza utando kama wa bui bui wa kawaida, tofauti yake tu ni kwamba unakua laini sana. Majani yaliyovamiwa hubadilika rangi na kuwa mekundu, kahawia au rangi ya kutu (rusty)
  • Athari ikizidi majani hufa na kuanguka yakianzia na majani yaliyokomaa. Athari ya wadudu hawa huanza mwanzoni mwa msimu wa kiangazi.

Namna ya kuwadhibiti
  • Watunze wadudu rafiki wanaokula wadudu hawa kwa kuepuka kutumia madawa ya wadudu yanayoangamiza wadudu wa aina zote (Broad-spectrum pesticides).
  • Usipande zao lako la muhogo karibu na shamba lililoathiriwa na wadudu hawa.

6. Cassava scales (Aonidomytilus albus)
Hawa ni wadudu wenye magamba na utando wenye rangi nyeupe mwili mzima, utando huo hufanana na unga mweupe. Wadudu hao huwa na urefu wa mm 2 hadi 2.5.

Wadudu hawa kufunika shina au majani na utando huo mweupe unaotoka kwenye mwili wao. Mdudu dume ana mabawa na hupaa umbali mfupi, lakini jike hana mabawa na hana miguu hukaa mahali pamoja muda wote, hasogei kutoka sehemu moja hadi nyingine (Sedentary).

Wadudu hawa husambazwa kwa upepo au wanyama/Binadamu kutoka sehemu moja hadi nyingine. Mvua kubwa na Upepo mkali huweza kuwaondoa wadudu kwenye mmea, pia ukame wa muda mrefu huongeza kasi ya uharibifu wa wadudu hawa.

© USDA ARS, Bugwood.org

Athari
  • Wadudu hawa hufyonza maji maji yenye chakula kwenye mashina na majani na kusababisha sehemu hizo za mmea kupungukiwa maji.
  • Majani yaliyovamiwa na wadudu hawa hupauka rangi, hunyauka na hatimae hudondoka.
  • Mmea ulioathiriwa na wadudu hawa hudumaa na hutoa mavuno hafifu na kidogo.
  • Wadudu hawa wanaweza kuua mmea endapo mmea huo uliathiriwa na ukame pamoja na wadudu wengine hapo awali.
  • Vipande vya kupandia vilivyotoka kwenye mmea ulioathirika, vikipandwa havichipui.

Namna ya kuwadhibiti
  • Weka mbolea za asili shambani kama za samadi au mboji ili kuboresha rutuba ya udongo.
  • Chagua vipande vya kupandia vilivyo safi na visivyokua na wadudu hawa.
  • Chunguza shamba lako na choma moto mashina yote yaliyoathirika.
  • Epuka kutumia madawa ya kemikali yatakayoua wadudu rafiki wanaokula wadudu hawa (Cassava Scales).
  • Loweka vipande vyako vya mashina vilivyoathirika kwenye juisi ya mizizi ya muhogo kwa saa moja (dakika 60) kabla ya kupanda, huua kabisa wadudu. hawa. Matumizi ya maji ya moto hayaui wadudu hawa.
  • Panda aina ya muhogo inayovumilia athari ya wadudu hawa.
  • Tunza vipande vyako vya kupandia kwa mkao wa wima, hupanguza athari ya wadudu hawa.
  • Panda mihogo yako kwa nafasi ya kutosha, husaidia kupunguza mlipuko wa wadudu hawa.
  • Badilisha mazao kwa kupanda mazao mengine tofauti na muhogo.



Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

Previous Post Next Post