Kilimo bora cha Karanga - Sehemu ya Tano (Growing Groundnuts - Part Five)


SEHEMU YA TANO

B: MAGONJWA

1. Damping-off /Kukatika mashina ya miche
Huu ni ugonjwa unaoathiri mmea katika kipindi cha awali cha ukuaji, husababishwa na vimelea vya fangasi aina ya Pythium spp. na Rhizoctonia solani.

Picha: Mche wa nyanya wenye damping off, kwa upande wa karanga hufanana hivi hivi Photo Credit: www.kb.gramophone.in

Athari/Dalili
  • Mbegu nyingi zilizopandwa hushindwa kuota kwa sababu ya kuoza zikiwa chini ya udongo na miche michanga hufa, hali inayopelekea kuwa na shamba lenye muonekano mbaya.
  • Miche michanga iliyoathirika na iliyofanikiwa kuchomoza juu ya ardhi huwa na muonekano wa kuoza sehemu ya shina usawa wa ardhi, kuoza huko huwa na rangi ya kahawia na sehemu hiyo hubonyea. Baadae mche huanguka na kufa.
  • Ugonjwa huu huongezwa kasi na unyevu wa udongo uliozidi shambani na jotoridi dogo la udongo.
Namna ya kudhibiti
  • Panda mbegu bora zilizothibitishwa kitaalamu na zisizokua na magonjwa.
  • Epuka kuongeza unyevu kupita kiasi shambani, hususani kwa kumwagilia. Au kama eneo lako linatwamisha maji mara tu baada ya mvua kunyesha tengeneza mifereji ya kuchepusha maji.
  • Epuka kutumia mbolea nyingi zenye kirutubisho cha Nitrogen kama UREA, NPK, SA, Boosters mbali mbali (Mbolea za kwenye majani) n.k.
  • Badilisha mazao kwa kupanda mazao jamii ya nafaka kama mahindi, mtama, uwele, ulezi n.k. Usipande karanga kwenye shamba moja misimu kadhaa mfululizo au kwenye shamba lililopandwa Pamba au mimea jamii ya mikunde.

2. Leaf spots (Cercospora spp.) /Madoa kwenye majani
Huu ni ugonjwa unaosababishwa na bakteria aina ya Mycosphaerella arachidis na Cercospora arachidicola, ugonjwa huu huathiri majani, mashina na sehemu zingine.

© Queen’s Printer for Ontario, 2012

Athari/Dalili
  • Majani hua na madoa ya mviringo yenye rangi ya kahawia iliyochangamana na rangi nyeusi, hali hii huonekana upande wa juu wa jani. Upande wa chini wa jani huwa na rangi hiyohiyo lakini iliyopauka. Pia wakati mwingine mstari wa rangi ya njano huonekana kuzunguka mviringo wa doa (Early Leaf spot). Pia hali hii huonekana kwenye mashina na sehemu zingine.
  • Ugonjwa ukizidi (Late Leaf spot), kunakua na miduara ya fangasi chini ya majani, na muonekano wa jani unakua rafu. Hatimae mmea hupukutisha majani na kudumaa.
Namna ya kudhibiti
  • Panda aina ya karanga inayovumilia ugonjwa huu
  • Mimea yote iliyoathirika na ugonjwa huu, ing'oe, ikusanye kisha ichome moto.
  • Badirisha mazao kwa kupanda mazao mengine tofauti na karanga

3. Rust (Puccinia arachidis) /Kutu
Huu ni ugonjwa unaofanana na kutu, husababishwa na vimelea aina ya Puccinia arachids huathiri majani na mashina ya mmea kasoro maua.

Photo Credit: Nigel Cattlin    Website: www.sciencesource.com

Athari/Dalili
  • Eneo lote la juu la mmea kuanzia kwenye shina kasoro maua, huwa na vivimbe vidogo vidogo vyenye maji ndani yake.
  • Mwanzoni vivimbe vya njano huanza kuonekana chini ya majani, baadae vibimbe hivyo huonekana juu ya majani.
  • Vivimbe vilivyopo kwenye mashina hutawanyika zaidi na huwa vikubwa zaidi kuliko vya kwenye majani. Vivimbe hivyo vikikua hupasuka na kutoa vitu vyenye rangi nyekundu iliyochangamana na Kahawia. Vitu hivi huwa ni vimelea (Spores) vya ugonjwa huu, Upepo ukivuma husambaza vimelea hivi kutoka mmea mmoja hadi mwingine, pia vinaweza kufika mbali hadi shamba lingine la karanga. Ugonjwa huu husababisha mmea kudumaa na uzalishaji kupungua.
Namna ya kudhibiti
  • Panda aina ya mbegu inayohimili ugonjwa huu
  • Badilisha mazao kwa kupanda mazao mengine tofauti na karanga.
  • Panda kwa wakati ili kuepusha mazingira hatarishi ya kuwepo na kuongezeka kwa ugonjwa huu kama; Kiwango cha juu cha unyevu hewani, Ukungu n.k


Posted by: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

Previous Post Next Post