KILIMO CHA PILIPILI KICHAA SEHEMU YA TISA
B: MAGONJWA
1. Fusarium wilt (Mnyauko Fuzari)
Huu ni ugonjwa wa kuvu
unaosababishwa na vimelea vya fangasi, vimelea hawa husambazwa kupitia udongo
(soil borne fungal disease), huenea sana wakati wakati wa joto kali. Ugonjwa
huu huathiri mmea wote ikiwemo mizizi, mashina, matawi na majani.
Picha: Fusarium wilt shared under a Creative commons license
Athari
- Mmea ulioathirika huwa dhaifu na
majani yake huwa ya njano.
- Ukikata shina usawa wa ardhi
utaona rangi ya kahawia iliyochangamana na nyekundu, pia ukipasua kwa ndani
zaidi utaona rangi ya kutu.
Namna ya kudhibiti
- Hakikisha usafi wa shamba
- Badilisha mazao
- Kama udongo unatwamisha maji,
tengeneza vimfereji vya kuondosha maji (drainage channels)
- Kama umetumia vyombo maalumu kwa
kuotesha miche, hakikisha unaviosha vizuri na kuvitunza mahala pasafi.
- Lima shamba lako kwa kina cha
kutosha na kuliacha shamba hilo lipigwe na jua kwa miezi kadhaa kabla ya
kupanda. Hii itasaidia kuua vimelea wanaosababisha ugonjwa huu.
- Mimea iliyoathirika iondolewe
shambani pamoja na udongo uliopo kwenye mizizi na ichomwe moto.
- Weka matandazo ya nyasi kavu (mulching),
matandazo haya husaidia kudhibiti joto la udongo. Ugonjwa huu huenea sana
wakati joto kali.
2. Southern blight (Sclerotium
wilt)
Ugonjwa huu husababishwa na
vimelea wa fangasi (Kuvu), ugonjwa huu hutokea kwa muda mfupi hususani kwa
maeneo yenye joto jingi na unyevu mwingi.
Athari
- Majani ya chini hunyauka
- Fangasi zenye rangi nyeupe huota
kwenye mashina
Namna ya kudhibiti
- Mimea yote iliyoathirika
ing'olewe pamoja na udongo wake kwenye mizizi kisha ipelekwe mbali na eneo la
shamba na ichomwe moto.
- Lima shamba lako kwa kina cha
kutosha hii itasaidia kuwaweka fangasi hao chini ya ukanda wa mizizi (Below the
root zone).
3. Anthracnose
Ugonjwa huu huathiri sana zao la pilipili, husababishwa na
vimelea wa fangasi (Kuvu). Husambazwa kutoka mmea mmoja hadi mwingine au kutoka
msimu mmoja hadi mwingine kupitia masalia ya mimea yenye ugonjwa huu.
Picha: Anthracnose Photo Credit: www.ipmimages.org
Picha: Anthracnose Photo Credit: www.pestnet.org
Athari
- Matunda ya pilipili huwa na maeneo meusi yaliyobonyea na
yenye majimaji baadae maeneo haya hubadirika na kutengeneza utando mweusi. Pia
unato wenye rangi ya pinki huweza kuonekana kwenye matunda, unato huu ni mbegu
(spores) ambazo husambaza ugonjwa huu wa fangasi.
- Matunda yaliyoathirika huoza.
Namna ya kudhibiti
- Ondoa na choma moto mimea yote iliyoathirika shambani pia
baada ya kuvuna choma moto masalia yote, kwa sababu ugonjwa huu huenezwa
kupitia masalia ya mimea iliyoathirika.
- Badirisha mazao
- Tumia mbegu zilizothibitishwa kitaalamu kwa sababu ugonjwa
huu husambazwa kupitia mbegu zilizotoka kwenye mmea ulioathirika na ugonjwa huu
(seed-borne).
- Kama unataka kuaandaa mbegu kutoka kwenye mimea
uliyopanda, hakikisha unachagua mimea yenye afya na isiyokua na ugonjwa.
- Vuna matunda ya pilipili mara tu yanapokomaa, kufanya hivi
husaidia kupunguza ya ugonjwa huu kujijenga kwenye matunda.
4. Bacterial spot (Madoa bakteria)
Ugonjwa huu husababiswa na vimelea
wa bakteria, husambaa haraka kwenye maeneo yenye joto jingi na unyevu mwingi.
Vilevile ugonjwa huu husambazwa kupitia mbegu (seed-borne).
Penn State Department of Plant Pathology & Environmental Microbiology Archives , Penn State University, Bugwood.org
licensed under a Creative Commons Attribution-Noncommercial 3.0 License
licensed under a Creative Commons Attribution-Noncommercial 3.0 License
Athari
- Husababisha madoa madoa yenye
rangi ya kahawia chini ya majani (Bacterial spots) na kwenye matunda.
- Bakteria hawa huingia kwenye
matunda na kusababisha matunda kuoza.
Namna ya kudhibiti
- Usiandae mbegu za kupanda kutoka
kwenye mmea ulioathorika na ugonjwa huu.
- Tumia dawa mbalimbali za ukungu
hususani zenye kiua sumu cha mancozeb.
5. Magonjwa ya virusi (Viruses disease)
Kuna magonjwa mengi ya virusi yanayoathiri zao la pilipili,
magonjwa hayo makubwa ni pamoja na Tobacco Etch Virus (TEV) na Potato Virus Y
(PVY). Magonjwa mengine ni pamoja na Pepper Mottle
Virus (PeMV), Pepper Veinal Mottle Virus (PVMV), Tobacco Mosaic Virus (TMV) na
Cucumber Mosaic Virus (CMV). Magonjwa yote hufanana dalili na athari kwenye
mmea.
Florida Division of Plant Industry , Florida Department of Agriculture and Consumer Services, Bugwood.org
licensed under a Creative Commons Attribution-Noncommercial 3.0 License.
licensed under a Creative Commons Attribution-Noncommercial 3.0 License.
Athari
- Majani hubadilika rangi na kuwa ya njano na hujikunja
kuelekea juu.
- Mmea ulioathirika hudumaa na hutoa matunda kidogo.
Namna ya kudhibiti
Njia madhubuti ya kudhibiti ugonjwa huu ni kukinga mmea
usipate maambukizi ya virusi hivi. Zifuatazo ni njia mahsusi za kudhibiti
ugonjwa huu.
- Tumia mbegu zilizothibitishwa kitaalamu kwani ugonjwa kama
TMV husambazwa kupitia mbegu.
- Hakikisha mmea hauna wadudu waharibifu wanaosambaza
ugonjwa huu kama Vidukari mafuta (Aphids) na wadudu wengine. Pulizia dawa
mbalimbali kuwaondoa wadudu hawa.
- Pia unaweza ukapanda mazao kama mahindi kuzunguka mipaka
ya shamba lako (berrier crops), zao la mahindi huzuia wadudu kama Vidukari
mafuta (Aphids) kuingia shambani. Pia punguza kushika mimea pasipo sababu,
kwani unaweza kusambaza ugonjwa kwenye mimea yenye afya.
- Badirisha mazao na kuondoa magugu kama Black nightshade, magugu haya huvutia wadudu wanaosambaza
magonjwa haya ya virusi. Tazama picha ya gugu hili kulifahamu.
Picha: Black night shade
MAVUNO
Pilipili kichaa huwa tayari kuvunwa baada ya wiki 8 hadi 12
baada ya kupandikizwa au wiki 3 hadi 6 baada ya kutoa maua, ingawaje hii
itategemeana na aina ya mbegu na hali ya hewa pamoja au msimu husika.
Matunda yakikomaa hubadirika rangi kutoka kijani kuwa njano,
rangi ya chungwa au nyekundu. Kwa hiyo uhitaji wa soko wa rangi mahsusi ya
pilipili utampa wasaa mkulima avune pilipili hizo wakati gani aidha wakati ziko
mbichi au wakati zimeiva, vuna pilipili zako mara
moja kwa wiki.
Kama utatunza shamba lako vizuri
na kufwata mbinu za kilimo bora kama nilivyoeleza kwenye makala hii, utaweza
kuvuna kilo 1000 hadi 3000 kwa ekari moja (tani 1 hadi 3 kwa ekari moja) sawa
na gramu 600 za pilipili mbichi kwa mche mmoja wa pilipili.
MWISHO WA MAKALA HII
Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo
Asante kwa elimu, iwapo kuna kitabu naomba kujua namna ya kukipata
ReplyDeleteAsante kwa somo hili la Pilipili, somo linaeleweka vizuri.
ReplyDeletePost a Comment