KILIMO CHA PILIPILI KICHAA SEHEMU YA NANE
4. Pepper hornworm
Huyu ni kiwavi mwenye muonekano wa kama pembe kichwani, ndio
maana wakamuita 'Hornworm'. Kiwavi huyu ni mkubwa hufikia urefu wa sm 9 na
upana wa sm 1.3, hujificha chini ya majani wakati wa mchana.
Athari
- Viwavi hawa hutafuna majani ya pilipili, wakati wachana
unaweza usiwaone, ila utagundua kama wapo baada ya kuona vipande vya majani
vilivyoanguka chini.
Namna ya kuwadhibiti
- Unaweza kuwaondoa kwa mkono na
kuwaua, hususani kama shamba lako ni dogo.
- Pia wadudu hawa wanaweza
wakapunguzwa na ndege pamoja mdudu anaeitwa 'Parasitic wasps', tazama picha
hapo chini kumfahamu
- Tumia dawa za kemikali zinazopatikana
kwenye maduka ya pembejeo za kilimo, ila hakikisha unatumia dawa zisizoua
wadudu rafiki, pia kumbuka kutumia dozi sahihi ya dawa kama ilivyoandikwa
kwenye kibandiko cha chupa ya dawa pamoja na kufwata ushauri wa wataalamu wa
kilimo.
5. Mites
Hawa ni wadudu wadogo sana wanaofanana na buibui, nao
hutengeneza utando kama walivyo buibui wa kawaida. Huwa na rangi nyekundu,
njano au kijani, wadudu hawa huvamia majani pamoja na maeneo mengine ya mmea.
Wakiwa wachache huwezi kuwagundua, ila wakiwa wengi utawagundua baada ya kuona
majani yamebadirika rangi na kuwa njano, utakaposogea karibu na kuchunguza
utaona mkusanyiko wa wadudu hawa wakiwa wametengeneza utando wao.
Picha: red spider mites Photo Credit: www.nature-and-garden.com
Athari
- Majani hubadirika rangi na kuwa ya njano pamoja na
kujikunja, pia jani huharibika muonekano wake pamoja na majani mengine
kupukutika. Pia na matawi nayo huharibika.
- Mmea hupukutisha maua na matunda yaliyotoka hayakui
vizuri.
- Athari ikizidi mmea hudumaa.
Namna ya kuwadhibiti
- Udhibiti wa wadudu hawa huanzia
kwenye hatua za awali za ukuaji wa mmea hususani kwenye kitalu mpaka shambani,
Chunguza kwa makini kwenye kitalu ili kubaini uwepo wa wadudu hawa vilevile
wakati wa kupandikiza, mmea wowote utakaonekana una wadudu hawa uondoe taratibu
kisha uchome moto. Ni muhimu kuiondoa taratibu mimea yenye wadudu hawa
kwasababu, wadudu hawa ni rahisi kuhama kutoka mmea mmoja hadi mwingine kwa
kushika mmea, pia kwenye nguo au upepo.
- Badirisha mazao kwa kupanda
mazao tofauti na yale yanayovamiwa na wadudu hawa kama mazao ya nafaka ikiwemo
mahindi, mtama n.k au mazao ya mafuta kama alizeti. Mazao mengine yanayovamiwa
na wadudu hawa ni pamoja na Viazi vitamu, Viazi mviringo, Nyanya, Kunde,
Maharage, Miembe, Michungwa, Miparachichi, Kahawa, Mipapai na Mipera. Hakikisha
unapanda pilipili kwenye maeneo ambayo hakuna mazao niliyoyaorodhesha hapo juu,
pia wakati wa kubadirisha mazao panda aina tofauti na mazao hayo.
- Pia unaweza ukatumia dawa za
kemikali zinazopatikana kwenye maduka ya pembejeo za kilimo. Sharti, tumia dawa
hizo kwa kufwata ushauri wa kitaalamu.
6. Nematodes (minyoo fundo)
Hawa ni minyoo wadogo sana (microscopic eelworms) waishio
kwenye udongo, hutegemea mizizi ya pilipili kuishi.
Picha: Root knot nematodes
Athari
- Minyoo hawa husababisha vivimbe vidogo vidogo kwenye
mizizi na kusababisha mizizi kuharibika kabisa. Hali hii hupunguza uwezo wa
mizizi kufyonza maji na virutubisho kutoka kwenye udongo.
- Athari ikizidi mmea hunyauka, utagundua hali hii pale
unapoona udongo wa shamba lako una unyevu wa kutosha lakini baadhi ya mimea
inanyauka na kufa.
Namna ya kudhibiti
- Andaa kitalu chako vizuri kwa kuchanganya udongo wa kitalu
na mbolea ya samadi iliyooza vizuri. Mbolea isiyooza vizuri au mbichi ndio
chanzo cha minyoo hawa, kumbuka, tatizo la minyoo hawa huanzia kwenye kitalu.
Kurejea sehemu ya awali ya makala hii kuhusu namna nzuri ya kuandaa kitalu
chako BOFYA HAPA.
- Badirisha mazao kwa kupanda mazao mengine tofauti na mazao
ya mbogamboga kama; Mazao ya nafaka kama mahindi, mtama n.k au mazao ya mafuta
kama Alizeti.
- Ukishaandaa shamba lako na kulilima vizuri, usipande bali
liache lipigwe na jua kwa mwezi mmoja au zaidi, ndipo baada ya hapo upandikize
miche yako. Mwanga wa jua ni tiba husaidia kuua vimelea mbalimbali kwenye
udondo ikiwa ni pamoja na minyoo hawa. Ili kufanikisha hili unaweza ukaandaa
shamba lako mapema kabla ya kitalu, mpaka miche inafikia kupandikizwa, shamba
lako litakua limepata mwanga wa jua kwa kiwango cha kutosha.
NB:
Hawa ni baadhi tu ya wadudu
wanaoathiri zao la pilipili/pilipili kichaa, kuna wadudu wengine wengi pia
ambao huathiri zao hili kama; Pepper budworm, Thrips, Corn earworm, Pepper
weevil, Fruit fly, Pepper maggot na Tropical white mite. Kipindi kijacho
nitaleta maelezo ya kina kuhusiana na wadudu hawa na namna ya kuwadhibiti.
Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo
Post a Comment