Kilimo Bora cha Pilipili kichaa - Sehemu ya Saba (Growing Chili pepper - Part Seven)


KILIMO CHA PILIPILI KICHAA SEHEMU YA SABA

MATUMIZI YA MBOLEA
Zao la pilipili hufanya vizuri sana kwenye udongo wenye maozea au samadi, kwa hekta 1 inahitajika Tani 10 - 20 sawa na Tani 4 - 8 kwa ekari moja, mbolea hii huchanganywa vizuri na udongo. Kama kuna changamoto ya kupata mbolea hizi kwa kiwango hicho, basi unaweza ukaweka kiganja kimoja cha samadi iliyooza vizuri kwa kila shimo kama nilivyoeleza kwenye kipengele cha kupandikiza miche hapo juu.

Pia unaweza ukatumia mbolea za chumvi chumvi zenye kirutubisho cha 'Phosphorus (P)' wakati wa kupandikiza, mbolea hizi husaidia kuimarisha mizizi ya miche michanga. Mbolea hizo ni pamoja na DAP, NPK, NPS, TSP n.k.

Kama nilivyokwishaeleza hapo mwanzo kwamba zao la pilipili huitaji udongo wenye pH kuanzia 5.5 - 7.5 na wenye kiwango kidogo cha kirutubisho cha Naitrojeni (N) kwa hiyo inakupasa utumie mbolea zenye kiwango kidogo cha kirutubisho cha Naitrojeni kama NPK, CAN n.k, usitumie mbolea aina ya UREA, kwa sababu mbolea hii ina kiasi kikubwa cha kirutubisho cha Naitrojeni, ukitumia UREA mmea utakua na majani mengi kuliko matunda.

Mara tu unapoona mmea umetoa maua ya kwanza basi ni wakati wa kuweka mbolea ya kukuzia aina ya CAN (Calcium Ammonium Nitrate). Mbolea hii husaidia kuongeza idadi ya matunda na kuyaboresha, kirutubisho cha 'Calcium' kilichopo kwenye mbolea hii husaidia kuzuia ulemavu wowote kwenye matunda, pia hoboresha ngozi ya matunda na kuimarisha. Weka mbolea hii kila baada ya wiki 2 tangu kutoa maua ya kwanza.

Pia ni muhimu kutumia mbolea za kwenye majani (Foliar fertilizer) au Booster, mbolea hizi zina virutubisho muhimu (Macro-nutrients) kama Nitrogen, Phosphorus na Potassium pamoja na virutubisho vidogo vidogo (Micro-nutrients) kama Magnesium (Mg), Calcium (Ca), Zinc (Zn), Boron (Bo), sulphur (S) n.k. Virutubisho vyote hivi ni muhimu kwa ukuaji wa mmea. Tumia mbolea hizi za maji pamoja na zile za chumvi chumvi kwa pamoja.

KUDHIBITI WADUDU WAHARIBIFU NA MAGONJWA

A: WADUDU WAHARIBIFU

1. Aphids (Vidukari mafuta)
Hawa ni wadudu wadogo wanaovamia mazao mengi ya mboga mboga ikiwemo pilipili. Wanakua na rangi ya kijani, kahawia au nyeusi, baadhi wana mabawa na wengine hawana. Wadudu hawa ni wadogo sana lakini wanaonekana kwa macho.


Picha: Aphids (Vidukari mafuta)

Athari
- Hufyonza majimaji yenye chakula kwenye mmea hususani nchini ya majani machanga na matawi.
- Wakizidi sana husababisha mmea kudumaa na kupunguza kutoa matunda, kwa sababu huwa wengi sana maeneo yanayotoa maua au matunda.
- Hutoa uteute kama unato (mafuta) ambao baadae huvunda na kutengeneza ukungu ambao huathiri uwezo wa jani wa kujitengenezea chakula, ukiwa kwenye matunda hupunguza hadhi ya soko ya tunda hilo.
- Wanavyofyonza majimaji hayo yenye chakula kutoka mmea mmoja hadi mwingine, husambaza ugonjwa virusi kama 'TMV' (Tobacco Mosaic Virus).

Namna ya kuwadhibiti
- Panda mahindi kuzunguza mipaka ya shamba lako kabla ya kupanda pilipili zako, hii itasaidia kutowavutia wadudu hawa kusogea shambani na kuvamia pilipili.
- Kama utaamua kutumia dawa za kemikali basi hakikisha unatumia dawa ambazo haziui wadudu rafiki kama 'Predatory beetles', wadudu hawa rafiki hula wadudu hawa, kwa hiyo husaidia kupunguza idadi yao. Pia dawa zingine huua wadudu rafiki wanaochavusha maua, hali itakayopelekea kupunguza idadi ya matunda. Kumfahamu mdudu huyu tazama picha hapo chini;

Picha: Predatory beetles (Lady bird beetle)

Pia hakikisha unatumia dawa hizo kwa kufwata maelekezo ya kibandiko cha chupa ya dawa pamoja na maelekezo ya wataalamu wa kilimo.

2. Crickets
Wadudu hawa hufanana na panzi wadogo, isipokua hawa wana mwili mkubwa na wana rangi nyeusi. Wadudu hawa huishi kwenye mashimo ya kwenye udongo karibia na mmea wa pilipili uliopo shambani na kwenye kitalu.
Picha: Crickets     Photo Credit: www.thedailygardener.com

Athari
- Wadudu hawa hufanya mashambulizi wakati wa usiku kwa kukata miche michanga na kuivutia ndani ya mashimo yao kwa ajili ya chakula, hali hii huharibu na hupunguza idadi ya miche, Wakati wa mchana wanajificha kwenye mashimo yao.

Namna ya kuwadhibiti
- Wadudu hawa hudhibitiwa wakati wa kuandaa shamba, hususani wakati wa kufyeka nyasi au vichaka pamoja na kulima. Baada ya kulima shamba liache likae kwa muda kidogo wakati huo unaandaa kitalu, mpaka miche ikifikia kupandikiza, wadudu hawa watakua wameliwa na ndege au mijusi.
- Kwa upande wa kitalu, kama eneo lako lina kiwango kikubwa cha wadudu hawa, tumia matrei au ndoo zenye udongo ambazo utaziweka juu ya kitu fulani au meza, au unaweza ukafunika kitalu chako na neti.

3. Cucumber beetle
Wadudu hawa huathiri sana kipindi cha awali cha ukuaji wa pilipili. Mdudu huyu ana rangi ya njano iliyochangamana na kijani na ana michilizi myeusi mgongoni pia hufikia urefu wa ¼ inchi (mm 6).

Picha: Cucumber beetle      Photo Credit: www.extension.msstate.edu

Picha: Cucumber beetle    Photo Credit: www.entnemdept.ufl.edu

Athari
- Wadudu hawa hutoboa matundu madogo kwenye majani, hali inayopelekea kupunguza ufanisi wa jani kutengeneza chakula.
- Kiwavi wa mdudu huyu huharibu mizizi ya pilipili.
- Wadudu hawa husambaza ugonjwa wa 'mnyauko bakteria' (Bacterial wilt) na baadhi ya magonjwa ya virusi (Mosaic viruses).

Namna ya kuwadhibiti
- Ondoa magugu kuzunguka mipaka ya shamba na ndani ya shamba la pilipili.


<<< SEHEMU YA SITA


Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

Previous Post Next Post