KILIMO CHA PILIPILI KICHAA SEHEMU YA SITA
KUPIMA UDONGO
Hatua hii ni muhimu sana kwa mazao
yote ikiwemo zao la pilipili, kupima udongo kutasaidia kufahamu hali ya udongo
kama virutubisho vilivyomo pamoja hali ya tindikali ya udongo (pH). Zao la
pilipili hufanya vizuri kwenye udongo usiotwamisha maji na wenye kiasi cha
tindikali (pH) kuanzia 5.5 - 7.5 na kiasi kidogo cha kirutubisho cha
Naitrojeni, kwa hiyo pH ikipungua au ikizidi zaidi ya kiwango hicho mmea
hautafanya vizuri. Ukitaka kupima udongo wa shamba lako waone wataalamu wa
kilimo (Ma Afisa Kilimo) walio karibu nawe.
Kwa mfano kama ikitokea shamba
lako lina pH kuanzia 3.9 - 5.0, shamba lako lina kiwango kikubwa cha asidi
(acids), hali hii inahitaji kuiongeza hiyo pH hadi kufikia 7.0.
Hali hiyo inabadilishwa kwa
kutumia chokaa (Lime), kama ikitokea shamba lako lina pH 4.0, hivyo
kitahitajika kiasi cha Tani 3.6 (3.6 Tonnes) za chokaa kuongeza pH hadi 7.0 kwa
ekari moja.
Chokaa huongezwa wakati wa kuandaa
shamba kabla ya kupanda, chokaa hii huchanganywa vizuri kwenye udongo.
Kama udongo umepimwa na kuna
upungufu wa virutubisho aidha Nitrogen, Phosphorus, Potassium, Magnesium,
sulfur, Zinc au Calcium n.k., mtaalamu wa kilimo atakushauli utumie kiasi gani
cha mbolea kwenye udongo huo.
KUANDAA SHAMBA
Kama yalivyo mazao mengine, shamba
lililokusudiwa kupanda pilipili lazima lilimwe vizuri, ikiambatana na
maandalizi ya kitalu kwa ajili ya kusia mbegu za pilipili. Vilevile kama shamba
lako limegundulika lina kiwango kikubwa cha asidi (acids) mfano pH 4.0, basi
ukishalima vizuri, ni wakati wa kuchanganya udongo wako na chokaa (Lime) kiasi
cha Tani 3.6 kwa ekari moja. Kama itagundulika pH ya udongo wako ni kuanzia 5.5
- 7.5 basi shamba lako linafaa kupanda zao hili.
KUANDAA KITALU
Mbegu za pilipili/pilipili kichaa
hupandwa kwanza kwenye kitalu ndipo baadae huamishiwa shambani. Yafwatayo ni
maelezo ya kina namna ya kuandaa kitalu;
1. Lima vizuri eneo lako la
kutengenezea kitalu
2. Tengeneza matuta yenye upana wa
mita moja na urefu wowote.
3. Weka mbolea ya samadi iliyooza
vizuri, kiasi cha ndoo moja kubwa ya samadi kwa m² moja, mfano kama tuta lako lina urefu wa mita 5, ina maana
eneo lake ni m²
5, sawa na ndoo kubwa 5 za samadi. Ichanganye vizuri mbolea hiyo na udongo,
kisha sawazisha juu ya tuta pawe tambalale.
Hakikisha mbolea ya samadi
unayotumia imeoza vizuri, kwani mbolea ya samadi mbichi huongeza uwezekano wa
minyoo fundo (Root nematodes) kwenye mizizi ya pilipili.
4. Baada ya kusawazisha matuta
yako, tandaza juu ya tuta nyasi kavu zilizokauka vizuri, kisha choma moto nyasi
hizo zikiwa juu ya tuta mpaka ziungue zote. Moto wa nyasi hizi husaidia kuua
wadudu na magonjwa ya kwenye udongo ambayo baadae huweza kuathiri mche wa
pilipili.
5. Baada ya nyasi kuungua acha
tuta lako lipoe kabla ya kusia mbegu.
6. Baada ya tuta kupoa, tengeneza
vimfereji kukatisha tuta vinavyoachana kwa sm 10.
7. Sia mbegu kwa kuziachilia
kidogo kidogo kwenye vimfereji hivyo, kisha fukia na udongo kiasi.
8. Baada ya kufukia vizuri,
tandaza nyasi kiasi kavu na laini juu ya tuta, kisha mwagilia maji vizuri.
Nyasi hizi husaidia kuzuia mbegu zilizopandwa kutawanyika wakati wa kumwagilia.
Nyasi hizo huondolewa baada ya wiki moja tangu kusia mbegu, wakati huu mbegu
zote huwa zinakua zimeota.
9. Baada ya kumwagilia maji,
pulizia dawa ya kuvu (ukungu) na wadudu ju ya nyasi hizo. Hii itasaidia mbegu
zote kuota na kuepusha kupata ugonjwa wa kuoza shina usawa wa ardhi (dumping
off).
10. Baada ya wiki moja tangu kusia
mbegu, ondoa taratibu nyasi hizo, kisha tengeneza kichanja chenye kimo cha mita
1 juu ta tuta, alafu juu tandaza nyasi kavu kwa ajili ya kivuli. Kichanja hiki
husaidia kuepusha miche dhidi ya jua kali au mvua kubwa. Endelea kumwagilia
maji asubuhi na jioni kila siku.
NB:
Utaratibu huu wa kuandaa kitalu ni
kwa mazao yote yanayohitaji kuandaa kitalu ikiwemo zao la pilipili.
KUPANDIKIZA MICHE SHAMBANI
Miche huwa tayari kupandikizwa shambani baada ya siku 30 -
40, wakati yakiwa na majani 8 - 10. Wiki moja kabla ya kupandikiza (siku 23 -
33) ondoa kichanja na punguza kiwango cha kumwagilia maji. Kama ulikua
unamwagilia asubuhi na jioni, basi anza kumwgilia jioni tu, hii ni kwa sababu
unaiandaa miche kuzoea hali ya shambani.
Wakati wa kupandikiza, ng'oa miche kwenye kitalu wakati kuna
unyevu wa kutosha, au mwagilia maji kitalu chako kabla ya kung'oa miche.
Using'oe miche kwenye kitalu wakati hakuna unyevu, utasababisha mizizi ya miche
kukatika. Hali hii itapelekea miche kukauka mara tu baada ya kupandikiza.
Hakikisha unapandikiza miche yako wakati wa jioni, au wakati
kuna mawingu, ukipandikiza wakati wa jua kali miche yako itakauka. Jambo
lingine la muhimu hapa ni kwamba usichelewe kupandikiza miche yako baada ya 30
au 40, kwani itakua imekomaa sana na ikipandikizwa haitastawi. Jitahidi
kupandikiza kabla ya siku 40, kuanzia siku ya 30 hadi 40 yenyewe.
Pia hakikisha shamba la kupandikiza miche lina unyevu wa
kutosha, chimba mashimo ya kupandikiza miche yako yenye kina cha sm 3 na yenye
nafasi ya sm 20 shina hadi shina na sm 60 - 75 mstari hadi mstari (sm 20 X sm
60 - 75).
Baada ya kuchimba mashimo hayo, weka mbolea ya samadi
iliyooza vizuri kwa kiasi cha kiganja kimoja cha mkono wako kwa kila shimo
kisha ichanganye vizuri mbolea hiyo na udongo.
Baada ya kuchanganya mbolea yako na udongo vizuri, panda
miche yako mara tu baada ya kuing'oa kwenye kitalu, ili kupunguza atari ya
kukauka. Fukia udongo vizuri kisha mwagilia maji, pia kwa wakati huohuo pawepo
na mtu mwingine anayepulizia dawa ya kuvu na wadudu.
PALIZI
Kama ilivyo mazao mengine, zao la
pilipili nalo huhitaji palizi kwa wakati. Nyasi zikizidi shambani mimea hudumaa
na uzalishaji hupungua. Pia unaweza ukaweka matandazo ya nyasi kavu (mulching)
shambani ili kuzuia upotevu wa maji hususani wakati wa kiangazi na kuzuia
magugu kuota.
Post a Comment