KILIMO CHA PILIPILI KICHAA SEHEMU YA SABA
MATUMIZI YA MBOLEA
Zao la pilipili hufanya vizuri
sana kwenye udongo wenye maozea au samadi, kwa hekta 1 inahitajika Tani 10 - 20
sawa na Tani 4 - 8 kwa ekari moja, mbolea hii huchanganywa vizuri na udongo.
Kama kuna changamoto ya kupata mbolea hizi kwa kiwango hicho, basi unaweza
ukaweka kiganja kimoja cha samadi iliyooza vizuri kwa kila shimo kama
nilivyoeleza kwenye kipengele cha kupandikiza miche hapo juu.
Pia unaweza ukatumia mbolea za
chumvi chumvi zenye kirutubisho cha 'Phosphorus (P)' wakati wa kupandikiza,
mbolea hizi husaidia kuimarisha mizizi ya miche michanga. Mbolea hizo ni pamoja
na DAP, NPK, NPS, TSP n.k.
Kama nilivyokwishaeleza hapo
mwanzo kwamba zao la pilipili huitaji udongo wenye pH kuanzia 5.5 - 7.5 na
wenye kiwango kidogo cha kirutubisho cha Naitrojeni (N) kwa hiyo inakupasa
utumie mbolea zenye kiwango kidogo cha kirutubisho cha Naitrojeni kama NPK, CAN
n.k, usitumie mbolea aina ya UREA, kwa sababu mbolea hii ina kiasi kikubwa cha
kirutubisho cha Naitrojeni, ukitumia UREA mmea utakua na majani mengi kuliko
matunda.
Mara tu unapoona mmea umetoa maua
ya kwanza basi ni wakati wa kuweka mbolea ya kukuzia aina ya CAN (Calcium
Ammonium Nitrate). Mbolea hii husaidia kuongeza idadi ya matunda na
kuyaboresha, kirutubisho cha 'Calcium' kilichopo kwenye mbolea hii husaidia
kuzuia ulemavu wowote kwenye matunda, pia hoboresha ngozi ya matunda na
kuimarisha. Weka mbolea hii kila baada ya wiki 2 tangu kutoa maua ya kwanza.
Pia ni muhimu kutumia mbolea za
kwenye majani (Foliar fertilizer) au Booster, mbolea hizi zina virutubisho
muhimu (Macro-nutrients) kama Nitrogen, Phosphorus na Potassium pamoja na
virutubisho vidogo vidogo (Micro-nutrients) kama Magnesium (Mg), Calcium (Ca),
Zinc (Zn), Boron (Bo), sulphur (S) n.k. Virutubisho vyote hivi ni muhimu kwa
ukuaji wa mmea. Tumia mbolea hizi za maji pamoja na zile za chumvi chumvi kwa
pamoja.
KUDHIBITI WADUDU WAHARIBIFU NA
MAGONJWA
A: WADUDU WAHARIBIFU
1. Aphids (Vidukari mafuta)
Hawa ni wadudu wadogo wanaovamia mazao mengi ya mboga mboga
ikiwemo pilipili. Wanakua na rangi ya kijani, kahawia au nyeusi, baadhi wana
mabawa na wengine hawana. Wadudu hawa ni wadogo sana lakini wanaonekana kwa
macho.
Picha: Aphids (Vidukari mafuta)
Athari
- Hufyonza majimaji yenye chakula kwenye mmea hususani
nchini ya majani machanga na matawi.
- Wakizidi sana husababisha mmea kudumaa na kupunguza kutoa
matunda, kwa sababu huwa wengi sana maeneo yanayotoa maua au matunda.
- Hutoa uteute kama unato (mafuta) ambao baadae huvunda na
kutengeneza ukungu ambao huathiri uwezo wa jani wa kujitengenezea chakula,
ukiwa kwenye matunda hupunguza hadhi ya soko ya tunda hilo.
- Wanavyofyonza majimaji hayo yenye chakula kutoka mmea
mmoja hadi mwingine, husambaza ugonjwa virusi kama 'TMV' (Tobacco Mosaic
Virus).
Namna ya kuwadhibiti
- Panda mahindi kuzunguza mipaka ya shamba lako kabla ya
kupanda pilipili zako, hii itasaidia kutowavutia wadudu hawa kusogea shambani
na kuvamia pilipili.
- Kama utaamua kutumia dawa za kemikali basi hakikisha
unatumia dawa ambazo haziui wadudu rafiki kama 'Predatory beetles', wadudu hawa
rafiki hula wadudu hawa, kwa hiyo husaidia kupunguza idadi yao. Pia dawa
zingine huua wadudu rafiki wanaochavusha maua, hali itakayopelekea kupunguza
idadi ya matunda. Kumfahamu mdudu huyu tazama picha hapo chini;
Picha: Predatory beetles (Lady bird beetle)
Pia hakikisha unatumia dawa hizo
kwa kufwata maelekezo ya kibandiko cha chupa ya dawa pamoja na maelekezo ya
wataalamu wa kilimo.
2. Crickets
Wadudu hawa hufanana na panzi wadogo, isipokua hawa wana
mwili mkubwa na wana rangi nyeusi. Wadudu hawa huishi kwenye mashimo ya kwenye
udongo karibia na mmea wa pilipili uliopo shambani na kwenye kitalu.
Picha: Crickets Photo Credit: www.thedailygardener.com
Athari
- Wadudu hawa hufanya mashambulizi wakati wa usiku kwa
kukata miche michanga na kuivutia ndani ya mashimo yao kwa ajili ya chakula,
hali hii huharibu na hupunguza idadi ya miche, Wakati wa mchana wanajificha
kwenye mashimo yao.
Namna ya kuwadhibiti
- Wadudu hawa hudhibitiwa wakati wa kuandaa shamba, hususani
wakati wa kufyeka nyasi au vichaka pamoja na kulima. Baada ya kulima shamba
liache likae kwa muda kidogo wakati huo unaandaa kitalu, mpaka miche ikifikia
kupandikiza, wadudu hawa watakua wameliwa na ndege au mijusi.
- Kwa upande wa kitalu, kama eneo lako lina kiwango kikubwa
cha wadudu hawa, tumia matrei au ndoo zenye udongo ambazo utaziweka juu ya kitu
fulani au meza, au unaweza ukafunika kitalu chako na neti.
3. Cucumber beetle
Wadudu hawa huathiri sana kipindi cha awali cha ukuaji wa
pilipili. Mdudu huyu ana rangi ya njano iliyochangamana na kijani na ana
michilizi myeusi mgongoni pia hufikia urefu wa ¼ inchi (mm 6).
Picha: Cucumber beetle Photo Credit: www.extension.msstate.edu
Picha: Cucumber beetle Photo Credit: www.entnemdept.ufl.edu
Athari
- Wadudu hawa hutoboa matundu madogo kwenye majani, hali
inayopelekea kupunguza ufanisi wa jani kutengeneza chakula.
- Kiwavi wa mdudu huyu huharibu mizizi ya pilipili.
- Wadudu hawa husambaza ugonjwa wa 'mnyauko bakteria'
(Bacterial wilt) na baadhi ya magonjwa ya virusi (Mosaic viruses).
Namna ya kuwadhibiti
- Ondoa magugu kuzunguka mipaka ya shamba na ndani ya shamba
la pilipili.
Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo
إرسال تعليق