Namna ya kutengeneza chakula cha kuku wa kisasa (Kuku wa nyama na wa mayai) - Sehemu ya Kwanza


SEHEMU YA KWANZA

Habari ndugu wasomaji wangu?, Leo nimekuja na maada inayohusu namna ya kuchanganya chakula cha kuku wa kisasa yaani wa mayai na wa nyama.

Chakula cha kuku kinachangia gharama ya uzalisaji kwa asilimia 80%. Ikiwa mfugaji ataweza kujitengenezea chakula hicho, ataweza kupunguza gharama hizo hadi kufikia asilimia 50 hadi 60%, hali hii itamfanya apate faida na kurudisha gharama za uzalishaji.

Muhimu ni kwamba inatakiwa mfugaji azingtie ubora wa malighafi wakati wa uchanganyaji, ukitumia maligafi zisizo na ubora utasababisha kuku wako kudumaa. Rai yangu ni kwamba kama utaona kuna ugumu wa wewe kutengeneza chakula hicho basi ni bora ukanunue kwenye makampuni yanayozingatia ubora wa uchanganyaji.

Vyakula visivyo na ubora husababisha kuku kudumaa na kupunguza kiwango cha kutaga mayai, magonjwa na hata vifo vya kuku. Kwa mfugaji kujitengenezea chakula cha kuku ni mojawapo ya njia za kuzingatia ubora wa chakula hicho pamoja na kupunguza gharama za uzalishaji. Mbali na mfugaji kujitengenezea chakula cha kuku, inatakiwa ubora wa malighafi za kutengenezea uzingatiwe sana.

Malighafi zinazotumika mara nyingi katika utengenezaji wa vyakula hivi ni pamoja na Mahindi yasiyokobolewa (Whole maize), Pumba za mahindi, Mashudu ya pamba, Maharage ya soya (Soya), Mashudu ya alizeti, Unga wa samaki au dagaa n.k.

Mbali na malighafi hizo nilizozieleza inatakiwa mfugaji aongeze virutubisho vingine na madini mbalimbali ili kuwapa kuku mchanganyiko wa chakula chenye virutubisho kamili.

Kuna fomula maalumu ya kutengenezea chakula cha kuku, Fomula hiyo inaitwa 'Pearson Square method'. Fomula hii inahusisha matumizi ya kiwango muhimu cha protini kwenye vyakula kinachoitwa 'Digestible Crude Protein' (DCP). Kirutubisho hiki ni muhimu sana kufahamu kiwango chake wakati wa utengenezaji wa vyakula vya kuku ama wanyama mbalimbali.

Vifuatavyo ni viwango vya kirutubisho hiki 'DCP' kwenye malighafi mbalimbali za kutengenezea vyakula vya kuku au wanyama mbalimbali;

Mahindi yasiyokobolewa = 8.23%
Soya = 45%
Unga wa samaki au dagaa = 55%
Pumba za mahindi = 7%
Mashudu ya alizeti = 35%

Mbali na kufahamu viwango hivyo vya DCP, kuna hatua nyingine ya kupata mgawanyo wa virutubisho kulingana na uhitaji wa kiwango cha protini kwa umri husika wa kuku au mnyama.

Sasa basi tuachane na mahesabu hayo, nimekurahisishia namna ya kuchanganya vyakula hivi kwa uwiano rahisi na utakaoeleweka vyema. Uwiano ni kuchanganya malighafi hizo mbalimbali kwa kiwango kilichopigiwa mahesabu tayari. Viwango hivyo vikishachanganywa vinafikia uzani wa kilo 100 kwa kila mchanganyiko ulio kamili.

Ufuatao ni mchanganuo wa uzani wa uchanganyaji kulingana na umri wa kuku, viwango hivi vimeshapigiwa mahesabu tayari ni kitendo tu cha mfugaji kununua malighafi zenye ubora na kuchanganya kwa kutumia viwango hivi.


A: KUKU WA MAYAI (LAYERS CHICKEN)
1. Kutengeneza chakula cha vifaranga wa wiki 1 hadi 4 (Chick mash)
Vifaranga wa kuku wanahitaji kiwango cha protini muhimu (Digestible Crude Protein) kuanzia asilimia 18 hadi 20%. Mchanganuo ufuatao hutengeneza uzani wa kilo 100 za chakula.

Mahindi Kilo 48
Pumba za ngano  Kilo 13
Mchanganyiko wa pumba za ngano na unga wa ngano (Pollard) Kilo 10
Alizeti Kilo 24
Unga wa samaki/dagaa Kilo 2
Chokaa Kilo 2.5

Vionjo (Additives)
Chumvi Gramu 40 (Kilo 0.04)
Premix Gramu 30 (Kilo 0.03)
Tryptophan Gramu 100 (Kilo 0.1)
Lysine Gramu 4 (Kilo 0.004)
Methionine Gramu 14 (Kilo 0.014)
Threonine Gramu 90 (Kilo 0.09)
Enzymes Gramu 70 (Kilo 0.07)
Coccidiostat Gramu 82 (Kilo 0.082)
Toxin binder Gramu 70 (Kilo 0.07)

Jumla Kilo 100.00

2. Kutengeneza chakula cha kuku wa wiki 4 hadi 18 (Growers mash)
Kuku hawa wanaokua wanahitaji kiwango cha protini muhimu (Digestible Crude Protein) kuanzia asilimia 16 hadi 18%. Mchanganyiko huu wa chakula husababisha kuku kukua kwa haraka sana, ikiwa ni maandalizi ya kuelekea umri wa kutaga.

Mchanganuo:
Mahindi Kilo 14
Pumba za mahindi Kilo 24
Mchanganyiko wa pumba laini za ngano na unga kiasi wa ngano (Pollard) Kilo 19
Pumba za ngano Kilo 14
Mashudu ya pamba Kilo 8.9
Mashudu ya alizeti Kilo 7
Unga wa soya Kilo 5
Chokaa Kilo 3
Unga wa mifupa Kilo 1
Unga wa samaki au dagaa Kilo 4

Vionjo (Additives)
Chumvi Gramu 37.2 (Kilo 0.0372)
Coccidiostat Gramu 1.4 (Kilo 0.0014)
Premix Gramu 50 (Kilo 0.05)
Zinc bacitracitrach Gramu 1.4 (Kilo 0.0014)
Mycotoxin binder Gramu 10 (Kilo 0.01)

Jumla Kilo 100.00



Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

1 تعليقات

  1. kama kuku wamayai akikula vizuri anapashwa kutaga mayaii ngapi kwasiku

    ردحذف

إرسال تعليق

أحدث أقدم