Namna ya kutengeneza chakula cha kuku wa kisasa (Kuku wa nyama na wa mayai) - Sehemu ya Pili


SEHEMU YA PILI

3. Kutengeneza chakula cha kuku wa wiki 18 na kuendelea (Layers Mash)
Chakula cha kuku wanaoanza kutaga huwa na kiwango muhimu cha Protini (Digestible Crude Protein) kuanzia asilimia 16 hadi 18. Chakula hicho ni muhimu kikawa na madini ya Calcium (Chakula chenye chokaa) kwa ajili ya utengenezwaji wa magamba ya mayai. Kuku ambao wana kiwango kidogo cha calcium hutumia akiba ya madini haya ya calcium iliyopo kwenye mifupa yao kutengenezea magamba ya mayai. Anza kuwapa kuku chakula hiki wakifikia umri wa wiki 18.

Mchanganuo:
Mahindi Kilo 48
Soya Kilo 17
Unga wa samaki au dagaa Kilo 11.3
Pumba za mahindi, Mpunga au Ngano Kilo 14.13
Chokaa (zina madini ya calcium) Kilo 9

Vionjo (Additives)
Premix Gramu 200 (Kilo 0.2)
Lysine Gramu 100 (Kilo 0.1)
Methionine Gramu 50 (Kilo 0.05)
Threonine Gramu 100 (Kilo 0.1)
Tryptophan Gramu 50 (Kilo 0.05)
Toxin binder Gramu 70 (Kilo 0.07)

Jumla Kilo 100.00

B: KUKU WA NYAMA (BROILERS)
Kuku wa nyama (Broilers) huwa na mahitaji tofauti ya vyakula vya nguvu, Protini na Madini kwa kila hatua ya ukuaji. Inampasa mfugaji atumie uwiano mzuri wa malighafi bora za chakula ili kupata uzalishaji mkubwa.

Kuku wa nyama wakiwa na umri mdogo huhitaji kiasi kikubwa cha protini kwa ajili ya kutengeneza misuli, manyoya n.k. Jinsi kuku wa nyama wanavyozidi kukua mahitaji ya nguvu kwa ajili ya kutunza mafuta mwilini huongezeka, wakati huohuo mahitaji ya protini hupungua.

Kwa hiyo kuku hawa wanahitaji kiasi kikubwa cha protini kipindi cha awali cha ukuaji kuliko kipindi ambacho wakiwa wakubwa.

Vyakula vya kuku hawa wa nyama lazima viwe na kiwango cha protini muhimu (Digestible Crude Protein 'DCP') kuanzia asilimia 22 hadi 24%, mchanganuo wa uwiano wa vyakula hivi ni kama ifuatavyo;

1. Kutengeneza chakula cha vifaranga wa nyama umri wa siku 1 hadi 21 (Broiler starter)
Wapatie kuku wako chakula hiki kwa siku 21, kila kuku atakula chakula kiasi cha Kilo 1 kwa siku hizo 21.

Mchanganuo:
Mahindi Kilo 57
Unga wa samaki au dagaa Kilo 17.1
Unga wa Soya Kilo 20
Chokaa Kilo 5.7

Vionjo (Additives)
Premix Gramu 100 (Kilo 0.1)
Lysine Gramu 50 (Kilo 0.05)
Threonine Gramu 50 (Kilo 0.05)

Jumla Kilo 100.00

2. Kutengeneza chakula kuku wa nyama kuanzia siku ya 21 hadi 42 (Broiler Finisher)
Wapatie kuku wako chakula hiki kwa awamu mbili, awamu ya kwanza wapatie kwa siku 14 yaani kuanzia siku ya 21 hadi siku ya 35  na awamu ya pili na ya mwisho kwa siku 7 kuanzia siku ya 35 hadi 42.

Mchanganuo:
Mahindi Kilo 14.3
Pumba za mahindi Kilo 24
Mchanganyiko wa pumba laini za ngano na unga kiasi wa ngano (Wheat Pollard) Kilo 19.3
Pumba za ngano Kilo 14
Mashudu ya pamba Kilo 8.6
Mashudu ya alizeti Kilo 7
Unga wa samaki au dagaa Kilo 4.3
Chokaa Kilo 3
Unga wa soya Kilo 5.4
Unga wa mifupa Gramu 60 (Kilo 0.06)

Vionjo (Additives)
Grower Premix Gramu 19 (Kilo 0.019)
Chumvi Gramu 7 (Kilo 0.007)
Coccidiostat Gramu 7 (Kilo 0.007)
Zincbacitrach Gramu 7 (Kilo 0.007)

Jumla Kilo 100.00


Muhtasari wa kulisha kuku wa nyama

Siku ya 1 hadi 21: Wapatie Starter Mash. Kila kuku atakula chakula kiasi cha Kilo 1 kwa siku hizo 21

Siku ya 21 hadi 35: Wapatie Finisher Mash. Kila kuku atakula chakula kiasi cha kilo 2 kwa siku hizo 14

Siku ya 35 hadi 42: Wapatie tena Finisher Mash. Kila kuku atakula chakula kiasi cha kilo 1 kwa siku 7.

ILANI:
Ili kuhakikisha kwamba kuku wako hawapati mshituko wa kubadilisha chakula inatakiwa ubadilishe chakula taratibu kwa mfumo ufuatao;

Siku ya 20: Changanya chakula, Starter Mash asilimia 75% na Finisher mash asilimia 25%

Siku ya 21: Changanya chakula, Starter Mash asilimia 50% na Finisher asilimia 50%

Siku ya 22: Changanya chakula, Starter Mash asilimia 25% na Finisher Mash asilimia 75%

NB:
Kuku wako wa nyama huwa tayari kuliwa au kuuzwa wakifikia umri wa siku 35 hadi 42, hufikia uzani wa kilo 1.5

Kwa mfugaji mwenye kuku zaidi ya 500 inatakiwa aandae chakula kiasi cha Tani 1 (Kilo 1000) kwa mara moja. Kiasi hicho cha tani 1 huwa ni jumla ya viroba 10 vya chakula vyenye kilo 100 kila kimoja sawa na mchanganuo wa utengezaji wa chakula nilioueleza hapa juu.

Ili kutengeneza tani moja hiyo ya chakula, fanya hivi; kwa kila aina ya chakula cha kuku wa mayai au wa nyama zidisha kila aina ya malighafi kwa 10. Jambo lingine muhimu ni kwamba chakula utakachotengeneza kitumike kwa mwezi mmoja tu si zaidi ya hapo. Hii itahakikisha chakula kinabaki salama wakati wote kwa afya za bora za kuku wako. Chakula ulichotengeneza kikikaa zaidi ya mwezi mmoja hupungua ubora hivyo huatarisha afya za kuku wako.


Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

2 تعليقات

إرسال تعليق

أحدث أقدم