Kilimo Bora cha Pilipili kichaa - Sehemu ya Nane (Growing Chili pepper - Part Eight)


KILIMO CHA PILIPILI KICHAA SEHEMU YA NANE

4. Pepper hornworm
Huyu ni kiwavi mwenye muonekano wa kama pembe kichwani, ndio maana wakamuita 'Hornworm'. Kiwavi huyu ni mkubwa hufikia urefu wa sm 9 na upana wa sm 1.3, hujificha chini ya majani wakati wa mchana.

"Tobacco Hornworm" flickr photo by OpCit  shared under a Creative Commons (BY) license

Athari
- Viwavi hawa hutafuna majani ya pilipili, wakati wachana unaweza usiwaone, ila utagundua kama wapo baada ya kuona vipande vya majani vilivyoanguka chini.

Namna ya kuwadhibiti
- Unaweza kuwaondoa kwa mkono na kuwaua, hususani kama shamba lako ni dogo.
- Pia wadudu hawa wanaweza wakapunguzwa na ndege pamoja mdudu anaeitwa 'Parasitic wasps', tazama picha hapo chini kumfahamu


- Tumia dawa za kemikali zinazopatikana kwenye maduka ya pembejeo za kilimo, ila hakikisha unatumia dawa zisizoua wadudu rafiki, pia kumbuka kutumia dozi sahihi ya dawa kama ilivyoandikwa kwenye kibandiko cha chupa ya dawa pamoja na kufwata ushauri wa wataalamu wa kilimo.

5. Mites
Hawa ni wadudu wadogo sana wanaofanana na buibui, nao hutengeneza utando kama walivyo buibui wa kawaida. Huwa na rangi nyekundu, njano au kijani, wadudu hawa huvamia majani pamoja na maeneo mengine ya mmea. Wakiwa wachache huwezi kuwagundua, ila wakiwa wengi utawagundua baada ya kuona majani yamebadirika rangi na kuwa njano, utakaposogea karibu na kuchunguza utaona mkusanyiko wa wadudu hawa wakiwa wametengeneza utando wao.

Picha: red spider mites        Photo Credit: www.nature-and-garden.com


Athari
- Majani hubadirika rangi na kuwa ya njano pamoja na kujikunja, pia jani huharibika muonekano wake pamoja na majani mengine kupukutika. Pia na matawi nayo huharibika.
- Mmea hupukutisha maua na matunda yaliyotoka hayakui vizuri.
- Athari ikizidi mmea hudumaa.

Namna ya kuwadhibiti
- Udhibiti wa wadudu hawa huanzia kwenye hatua za awali za ukuaji wa mmea hususani kwenye kitalu mpaka shambani, Chunguza kwa makini kwenye kitalu ili kubaini uwepo wa wadudu hawa vilevile wakati wa kupandikiza, mmea wowote utakaonekana una wadudu hawa uondoe taratibu kisha uchome moto. Ni muhimu kuiondoa taratibu mimea yenye wadudu hawa kwasababu, wadudu hawa ni rahisi kuhama kutoka mmea mmoja hadi mwingine kwa kushika mmea, pia kwenye nguo au upepo.

- Badirisha mazao kwa kupanda mazao tofauti na yale yanayovamiwa na wadudu hawa kama mazao ya nafaka ikiwemo mahindi, mtama n.k au mazao ya mafuta kama alizeti. Mazao mengine yanayovamiwa na wadudu hawa ni pamoja na Viazi vitamu, Viazi mviringo, Nyanya, Kunde, Maharage, Miembe, Michungwa, Miparachichi, Kahawa, Mipapai na Mipera. Hakikisha unapanda pilipili kwenye maeneo ambayo hakuna mazao niliyoyaorodhesha hapo juu, pia wakati wa kubadirisha mazao panda aina tofauti na mazao hayo.

- Pia unaweza ukatumia dawa za kemikali zinazopatikana kwenye maduka ya pembejeo za kilimo. Sharti, tumia dawa hizo kwa kufwata ushauri wa kitaalamu.

6. Nematodes (minyoo fundo)
Hawa ni minyoo wadogo sana (microscopic eelworms) waishio kwenye udongo, hutegemea mizizi ya pilipili kuishi.

Picha: Root knot nematodes

Athari
- Minyoo hawa husababisha vivimbe vidogo vidogo kwenye mizizi na kusababisha mizizi kuharibika kabisa. Hali hii hupunguza uwezo wa mizizi kufyonza maji na virutubisho kutoka kwenye udongo.
- Athari ikizidi mmea hunyauka, utagundua hali hii pale unapoona udongo wa shamba lako una unyevu wa kutosha lakini baadhi ya mimea inanyauka na kufa.

Namna ya kudhibiti
- Andaa kitalu chako vizuri kwa kuchanganya udongo wa kitalu na mbolea ya samadi iliyooza vizuri. Mbolea isiyooza vizuri au mbichi ndio chanzo cha minyoo hawa, kumbuka, tatizo la minyoo hawa huanzia kwenye kitalu. Kurejea sehemu ya awali ya makala hii kuhusu namna nzuri ya kuandaa kitalu chako BOFYA HAPA.
- Badirisha mazao kwa kupanda mazao mengine tofauti na mazao ya mbogamboga kama; Mazao ya nafaka kama mahindi, mtama n.k au mazao ya mafuta kama Alizeti.
- Ukishaandaa shamba lako na kulilima vizuri, usipande bali liache lipigwe na jua kwa mwezi mmoja au zaidi, ndipo baada ya hapo upandikize miche yako. Mwanga wa jua ni tiba husaidia kuua vimelea mbalimbali kwenye udondo ikiwa ni pamoja na minyoo hawa. Ili kufanikisha hili unaweza ukaandaa shamba lako mapema kabla ya kitalu, mpaka miche inafikia kupandikizwa, shamba lako litakua limepata mwanga wa jua kwa kiwango cha kutosha.

NB:
Hawa ni baadhi tu ya wadudu wanaoathiri zao la pilipili/pilipili kichaa, kuna wadudu wengine wengi pia ambao huathiri zao hili kama; Pepper budworm, Thrips, Corn earworm, Pepper weevil, Fruit fly, Pepper maggot na Tropical white mite. Kipindi kijacho nitaleta maelezo ya kina kuhusiana na wadudu hawa na namna ya kuwadhibiti.



Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

أحدث أقدم