Kilimo bora cha Mpunga - Sehemu ya Kwanza (Growing Paddy - Part One)


KILIMO CHA MPUNGA SEHEMU YA KWANZA

Zao la mpunga, Rice (Oryza sativa) hupandwa maeneo mengi nchini Tanzania, Afrika mashariki, Afrika na ulimwenguni kote kwa ujumla. Zao hili hutumika kama chakula. Mchele una wanga wa kutosha hivyo hutumika kwa namna nyingi kama kutengenezea keki, vitumbua, supu, kifungua kinywa, kuliwa kama wali, pilau n.k. Baadhi ya nchi zingine kama Japan mchele hutumika kutengenezea pombe aina ya waini inayoitwa “Saki”. Vilevile mashina ya mpunga huweza kutumika kwa kuezekea nyumba, kulishia mifugo n.k.

AINA
Mpunga unaolimwa hapa afrika ikiwemo Tanzania upo wa aina mbili;

1) Mpunga uliotoka bara la Asia (Oryza sativa) - aina hii hupandwa maeneo mengi na hupendwa sana
2) Mpunga uliotoka bara la Afrika (Oryza glaberrima)

Pia zao la mpunga huweza kugawanywa katika makundi manne kulingana na kiwango cha uwepo wa maji (water regimes) kama;

1) Mpunga wa kumwagiliwa (irrigated)
2) Mpunga unaotegemea mvua (maeneo ya bondeni)
3) Mpunga unaotegemea mvua (maeneo ya mwinuko)
4) Mpunga unaopenda maeneo yenye kufurika maji (flood prone)

MAZINGIRA
Zao la mpunga hupendelea ardhi yenye maji ya kutosha au maji yaliyofurika katika wakati wote wa ukuaji wake. Joto linalotakiwa kwa ukuaji wa zao hili ni kuanzia nyuzijoto 20ºC hadi 37.7ºC, joto chini ya nyuzi joto 10ºC mmea hushindwa kufanya kazi na ukuaji wa mmea husimama. Pia zaidi ya nyuzijoto 38ºC uzalishaji wa mmea hupungua.

Kiwango cha tindikali ya udongo kinachohitajika kwa uzalishaji wa mpunga ni kuanzia Ph 5.0 hadi 7.0, ingawaje pia mpunga unaweza ukafanya vizuri kwenye udongo wenye tindikali kuanzia pH 3 hadi 10. Zao hili hufanya vizuri kwenye muinuko kuanzia m 0 hadi m 2500 kutoka usawa wa bahari, ingawaje maeneo mengi duniani mpunga huzalishwa maeneo ya mabonde na yenye unyevu wa kutosha. Kiasi cha mvua kinachohitajika ni kuanzia mm 800 hadi mm 2000 kwa mwaka, ikiwa kiasi cha mvua kikawa chini ya mm 1250 kwa mwaka lazima itumike njia ya umwagiliaji ili kufidia mapungufu ya maji.

Zao hili huvumilia udongo wenye chumvi katika hatua fulani za ukuaji, katika hatua ya uotaji kunakua hakuna shida ila sio nzuri wakati miche imekua. Zao hili hupendelea udongo unaotunza maji, shamba la kupanda mpunga linatakiwa liwe tambalale ili kuruhusu kufurisha maji. Kwa namna hii unaweza kuligawanya shamba lako kwenye majaruba ili kutengeneza vijishamba vyenye ardhi tambalale.

KUANDAA MICHE NA KUPANDA
Zao la mpunga huanza na kuandaa miche ambayo baadae hupandikizwa shambani, ili kupata miche bora zingatia yafuatayo;

1. Kuchagua mbegu bora
Chagua mbegu zenye ujazo na zenye afya

2. Kutibu mbegu kabla ya kupanda
Njia hii husaidia kuua na kukinga mbegu dhidi ya wadudu waharibifu au magonjwa yaliyopo ndani ya mbegu au kwenye udongo, utaratibu huu huhakikisha mbegu zinaota vizuri na kupatikana miche bora. Zifuatazo ni njia bora za kuzitibu mbegu kabla ya kupanda;

a) Kutibu mbegu kwa maji ya moto (Hot water treatment)
Njia hii hutumika kwa mazao mengi ikiwemo mpunga, loweka mbegu za mpunga kwenye maji ya moto yenye joto la nyuzijoto 38ºC kwa muda wa dakika 10, baadae zitoe kwenye maji kisha zikaushe ndani kwenye nyuzi joto 21ºC hadi 23ºC. Wakati wa kukausha zitandaze mbegu hizo juu ya karatasi kavu. Njia hii husaidia kuua minyoo wadogo wanaoitwa nematode (Aphelenchoides besseyi), minyoo hawa husababisha ugonjwa unaoitwa ‘white tip disease’

b) Koloweka mbegu kabla ya kupanda (Seed soaking)
Njia hii hufanywa kwa kuloweka mbegu kwenye maji ya baridi kwa muda wa masaa 24 (siku moja), ili kupunguza muda wa kuota na kuoza mara zitakapopandwa. Wakati wa kuloweka mbegu badirisha maji ili kuondoa sumu na kuruhusu hewa safi. Usiloweke mbegu zaidi ya masaa 48 (siku mbili), kwani mbegu zitaoza. Baada masaa 24 zipande mbegu hizo mara moja, ukichelewa zitaoza.

c) Kuotesha mbegu (Pre-sprouting)
Njia hii mbegu huwekwa kwenye maji na kutolewa, baadae hufunikwa na majani makavu kwa masaa 24 hadi 48, hii itasaidia kuwa na uotaji uliosawa. Epuka kuotesha muda mrefu zaidi ya masaa 48.

3. Kuandaa kitalu
Andaa vizuri kitalu kama ifuatavyo;

a) Lima vizuri eneo lako utakaloandaa kitalu angalau wiki 2 kabla ya kupanda na kufurisha maji (flooding)

b) Chabanga vizuri eneo hilo wiki moja kabla ya kupanda ili kuondoa mabonge mabonge na kutengeneza udongo laini.

c) Punguza maji kwenye eneo hilo siku moja kabla ya kupanda ili kubaki na udongo tifutifu wenye maji kiasi; ikiwa ukapanda kwenye udongo wenye maji mengi na tope, mbegu zitafukiwa kwenye tope na hazitaota.

d) Eneo la kitalu lenye ukubwa wa m2 350 huzalisha miche itakayotosha kupandikiza shamba lenye ukubwa wa hekta 1 (ekari 2.5).

4. Kupanda mbegu kwenye kitalu
Baada ya kuandaa kitalu panda mbegu zako kwa kuzirusha na kuzitawanyisha vyema kwenye eneo la kitalu (Broadcasting). Kiasi cha mbegu kinachohitajika kwa m2 1 ni gramu 80 hadi 100, kwa ekari moja ni Kilo 20, kwa hekta moja ni Kilo 50.

Baada ya kupanda usimwagilie maji papo hapo, subiri baada ya siku chache ndipo umwagilie maji ili kuongeza unyevu, ila yasiwe yasiwe maji ya kufurika (flooding). Baada ya mbegu kuota na kuchomoza endelea kuongeza maji kidogo kidogo kuanzia kina cha sm 1 hadi 3 kulingana na ukuaji wa miche.

Miche huwa tayari kupandikizwa baada ya wiki 3 hadi 4 tangu kupanda, itategemeana na mwanga wa jua, joto na aina ya mbegu.

Makala na: Lusubilo A. Mwaijengo

Post a Comment

Previous Post Next Post